KOCHA SIMBA AJA NA MALENGO MENGINE YA KITOFAUTI MSIMU HUU
Kocha wa Simba, Patrick Aussems amesema ili aweze kutetea kibarua chake ndani ya kikosi hicho amepanga kutwaa mataji manne ambayo yatapoza hasira za mabosi wake na mashabiki wa timu hiyo baada ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha huyo amepanga kutwaa mataji hayo baada ya hivi karibuni kikosi hicho kutupwa nje kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na UD do Songo ya Msumbiji kwa sheria ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Mataji ambayo Aussems anayataka ni Ligi Kuu Bara, Kombe la SportPesa, Kombe la Shirikisho (FA) na Kombe la Mapinduzi.
Aussems ameliambia Championi Ijumaa, kuwa kwa sasa hesabu zake zote ni kuhakikisha kwamba anatetea ubingwa wa ligi ikiwa ni sehemu ya kipengele cha mkataba wake pamoja na kuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo ikiwa ni baada ya kushindwa kutimiza moja ya malengo ambayo wamejiwekea kwa msimu huu.
“Kitu kilichopo mbele yangu kwa sasa ni kuona hatufanyi tena yale yaliyojitokeza katika mechi yetu ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Tulitarajia kufika mbali lakini hesabu zikagoma.
“Kwa sasa malengo yangu ni kutwaa kila taji na sitanii kwenye hilo, ninajua nitafanikisha baada ya kutolewa huku kwenye Ligi ya Mabingwa,” alisema Aussems.
0 COMMENTS:
Post a Comment