YONDANI AVUNJA UKIMYA, AAMUA KUFUNGUKA JUU YA KIWANGO CHA MGHANA
Beki mkongwe wa Yanga, Kelvin Yondani amekubali kiwango cha Mghana, Lamine Moro huku akipata matumaini ya kufanya vizuri kwenye msimu huu kutokana na ubora wa safu nzuri ya ulinzi.
Yondani alisema kuwa kwa kipindi kifupi amefurahishwa na aina yake ya uchezaji kuokoa na kupunguza hatari golini kwao, pia anavyokumbusha majukumu ya kila mchezaji uwanjani.
“Msimu uliopita tulikuwa na safu nzuri ya ulinzi, lakini msimu huu naona imeongezeka zaidi kwa kuanzia mabeki wa pembeni na kati, hiyo ni kutokana na usajili bora uliofanywa na viongozi,”alisema Yondani ambaye anaishi Kigamboni na mkewe na familia.
“Ni matarajio yangu kuona msimu huu tukifanya vizuri katika ligi na michuano ya kimataifa na hilo nimelithibitisha kwenye mchezo wetu wa Rollers ambao nilicheza pamoja na mabeki wapya katika kikosi cha kwanza
“Namzungumzia Lamine ambaye katika mchezo huu tulicheza vizuri kwa kuelewana na kuokoa hatari nyingi golini likiwemo bao lililokuwa linaelekea wavuni ambalo aliliokoa kwa kichwa, hiyo ni ishara tosha kuwa msimu huu ni wetu,” alisema Yondani ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba.
Yondani na safu yake ya ulinzi ataikabili Zesco ya Zambia katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa, wakivuka hapo wanakwenda kwenye makundi.
0 COMMENTS:
Post a Comment