Ligi Kuu Tanzania Bara imeshaanza kutimua vumbi mabingwa watetezi ambao ni Simba wanaanza rasmi kazi yao Agosti 29 kwa kuanza kazi mbele ya JKT Tanzania.
Kazi kubwa
ambayo wanayo ni kutetea kombe lao walilonalo mkononi huku ushindani ukitajwa
kuwa mkubwa kutokana na timu nyingi kujipanga.
Miongoni mwa
nyota wapya ambao wamesajiliwa msimu huu na kushtua kidogo ndani ya Simba ni
aliyekuwa nahodha wa Yanga Ibrahim Ajibu ambaye amesaini kandarasi ya miaka
miwili.
Uwezo wake
kwa msimu wa mwaka 2018-19 anashikilia rekodi ya kutoa pasi nyingi za mabao
akiwa amefanya hivyo mara 17 na alifunga mabao 6.
Hesabu zake kwa sasa ndani ya klabu yake mpya zipo namna hii:-
Kwa nini Simba?
“Hakuna
mchezaji anayeweza kuchagua kambi, nilikuwa Simba awali kabla ya kuibukia Yanga
na sasa nimerejea Simba hakuna tatizo lolote.
“Kikubwa ni
kubaki kwenye maisha yangu ya soka na kuendelea kucheza soka kwani maisha
lazima yaendelee siku zote.
Dili la TP Mazembe limeishaje?
“Nilizungumza
nao awali nikaona dili lao ni la kawaida, hivyo haikuwa na ulazima mimi kusaini
sehemu ambayo sina maslahi mazuri.
“Nilitazama
dili la Simba nikagundua kwamba lipo vizuri nikaamua kusaini hivyo wakati
mwingine tutajua yatakayotokea mbele.
Ushindani wa namba?
“Hauwezi
kufikiria ushindani wa namba kwa sasa, hakuna sehemu
ambayo hakuna ushidani wa namba kila timu hilo lipo hata kule nilikokuwa
kulikuwa na ushindani na ndio maana kuna wakati nilianza benchi ama nilipokuwa
sipo sawa kuna wachezaji walicheza.
“Sina hofu
na benchi kwani kazi ya kupanga kikosi ni ya kocha yeye ndiye anayeamua nani
aanze na nani akae benchi, jitihada na kujituma ndicho ninachofikiria.
Mipango ndani ya Simba?
“Siwezi
kufanya mipango peke yangu ni lazima nishirikiane na wachezaji wenzagu, wakati
huu tunaamini tutakuwa bora na tutafanya mambo makubwa.
“Kitu
kikubwa ambacho mashabiki wanahitaji ni matokeo hivyo tutafanya kazi kubwa
kupata matokeo chanya wakati wa ligi na mashindano mengine.
Mashabiki wa Yanga unawaambia nini?
“Maisha ya
mpira yanabadilika, mchezaji kuhama ni jambo la kawaida kwa kuwa ni kazi yake,
walikuwa nasi bega kwa bega na walitupa sapoti nami ninawashukuru kwa hilo.
“Kwa sasa
nipo sehemu nyingine haina maana kwamba tunakuwa maadui bado sisi ni marafiki
na shabiki atabaki kuwa shabiki hivyo wasikasirike katika hili haya ni maisha.
Rekodi yako je?
“Hicho ni
kitu ambacho kipo kwenye mipango, kila baada ya siku kuanza hesabu zangu ni
kuona kwamba ninafanya vema kwa manufaa ya timu na Taifa kiujumla hivyo muda
upo na rekodi zimewekwa ili zivunjwe.
Kipi kitakupa ushindi?
“Sishindani peke yangu, ushirikiano ambao utakuwa ndani ya timu ndio
utakaotupatia mafanikio na ushindi kwenye mashindano yetu ambayo tutashiriki.
Mashabiki wa
Simba unawaambia nini?
“Haraka haraka haina baraka walisema, hivyo ni muda wao wa kutulia wenyewe watanipenda kwani ninaamini tutafanya mengi makubwa.
“Simba ni timu
kubwa na ina wachezaji wengi wakubwa na kitakachotokea kitakuwa kikubwa
mashabiki wasiwe na hofu.
Usajili
uliofanywa je unauzungumziaje?
“wote wanastahili ndio maana wamesajiliwa, wengi nilikuwa nafanya nao kazi na wengine wametoka sehemu nyingine ila tofauti zote zinawekwa pembeni na kikubwa ni kazi,” anamalizia Ajibu.
0 COMMENTS:
Post a Comment