HI NI NEEMA, MMOJA YANGA AMWAGIWA MIFEDHA
MSHAMBULIAJI wa Yanga raia wa Uganda, Juma Balinya Jumamosi iliyopita alioga noti kutoka kwa viongozi na mashabiki wa timu hiyo waishio Botswana na nchi jirani.
Hiyo ni baada ya kufunga bao pekee la dakika 40 alilolifunga kwa njia ya faulo nje kidogo ya 18 baada ya yeye mwenyewe kuchezewa vibaya na beki wa Township Rollers.
Bao hilo lilitosha kuiwezesha timu yake kufuzu hatua ya Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Botswana ambao ulimalizika kwa Yanga kushinda bao 1-0.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu na kuthibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, mshambuliaji huyo alimwagiwa fedha hizo kama pongezi baada ya bao lake safi alilolifunga.
Mwakalebela alisema kuwa fedha hizo alipewa mara baada ya mchezo huo kumalizika kutokana na mashabiki hao kumfuata kwenye vyumba vya kubadilishia nguo uwanjani hapo huku wengine wakimfuata hotelini na kumpatia fedha hizo.
Aliongeza kuwa uongozi pia umepanga kuwapatia fedha wachezaji na benchi lote la ufundi kama motisha ya kuongeza bidii katika michezo inayofuata ya michuano hiyo ya kimataifa na kitaifa.
“Kiukweli wachezaji wote walistahili pongezi kutokana na kiwango cha kila mchezaji ambacho amekionyesha uwanjani na kufanikiwa kufuzu Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Ushindi huo umepokelewa vizuri na mashabiki waishio
Botswana na nchi za jirani ikiwemo Afrika Kusini ambao walifuraishwa na bao la Balinya na kushawishika kumtunza fedha mara baada ya mchezo huo.
“Balinya alipata fedha nyingi kutoka kwa mashabiki hao, pia kama uongozi umepanga kutimiza ahadi yake ya kuwapa mamilioni wachezaji na benchi la ufundi baada ya kufanikiwa kufuzu hatua inayofuatia ya michuano hii mikubwa Afrika kwa kuwafunga nyumbani kwao Rollers,” alisema Mwakalebela.
BALINYA AFUNGUKA
Akizungumza baada ya mchezo huo, Balinya alisema nguvu ya kupambana waliyoionyesha katika mchezo wao na Township Rollers huko Botswana ndiyo hiyo watakayoingia nayo katika mechi zao za ligi kuu.
“Tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kupata matokeo ya ushindi dhidi ya Township Rollers, mechi hiyo imetuwezesha kusonga mbele katika hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Hata hivyo, kinachofuatia sasa ni nguvu hii kwenda kuitekeleza pia katika mechi zetu za ligi kuu ili kuhakikisha tunafanya vizuri na kutimiza lengo letu la kuwa mabingwa,” alisema Balinya.
Ikumbukwe kuwa keshoa Jumatano, kikosi cha Yanga kitashuka uwanjani kukipiga dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa ligi kuu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
0 COMMENTS:
Post a Comment