MOTO utawake
leo uwanja wa Karume kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao utawakutanisha
mabingwa watetezi Simba ambao watakaribishwa na Biashara United kuzisaka pointi
tatu muhimu ndani ya Ligi Kuu Bara.
Simba imecheza jumla ya mechi tatu na kushinda
mechi zake bila kupoteza hata moja huku wenyeji Biashara United wakiwa
wamepoteza michezo mitatu na kujikusanyia pointi moja pekee kwani walipoteza
michezo mitatu na kutoa sare moja.
Biashara
United ilifungua kete yake ya kwanza kwa kupoteza mbele ya Kagera Sugar wakiwa
nyumbani kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar na wakapoteza mchezo wa
pili mbele ya Mbao FC kwa kufungwa bao 1-0 ugenini uwanja wa CCM Kirumba
wakaambulia sare mbele ya Alliance kwa kufungana bao 1-1 na kupoteza mchezo
wake wa nne mbele ya JKT Tanzania kwa kufungwa bao 1-0 uwanja wa Karume.
Simba wao
kwa sasa wameanza kuwasha moto ndani ya TPL kwani michezo yao yote mitatu
wamekomba pointi tatu walianza kukusanya pointi mbele ya JKT
Tanzania kwa ushindi wa mabao 3-1 kisha wakasepa na pointi tatu mbele ya Mtibwa
Sugar kwa ushindi wa mabao 2-1 na kumalizia kulipa kisasi mbele ya Kagera Sugar
kwa ushindi wa mabao 3-0 uwanja wa Kaitaba.
Mambo haya
yatanogesha mchezo wa leo na kuufanya uwe wa kuvutia kwa timu zote mbili ndani
ya dakika 90:-
Kuvunja mwiko na kuendeleza ubabe
Hapa timu
zote mbili zinahaha kutafuta rekodi mpya kwa kuvunja mwiko na nyingine ikihaha
kuendeleza ubabe. Biashara hesabu zao kubwa ni kuvunja mwiko ambao msimu
uliopita ulivunjwa na Simba kwa kufungwa mabao 2-0 na yote yakifungwa na
nahodha John Bocco jambo lililowaumiza mashabiki na viongozi hvyo leo lao ni
moja tu kulipa kisasi.
Simba wao
wanaingia uwanjani wakiwa na hesabu za kuendeleza ubabe wao ambao waliuanzisha
msimu uliopita kwa kusepa na pointi tatu muhimu ili kulinda rekodi yao ya
kucheza mechi nyingi bila kufungwa.
Heshima
Biashara
United leo inahitaji heshima kwani inatambua kwamba Simba ana hasira za
kutolewa Ligi ya Mabingwa hivyo lazima apambane kurejea kwenye ubora wake msimu
ujao jambo ambalo litaongeza ushindani wa mchezo wa leo.
Pia Simba haitakuwa na presha kubwa kwenye
mchezo wa leo kutokana na matokeo ambayo imeipata mpaka sasa kwenye michezo
yake mitatu kwa kujikusanyia pointi tisa wakiwa ni vinara kwenye ligi.
Tatizo la Biashara limefanyiwa kazi
Tayari
kwenye michezo minne ambayo wamecheza mpaka sasa, safu ya ushambuliaji wa
Biashara United imeonesha kuwa ni nyanya huku washambuliaji wake wengi wakiwa
ni butu jambo ambalo limefanya Kocha Msaidizi, Omari Madenge kulifanyia kazi
kwa ukaribu hivyo leo atatesti mitambo yake upya mbele ya Simba.
Mpaka sasa
safu ya Biashara United imefunga bao moja pekee ndani ya dakika 360 huku Innoncent
Edwin ndiye aliyefunga bao mbele Alliance wakati timu ikilazimisha sare ya
kufungana bao 1-1.
Kagere leo kazi anayo
Mshambuliaji
wa Simba, Meddie Kagere ndiye mchezaji atakayekuwa analindwa leo na Biashara
United kutokana na kasi yake ya kucheka na nyavu kwani ndani ya dakika 270
ambazo ni sawa na mechi tatu ametupia jumla ya mabao matano na akitoa assiti
mbili za mabao.
Karume yaigomea Biashara
Kwenye
michezo miwili ambayo Biashara United wamecheza uwanja wa Karume hawajaambulia
hata bao moja zaidi ya kuruhusu mabao matatu na kupoteza jumla ya pointi sita
kwani walianza kufungwa mbele ya Kagera Sugar mabao 2-0 kabla ya kupoteza mbele
ya JKT Tanzania kwa kufungwa bao 1-0.
Hasira za
kupoteza michezo miwili ya nyumbani ziliufanya uongozi wa Biashara United
kuketi kikao kizito wakiongozwa na Mwenyekiti Seleman Mataso kutafuta dawa mpya
ambayo itaanza kufanya kazi leo mbele ya Simba.
Makocha hawa
hapa
Omary
Madenge , Kocha msaidizi wa Biashara United amesema kuwa wanatambua mchezo
utakuwa mgumu ila watapambana.
“Msimu
uliopita tuliambulia pointi moja kwa Simba, msimu huu tupo vizuri na lengo letu
ni kuona tunapata pointi tatu muhimu.
Patrick
Aussems, Kocha wa Simba amesema kuwa mchezo utakuwa mgumu kutokana na ugumu wa
uwanja pamoja na ushindani ila hesabu zake ni pointi tatu.
0 COMMENTS:
Post a Comment