September 17, 2019


Machungu ya kidonda cha mashabiki wengi wa Simba cha kumpoteza straika wao kipenzi, Emmanuel Okwi raia wa Uganda yanaanza kupoa kutokana na uwepo wa straika Miraji Athuman ‘Shevchenko’ au Sheva.

Awali, kabla ya Miraji, wengi walijua kwamba straika Mcongo Deo Kanda ndiye angechukua mikoba ya Okwi aliyetimkia Al Ittihad ya Misri lakini imekuwa kinyume chake na sasa wanamtazama Miraji kama mtu wao muhimu katika kuwapatia matokeo mazuri.

Miraji ambaye alikuwa kwenye kikosi cha dhahabu cha vijana cha Simba kilichotwaa ubingwa wa ABC Super8 Cup 2012, alionyesha kwamba anafaa kuchukua mikoba hiyo baada ya kuisaidia Simba kupata sare ya bao 1-1 kwenye mechi na UD do Songo ya Ligi ya Mabingwa lakini wakatolewa kwa sheria ya bao la ugenini.

Championi Jumatatu, linakuchambulia matukio ya Miraji ambayo ameyafanya kiasi cha kuwakuna mashabiki wa timu hiyo na kumuona mkombozi wao mpya.

ASABABISHA PENALTI NA DO SONGO

Kwenye mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika Simba walikuwa na wakati mgumu kutokana na hadi dakika ya 86 kutofunga bao lolote kabla ya Miraji kuja kusababisha bao lao.

Miraji ambaye msimu uliopita alikuwa Lipuli FC ya Iringa, aliingia dakika ya 62 kwenye mechi hiyo akichukua nafasi ya Sharaf Shiboub kisha dakika ya 86 akaenda kusababisha penalti pekee ambayo ilizalisha bao la Simba lililofungwa na Erasto Nyoni.

AWAUA JKT TANZANIA

Miraji kuonyesha kwamba yuko moto kwenye mechi yake ya kwanza ya ligi akiwa na Simba aliwachapa JKT Tanzania kwenye mechi iliyoisha kwa mabao 3-0. Mabao mengine yalifungwa na Meddie Kagere.

Kwenye mchezo huo Miraji ambaye anatumia jezi namba 21 akiwa kikosini hapo alitokea benchi kisha baadaye alifunga bao ambalo liliwapa uhakika Simba wa kupata pointi zake tatu kwenye mechi ya kwanza ya ligi.

AWALAZA NA VIATU MTIBWA

Ijumaa iliyopita wakati Mtibwa Sugar wakijua tayari wamewaweza Simba na wataenda nao sare ya bao 1-1, mambo yalibadilika baada ya kulizwa na Miraji ambaye alifunga bao la pili la Simba kwenye mechi hiyo na kuipa timu yake ushindi wa mabao 2-1.

Mshambuliaji huyo alikuja kugonga msumari wa pili na wa mwisho kwa Simba kwenye mechi hiyo na kuifanya klabu yake kukusanya pointi sita ikiwa moja ya timu ambazo ziko juu kwenye msimamo.

MZEE WA MABAO YA MWISHO

Kutokana na mwenendo wake Miraji tayari ameshapachikwa jina la Mzee wa Mabao ya Mwisho, kwani ndiye mchezaji ambaye anafunga au kusababisha mabao ya mwisho kwenye mechi zao kila mara.

Alianza na kusababisha bao dakika ya 86 dhidi ya Do Songo, kisha dhidi ya JKT Tanzania akafunga bao la tatu na hata kwenye mechi na Mtibwa ndiye aliyefunga bao la pili na la mwisho kwa timu yake.

SILAHA YA AUSSEMS

Kocha wa Simba, Patrick Aussems amekuwa akimtumia Miraji kama silaha yake pale anapoona mambo yamekuwa magumu. Alimtumia kama silaha kwenye mechi na Do Songo, JKT na Mtibwa ambapo kwenye mechi zote alifanya kile ambacho kocha huyo alitaka kwa kufunga mabao na kuipa timu yake pointi.

MTOTO WA NYUMBANI

Kitu ambacho unaweza ukawa hujui ni kwamba Miraji ni mtoto wa nyumbani pale Simba. Alianza soka lake Simba ya watoto (Simba B) na alikuwa kwenye kile kizazi cha dhahabu cha Simba kilichochukua ubingwa 2012.

Kikosi hicho kiliwajumuisha Jonas Mkude, Said Ndemla, Miraji Athuman, Haroun Chanongo, Edward Christopher, Omary Salim, Miraj Adam, Abdallah Seseme, Hassan Isihaka na wengineo.

MWENYEWE ANAFUNGUKA

“Mimi kwenye mechi wakati nikiwa benchi huwa na kawaida ya kuwasoma wapinzani juu ya makosa ambayo wanayafanya na ndiyo imekuwa silaha yangu kubwa ninapoingia ninafanya vizuri na kufunga.

“Lakini pia mara nyingi kocha Aussems amekuwa akinipa maelekezo ya kwamba ninatakiwa kuomba mipira na kushambulia kwa kwenda mbele ndiyo maana ninafunga kwenye mechi zetu,” anasema Miraji.

MATOLA AMFUNGUKIA

Kocha wa zamani wa Miraji akiwa Simba B, Selemani Matola ambaye ni mchambuzi wa gazeti hili la Championi, amefunguka juu ya kiwango cha straika huyo kama ifuatavyo: “Ninampongeza sana kwa kiwango anachokionyesha kwani ni tangu alipokuwa timu B. Hashuki kiwango chake kwa muda wote ambao nimemjua lakini ninaona kabisa akiwa msaada mkubwa kwa Simba.

“Wakati akiwa Simba B ndiyo alikuwa staa wangu na anajiamini, atakuwa msaada mkubwa, ninamuona akifanya vizuri hapo na atakuwa bora zaidi ya wachezaji wengi ambao amewakuta hapo.”

8 COMMENTS:

  1. si rahisi kama unavyodhani,kwani okwi ni level nyingine brother huwezi kumlinganisha na madenge hata kwa dakika moja,isipokua tu bwana mdogo anajituma na endapo ataendelea kwa mwendokasi huu atafika mbali,tunamuombea sana ila sio kwakumlinganisha na pro okwi.

    ReplyDelete
  2. Miraji anaweza kuwa zaidi ya Okwii hakuna shaka yeyote na kama angekuwa mchezaji wa kigeni basi hivi sasa Miraji ni staa mkubwa sana Tanzania.

    ReplyDelete
  3. Muhimu kwa mchezaji yeyote ni kuwa na discipline ndani na nje ya uwanja. Hana sababu ya kufananishwa na mchezaji yeyote. Thamani yake ni mchango wake kwa timu kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo. Sasa ndio kwanza mechi ya pili na safari ndio imeanza. Da Silva nae pia anarudi. Wote watathaminiwa kulingana na mchango wao.

    ReplyDelete
  4. Kwenye mpira kila mtu ana style yake...muhim ni nidham, mazoez na kujitambua simama kama miraji athumani na sio mrithi wa mtu...kila mtu anahutaj kuwa part of history

    ReplyDelete
  5. uongo miraj hafanan na okwi hata kdogo.

    ReplyDelete
  6. Okwi alikua zaidi ya mhimili pale simba,tuache unafiki kwa miraji kumlinganisha na okwi hapana bado sana.

    ReplyDelete
  7. Miraji athumani ni mzuri ila deo kanda ni mzuri zaidi,mfumo wa simba unamtumia kama winga ndio maana amekuwa mpiga krosi nyingi kuliko kuingia kwenye penati boksi kitu kama hiki kilimuathiri pia Okwi msimu uliopita kwa kumaliza kipindi kirefu bila kufunga, kocha amuamini tu awe anaingia kati

    ReplyDelete
  8. Miraji ana nafasi ya kuziba pengo la okwi, kuziba pengo si lazima acheze kwa kiwango sawa na okwi bali kufanya majukumu sahihi hasa la kufunga.

    Muandishi yupo sahihi sana kwa dakika za Miraji na matokeo ni taswira nzuri kwa simba

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic