October 13, 2019



KILIO kwa timu zetu zote za Bongo kushindwa kutinga hatua inayofuata kwenye michuano ya kimataifa ni jambo ambalo linaumiza kuona namna tunavyopoteza nafasi za wazi kuyafikia malengo ambayo tunayawaza kwa muda mrefu.

Simba ambao walianza kutupwa nje mapema kwenye Ligi ya Mabingwa licha ya msimu uliopita kufanya vema kwenye michuano hiyo na kutinga hatua ya robo finali wameshindwa kuyafikia malengo yao kutokana na kuhamishia mpira mdomoni badala ya kuweka nguvu kwenye uwekezaji.

Tuliona namna walivyokuwa na tambo kuhusu upana wa kikosi chao licha ya kufanya usajili makini ila bado kuna kazi ilitakiwa kufanya kufikia malengo ambayo walijiwekea mwanzo wa msimu.

Kufikia mafanikio mwanzo inaonesha kwamba ilikuwa ni kama bahati kwao licha ya kufanya makubwa ila msimu huu wamechemka mapema kutokana na papara na kujiamini kuliko pitiliza jambo ambalo kwa sasa limeacha maumivu kwenye mioyo ya mashabiki.

Kwa upande wa KMC hawa ilikuwa ni bahati kimjini inaitwa zali hawakujua wanahitaji nini kwenye michuano ya kimataifa kwani hawakufikiria kama ingetokea hivyo kwao siwezi kuwalaumu japo nao wametibua rekodi zao kimataifa.

Kutolewa kwao nyumbani kumewafanya hata Simba nao kuiga kwao licha ya wao kuwa kwenye Kombe la Shirikisho na sasa tumebaki watazamaji kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku wengine wakizidi kuchanja mbuga wanatuacha palepale walipotukuta.

Anguko la Azam FC ni funzo kwetu na kila timu inapaswa itambue kwamba hata kama una kila kitu ukakosa umakini ni rahisi kuanguka kutokana na ukweli kwamba mpira kwa sasa umebadilika na kila timu inatafuta matokeo.

Ni nini ambacho walikosa Azam FC kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho? Je kwa upande wa Simba walikosa nini msimu huu kufikia malengo ambayo walijiwekea? Ukitazazama Azam FC na Simba uwekezaji wao ni mkubwa na fedha zipo.

Kutolewa mapema inamaanisha kwamba kuna kitu ambacho kinakosekana ndani ya timu ni lazima kitafutwe mpema ili kujiaanda kwa ajili ya wakati ujao kutoambulia maumivu kama haya.

Usajili wa Azam FC na Simba unaingia kwenye rekodi ya usajili wa gharama matokeo yake yamejificha wapi kwa sasa? Inaonekana yamejificha kwenye kutolewa kwenye michuano ya kimataifa, ajabu ni kwamba timu zote mbili kubwa zina matatizo ambayo ukiangalia hayaonekani kirahisi hivyo kwa kuwa hawayasemi ni wakati wao kuyatatua.

KMC wao nilishamalizana nao kwamba ugeni umewaponza maana Azam wao wana muda mrefu wanashiriki michuano ya kimataifa tangu mwaka 2013 wamecheza zaidi ya michezo 10 sasa hapo uzoefu gani ambao wanauhitaji kwa sasa zaidi ya kufanyia kazi kile kinachowarudisha nyuma?

Yanga nao ambao kwa sasa wapo hatua ya Kombe la Shirikisho hawajawa na muunganiko makini hasa kwenye safu ya ushambuliaji pamoja na umaliziaji, kwa sasa ni muda sahihi wa kuweka mipango sawa hasa kwa kutazama yale ambayo yaliwaponza kushindwa kutinga hatua ya makundi.

Timu inaonekana inashindwa kuwa na mipango mizuri ya umaliziaji nafasi ambazo wanazitengeneza na kukosa kabisa washambuliaji, huu ni ugonjwa unaozitesa timu nyingi kushindwa kupenya hatua za kimataifa ni wakati wa kujipanga  kufuta makosa yote yaliyopita.

Ni muda makini wa Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera kuangalia namna bora ya kutafuta ushindi na sio kujilinda hasa kwenye mechi atakazoanza nyumbani ni muhimu kufunguka na kutafuta matokeo kwanza kisha timu ijilinde ikiwa imeshapata ushindi.

Itakuwa ngumu kupata matokeo endapo timu itaanza kujilinda ilihali ina nafasi ya kushinda jambo ambalo limekuwa likiigharimu timu kushindwa kufanya vema kwenye michuano ya Kimataifa hasa katika mechi za karibuni.

Mzigo mzito unakuwa kwa mabeki ambao hawana ujuzi wa kushambulia wao wanaongezewa mzigo wa kulinda timu kwani kama timu haishambulii inatoa nafasi kwa mpinzani kulisakama lango namna anavyotaka na inakuwa rahisi kupoteza.

Yote kwa yote wachezaji wetu wanapaswa wajitambue kwamba ni muda wao kuonyesha uwezo wao wote kwenye michuano ya kimataifa na kujiweka sokoni itakuwa ni rahisi kuyafikia mafanikio ambayo 
wanayahitaji.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic