NYOTA YANGA WAMPA PRESHA LWANDAMINA
Kocha Mkuu wa Zesco United, George Lwandamina amesema anashindwa kuielezea Yanga kwa sasa kwa kuwa imefanya usajili wa wachezaji wapya wa kigeni ambao wanaonekana kuwa na uwezo tofauti lakini pia vitu vingi katika klabu hiyo vimebadilika.
Lwandamina ambaye aliwahi kuinoa Yanga kwa misimu miwili, kesho Jumamosi atakutana na timu yake hiyo ya zamani katika mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika kutafuta nafasi ya kutinga hatua ya makundi, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Lwandamina alisema anashindwa kuielezea Yanga ya sasa na mchezo wenyewe kwa jumla kwa kuwa vitu vingi katika klabu hiyo vimebadilika huku akiweka wazi kuwa Yanga imefanya usajili mzuri kwa kipindi hiki hivyo mtu pekee anayemfahamu katika timu hiyo ni kocha msaidizi wa Noel Mwandila ambaye aliwahi kufanya naye kazi.
“Siwezi kuizungumzia Yanga kwa sasa, ni timu mpya, ina viongozi wapya, kocha mpya na mfumo mpya pia, kila kitu ni kipya, imefanya usajili wa wachezaji wengi wa kigeni ambao inaonekana wana uwezo mkubwa, watu wote ni wageni kwangu isipokuwa kijana wangu Noel ambaye nilimuacha miaka miwili iliyopita,” alisema Lwandamina.
Wakati huohuo, Zesco walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana lakini walikataa waandishi wa habari kuingia uwanjani hapo kushuhudia mazoezi hayo huku kukiwa na ulinzi mkali muda wote.
siyo misimu miwili ni msimu mmoja na 1/2
ReplyDelete