NA SALEH ALLY
KUTOLEWA kwa Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika, hakuwezi kuwa gumzo kubwa kuliko Yanga itafanya nini katika mechi zake zijazo za kimataifa.
Yanga itacheza Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni timu pekee ya Tanzania ambayo imebaki inashiriki michuano ya kimataifa kwa msimu wa 2019/20.
Timu nyingine zote tatu ambazo zilikuwa zinakamilisha idadi ya nne kwa mara ya kwanza Tanzania kuwa na timu mbili Ligi ya Mabingwa na mbili Kombe la Shirikisho, zimetolewa michuano ya kimataifa.
Kama unakumbuka tulianza na timu nne ikiwa ni nafasi mbili za nyongeza, moja upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine Kombe la Shirikisho Afrika. Hii ilikuwa ni baada ya Simba kufanya vizuri na kufika robo fainali katika msimu wa 2018/19.
Bahati mbaya kabisa, hatua ya awali, timu mbili yaani Simba wenyewe upande wa Ligi ya Mabingwa na KMC kwenye Kombe la Shirikisho, wakang’oka.
Tukabakiza timu mbili ambazo ni Yanga na Azam FC ambao walikwenda hatua ya kwanza. Azam nao wametolewa na Triangle ya Zimbabwe baada ya kufungwa jumla ya mabao 2-0, wakipoteza 1-0 katika kila mchezo.
Yanga nao wameng’oka katika Ligi ya Mabingwa lakini wanaendelea kubaki kwa kuwa wamekosa nafasi kucheza hatua ya makundi, wanakwenda Kombe la Shirilkisho.
Nimeangalia mechi ambayo Yanga wametolewa na Zesco ya Zambia ambayo inafundishwa na George Lwandamina, mmoja wa makocha bora Afrika aliyewahi kuinoa Yanga na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Mechi ya kwanza iliisha kwa sare ya bao 1-1 jijini Dar es Salaam na kule Ndola nchini Zambia, Yanga ikiwa ugenini ikafungwa kwa mabao 2-1 zikiwa zimebaki dakika chache mechi kwisha.
Bao la Zesco limepatika kwa kiungo kinda wa Yanga, Abdulaziz Makame kujifunga wakati akijaribu kuokoa krosi baada ya beki Ally Ally kuwa ametokwa.
Wakati mechi inaanza, utafikiri Zesco wangeifunga Yanga mabao matatu, manne au hata matano. Hata walipopata bao katika dakika ya 25 kupitia kwa Jesse Were, ilionekana sasa Yanga inadidimia.
Mapambano ya kiwango cha juu kabisa cha wachezaji wa Yanga, yaliifanya Zesco kukosa mbinu. Maana walisawazisha na kuendelea kushambulia.
Pamoja na kwamba Zesco walishambulia sana lakini Yanga walionekana kuwazidi mbinu. Hakuna ubishi wengi walitarajia Yanga kufungwa mabao mengi lakini tumeona, ilikuwa ni vita hasa ya wanaume.
Hapo ndio najiuliza, kwamba Yanga wana sababu ipi hasa ya kujilaumu au kuanza kuchanganyikiwa? Maana pamoja na kutolewa, bado hawajapoteza sifa ya kuwa wawakilishi wa Tanzania katika michuano iliyo chini ya Shirikisho la Soka la Afrika (Caf), tena safari hii wakiwa wawakilishi pekee.
Kweli Ligi ya Mabingwa ni kubwa sana, soka ndivyo lilivyo, ukikosea unaadhibiwa na Yanga tumeona suala la kuwa na wachezaji kadhaa wasio na uzoefu wa mechi za kimataifa kwa kiwango cha Ligi ya Mabingwa Afrika, kimewaathiri.
Sasa wanakwenda Kombe la Shirikisho na tunajua, kuna timu zilizoshika nafasi za pili katika nchi zao, zile ambazo zilibaki kidogo kuwa mabingwa na zile zilizotolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyo kwa Yanga, ndio inakwenda kukutana nazo.
Sasa Yanga iendelee kuwaza kilichotokea na kukifanya ndio mjadala mkuu, au kuachana nacho na kuangalia nini kitafuata na nini cha kufanya katika mechi zake zijazo za michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa Caf kwa upande wa klabu?
Jibu liko wazi, Yanga hawapaswi kulaumiana au kulalamika kwa muda mrefu na muhimu sasa ni suala la kuangalia nini kitafuatia katika mechi zao zijazo za Ligi Kuu Bara na pia michuano hiyo ya kimataifa.
Kila makosa, yanatengeneza funzo na yanakuwa faida kwa mwendo unaofuata. Kama ulikosea halafu ukabaki unalia na kulalama muda wote, unatengeneza wigo mwingine wa kukosea zaidi.
Huu ni wakati wa Yanga kufikiri chanya na kuachana na mijadala itakayowachanganya zaidi kwa kuwa mafanikio ya Kombe la Shirikisho bado yana faida kwao na Tanzania kwa ujumla.
Simba ni kiongozi kwa mashindano ya kimataifa Tanzania na Yanga wapende wasipende ama watake wasitake huo ndio ukweli. Yanga waliibeza Simba kwa kufika hatua ya robo fainali msimu uliopita kwa kusema kuwa mfumo wa mashindano ya klabu bingwa Africa umebadilishwa na kuwa rahisi zaidi kwa timu kuingia hatua za makundi? Lakini mara pa Mungu akata mzizi wa fitina kwa Yanga kupata shavu la kuiwakilisha nchi kwenye mashindano hayo hayo ya klabu bingwa Africa sambamba na Simba. Kama vile haitoshi Mungu akatenda maajabu zaidi yasitegemewa pale simba ilipotupwa nje ya mashindano na kuiacha Yanga kuwa mwakilishi pekee wa kugombania taji la mabingwa la Africa kwa klabu za Tanzania kana kwamba Yanga walitenda walichotenda ili Simba aondoshwe kifadhaha fadhaha hivi ili wao wafike mbali zaidi ya pale alipoishia Simba na kukata ngebe za wanamsimbazi.Ila kilichotokea kwenye ushiriki wa Yanga klabu bingwa Africa ni kwamba bado wanamengi sana ya kujifunza kutoka kwa Simba ili watoboe zaidi. Wana Yanga wanahasira na Simba hakuna ubishi kwani ubingwa wa ligi wanausikia redioni tu. Na tayari Yanga wamepokonywa wachezaji kadhaa na Simba waliokuwamewasajili na waliokuwa wanataka kuwasajili kiasi kwamba Yanga mara kadhaa huishia kusajili wachezaji ambao Simba huwa hana haja nao. Haya ni mateso kwa wana Yanga ni si ajabu hata kidogo kwa wafuasi hao wa Yanga kukimbilia nguvu za giza ili kuipiga Simba kwenye mambo yake ili isifanikiwe lakini licha ya hasira zote hizo za Wanayanga utakuwa ujinga kwao kuacha kuiga yale mazuri ya Simba kwa faida ya klabu yao. Kwa mfano Yanga wamepoteza nafasi ya kusonga mbele zaidi klabu bingwa Africa kwa sababu ya kushindwa kufuata kauli mbiu ya Simba inayosema "kwa mechi za nyumbani kufa au kupona lakini mgeni lazima apigwe kwa mkapa". Yanga bila ya kuutumia uwanja wa nyumbani kwa faida yao basi hawawezi kufika popote pale kimataifa .
ReplyDeleteTatizo la kuhara huku unacheka ndio hilo lililokusibu we mtu,angalia usije wachafua wenzio hapo ulipo!
DeleteUkweli unauma bana we mtoa maoni wa kwanza unakera ila huo ndio ukweli .
ReplyDelete