October 3, 2019



MASHABIKI kwa sasa wanaitazama safari ya timu ya Taifa ya Tanzania kwenye michuano ya Chan inayotarajiwa kufanyika nchini Cameroon mwaka 2020 ikiwa imeanza kukumbwa na misukosuko mapema.

Ikumbukwe kuwa mchezo wetu uliochezwa uwanja wa Taifa dhidi ya Sudan haukuwa na matokeo chanya kwa upande wetu kutokana na kupoteza kwa kufungwa bao 1-0.

Ni matokeo yasiyopendeza kwa mashabiki pamoja na Taifa kwani tulikuwa nyumbani na nafasi tulikuwa nayo ya kushinda mwisho wa siku ni matokeo ambayo yamepatikana.

Kwa sasa ambacho kinatakiwa kufanyika ni utulivu kwa mashabiki na kuendelea kuipa sapoti timu ya Taifa kwani bado dakika 90 za mwisho kumpata mshindi.

Kwa namna mpira wa sasa ulivyo kila timu ina nafasi ya kushinda popote pale iwe ugenini ama nyumbani hivyo safari ya kutafuta ushindi inaendelea na inawezekana.

Mashabiki wengi wamekuwa wakiipa sapoti timu yao ya Taifa hili ni jambo la kupongeza na linapaswa liendelee muda wote kwa ajili ya kuleta ile hamasa.

Mpira ni mchezo wa  wazi kwa sasa na kila timu ambayo itajipanga sawasawa ina nafasi ya kushinda kwenye mchezo wake iwe nyumbani ama ugenini.

Lengo letu la kwanza ambalo ni kubwa kwenye mashindano haya ni  kufika mbali na ili kufika mbali ni lazima kupambana na kupata matokeo chanya.

Furaha ya mashabiki ni kuona timu inapata matokeo chanya kwenye michezo yote hilo ndilo ambalo wachezaji na benchi la ufundi linahitaji pia ila tatizo ni kwamba timu zote zinatafuta matokeo na ushindani ni mkubwa.

Kwa kuwa wapinzani wetu Sudan wametufunga kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa hapa nyumbani ni wakati wetu kuungana kwa ajili ya kwenda kuwamaliza kwao ili kupata ushindi na kusonga mbele.

Pia tukitaka kuwa na nguvu ya kuendelea kusonga mbele kuna umuhimu wa sapoti ya mashabiki ambayo imeanza tangu awali kuendelea na kuwapa moyo wachezaji wetu pale ambapo watakuwa wanapambana.

Ni muda wetu kuungana na kujenga kwa pamoja na sio kuanza kutengana kwa kuwa timu yetu imepoteza mchezo licha ya maumivu kuwa yetu sote ila ni matokeo ya mpira.

Wakati mwingine yanakuwa ni ya kikatili sana naya kuumiza hasa ukizingatia kwamba mashabiki na wadau wengi walijitokeza kuipa sapoti timu yao ya Taifa uwanja wa Taifa.

Kazi ni kubwa kwa sasa kuona namna gani timu itapata matokeo kwenye mchezo wa marudio na sio kuegemea kuwalaumu wachezaji hakuna ambaye alikuwa anapenda kupoteza mchezo wake.

Jukumu la pili ambalo lipo mkononi mwa wachezaji ni kwenda kutafuta matokeo kwenye mchezo wa pili wa marudiano.

 Tuliangukia pua mchezo wetu mbele ya Sudan ipo wazi mashabiki wasichukue matokeo hayo kuihukumu timu yao bado wanapaswa waendelee kuwa wazalendo na kuiunga mkono timu yao ya Taifa.

wachezaji wanapaswa waendelee kufanya kitu cha kipekee kwa kujituma uwanjani kutafuta matokeo chanya na kurejesha furaha ya watanzania.

Nidhamu yao itakuwa na manufaa endapo watakuwa na juhudi kutafuta matokeo kwenye mchezo wa marudio na ili kurejesha furaha kwa mashabiki na Taifa kiujumla.

Kwa matokeo ya awali kila mmoja ameumia na haikuwa malengo kufanya hivyo kwani wachezaji walicheza mpira na mwisho wa siku kushindwa kumalizia nafasi kumeiponza timu na Taifa kiujumla.

Kwa sasa ni muda wa kuungana na kuendelea kushikamana kwa ajili ya kuongeza nguvu kuelekea mchezo wa marudio ambao utaamua nani ni mshindi.

Kazi haitakuwa nyepesi kutokana na wapinzani kuwa na faida ya bao la ugenini ila haileti shida kwa kuwa mpira ni ndani ya dakika tisini na kila timu inaingia uwanjani kutafuta matokeo.

Mashabiki waendelee kutoa sapoti kwa timu yao bila kuchoka na inawezekana kuwa na nguvu mpya kwenye mchezo wa marudio.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic