October 13, 2019



ABDULAZIZ Makame, kiungo wa Yanga kwa sasa wengi  bado wanamyooshea vidole wakiamini kwamba ameiua timu yake anayoitumika kwa sasa ndani ya kikosi hicho.

Ikumbukwe kuwa Makame alikuwa ni miongoni mwa kikosi kilichoivusha Yanga hatua ya awali na kutinga hatua ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa hivyo kwa sasa hatuna mashaka na uwezo wake.

Kujifunga kwakwe mbele ya Zesco United kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa dakika za usiku sio kosa kwake ni bahati mbaya.

Haikuwa mipango yake na kama ulitazama vema mchezo ule ambao umeitoa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa na kuangukia Kombe la Shirikisho alikuwa mpambanaji mkubwa.

Ametimiza majukumu yake kwa umakini ila kosa moja ambalo limetokea linafaya wengi wasahau kwamba yeye ni mchezaji na binadamu hivyo kukosea ni sehemu ya maisha.

Bado ana nafasi ya kufanya makubwa ndani ya timu yake ya Yanga ukizingatia ni kijana mpole na msikivu awapo uwanjani lazima upende kumuangalia namna anavyofanya.

Juhudi zake zisipuuzwe ghafla na maneno ya watu ambao hawana nia njema na wachezaji wetu wa ndani ambao ni hazina kwetu.

Wakati uliopo kwa sasa mpira hauna lawama zaidi ya kujifunza kupitia makosa na kutazama namna mpya ya kujenga na sio kubomoa.

Faida ipi ambayo watu wataipata kwa kumyooshea vidole kijana Makame kwamba hakuwa na uwezo wa kucheza ndani ya Yanga?.

Hata Kocha Mkuu wa timu Mwinyi Zahera mwenyewe amekiri kwamba Makame alikuwa amechoka na alikuwa anazidi kupambana licha ya kuchoka kwake.

Tazama vizuri hata baada ya kuona amejifunga nguvu zake zote ziliisha ila alianza kurejea taratibu kwenye uwezo wake licha ya kushindwa kumaliza mpira kwa kiwango ambacho alianza nacho.

Nasema kwamba ni muda wa kutazama mazuri na kusahau mabaya ya Makame, tumpe nafasi kwa ajili ya kuendelea kulitumia Taifa tusianze propaganda za mtaani kummaliza nguvu Makame.

Kila mmoja anatambua kwamba hakuna mchezaji anayependa kujifunga lakini suala la matokeo ya mpira halitabiriki chochote kinaweza kutokea.

Ni muda wa mashabiki kuendela na sapoti kwa wachezaji wetu wote wanaoshiriki michuano ya kimataifa bila kuwabagua.

Makame muda wako wa kusimama ni sasa usikate tamaa, nyanyuka uwezo unao na nguvu unazo ukikata tamaa utajipoteza.

Usikubali kujilaumu ni muda wako wa kujisamehe na kuanza maisha upya, siku zinakwenda na mambo mapya yanakuja.

Achana na hisia kwamba umeshindwa kwenye mechi za kimataifa bado wewe ni wa kimataifa na uzizimishe taa ya mafanikio yako ambayo umeiwasha.

Timu zote ambazo zimeshiriki michuano ya kimataifa zinastahili pongezi licha ya kushindwa kufika mbali hapa nazungumzia Azam FC, KMC, Malindi na Simba ambao hawa safari zao zimekata mapema.

Wakati wao wa kujipanga kimataifa watakapopata nafasi ni muhimu kwa kufanyia kazi makosa yao yote ambayo wameyafanya msimu huu.

Kwa Yanga ya Makame, safari bado inaendelea kwani baada ya kufungashiwa vilago Ligi ya Mabingwa muziki unahamia Kombe la Shirikisho.

Ni muda sahihi kwa timu ya Yanga kutambua kwamba Taifa linawatazama kwa ukaribu na kwa umakini kwani hakuna muda wa kutafuta sababu tena.

Matokeo ya uwanjani yanabebwa na kujiandaa vema kwenye michuano ya kimataifa hivyo kikubwa ni kwamba hakuna mwenye uhakika na matokeo.


2 COMMENTS:

  1. Makame anatakiwa kurudi nyumbani Simba alipokulia kabla hajashushiwa balaa la kuambiwa kuwa anasaliti. Akitaka kuishi kwa amani na ndoto ya kufika mbali zaidi basi afikirie kurudi Simba mapema kabisa.

    ReplyDelete
  2. Ndio tatizo la kuchukua wachezaji wanaofahamika kuwa mizizi yao ipo Simba. Yanga walijifanya wajanja kumuwahi huyo mchezaji wakati Simba walikuwa na mpango wa kumrejesha mtoto nyumbani. Na bado!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic