October 3, 2019


MAUMIVU ni ya Taifa zima kiujumla hasa kwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kuanza kwa kuangukia pua mchezo wake wa kuwania kufuzu hatua ya Chan dhidi ya Sudan kwa kufungwa bao 1-0.

Haikuwa matarajio ya wengi kuona timu yetu ambayo tunaipenda ikipoteza mbele ya umati wa mashabiki wake waliojitokeza kuipa sapoti kwa hali na mali uwanja wa Taifa.

Wengi tulitarajia timu yetu ingetutoa kimasomaso kimataifa kwa kumaliza kazi mapema badala yake imejiongezea mzigo wa kwenda kufanya kimataifa.

Kwa sasa naona wengi wameanza kukata tamaa hilo sio sawa kuikatia tamaa timu ya Taifa kwani mchezo wa kwanza dakika 90 zimekamilika kilichobaki ni kwenda kukamilisha dakika 90 zinazofuata.

Nafasi yetu ilikuwa kubwa na wengi walikuwa wanaamini kwamba kazi ya kwanza inamalizwa hapa na kwenye mchezo wa pili ilikuwa ni kukamilisha ratiba kibabe mambo yemegeuka chini juu juu chini.

 Tulikuwa tunatafuta matokeo kama ambavyo wapinzani wetu Sudan walikuwa wanafanya na mwisho wa siku mshindi akapatikana kwenye mchezo wa kwanza ambaye ni Sudan.

Bado tunapambana na moto wa kutafuta matokeo unaendelea wote tunapaswa kuendelea kuipa sapoti timu yetu kushindwa kupata matokeo haina maana kuwa kazi imekwisha.

Watu washikamane na kuendelea kuwa kitu kimoja ukizingatia kwamba Taifa ni letu sote na wachezaji pia ni wakwetu hatuwezi kuwakataa kwa sasa kisa kukosa matokeo uwanjani.

Matokeo popote yanatafutwa iwe ugenini ama nyumbani hivyo kwenye mchezo wa pili wa marudio unaotarajiwa kufanyika Octoba 10 tunapaswa tukazane kutafuta matokeo.

Hatutakiwi kukata tamaa kwa kushindwa kupata kile tulichokuwa tunakitafuta bali tunapaswa tuongeze juhudi kutafuta kile ambacho tunakihitaji kwa sasa ambacho ni matokeo.

Nafasi ipo ya kupata matokeo kama ambavyo wao waliweza kupata kile ambacho walikuwa wanakitaka awali kwenye mchezo uliochezwa uwanja wa Taifa.

Benchi la ufundi kwa sasa pia lina kazi ngumu ya kufanya kwa ajili ya kuona timu inapata matokeo na kupenya hatua inayofuata kutokana na ushindani kuwa mkubwa.

Kushindwa kwa mbinu ya kwanza kunapaswa kuwe ni chachu ya hasira ya kutafuta mafanikio kwenye mchezo wa marudio hasa kwa kufanyia kazi mapungufu ambayo yamejitokeza.

Kiufundi hakuna matatizo mengi ambayo yamekuwa yakifanyika kwenye timu yetu hasa wachezaji ambao wameitwa kuonyesha bidii kwenye kutafuta matokeo wanashindwa na spidi ya mchezo hasa kwenye umaliziaji.

Wengi wamekuwa wakifanya mambo mazuri uwanjani ila umaliziaji unakuwa tatizo kubwa kwa wachezaji wetu wa timu ya Taifa ambapo kila mmoja amekuwa akishindwa kutulia anapokuwa eneo la hatari.

Wachezaji wote ambao wanaichezea timu ya Taifa wamekuwa na tatizo la kushindwa kutulia wanapofika ndani ya eneo la hatari kwa kushindwa kuamua nini wafanye kupata bao.

Wamekuwa na ugonjwa wa papara kila wanapoingia eneo la goli jambo ambalo linapaswa litafutiwe dawa mapema kabla ya mechi ya marudio ili kuona timu inapata ushindi.

Umaliziaji ni tatizo ambalo linaigharimu timu yetu ya Taifa kutokana na kushindwa kuwa na mipango makini na endelevu kwa wachezaji wa ndani ambao wanacheza kutafuta matokeo.

Wachezaji wana jukumu kubwa la kupunguza papara wakiwa ndani ya eneo la 18 kwa kutengeneza muunganiko mzuri ambao utatoa matokeo chanya kwa Taifa.

Umakini ukikosekana ni ngumu kwa timu kupata matokeo hata ikiwa inashambulia mwanzo mwisho jambo ambalo kwa sasa limejenga usugu kwenye timu ya Taifa.

Wachezaji wanapaswa wawe na akili ya ziada ndani ya uwanja kwa kujua namna ya kujipanga kwani pia kuna tatizo la kujisahau hasa kwa kushindwa kujua kwamba mpira unaelekea wapi nao waelekee wapi.

Namna teknolojia ilivyokuwa kubwa kwa sasa na mpira nao unazidi kukua hivyo kama njia na hesabu zitakosewa inakuwa rahisi kupotea kwenye ramani mapema.

Tumeona namna ambavyo krosi zinapigwa kwa wachezaji wetu bado hazjiwa na faida kwa timu yetu nalo linapaswa litazamwe na lifanyiwe kazi kwa wachezaji kutambua kwamba hakuna miujiza kwenye kutafuta matokeo.

Tunaamini kwamba kama nafasi ya kuumaliza mchezo ulikuwa mikononi mwetu basi nafasi hiyo tunayo kutokana na aina ya wachezaji ambao tupo nao kwa sasa ni jambo la kusubiri.

Tunapaswa tutambue kwamba mchezo wa marudio hautakuwa mwepesi kutokana na ukweli kwamba wenzetu hawa wana bao la ugenini jambo linaloongeza ugumu.

Hilo litupe hasira ya kuongeza juhudi kutafuta matokeo mapema tukiwa ugenini kwa wachezaji kujitambua na kutafuta matokeo mwanzo mwisho mpaka kielelewekke.

Wachezaji wetu ni wazuri pia wapo  ambao wakipewa mafunzo watafanya vizuri hapo baadaye tuna kazi ya kuandaa kizazi ambacho kitakuja kuwa na mwendelezo mzuri baadaye.

Benchi la ufundi kiujumla nina imani matatizo wameyaona na watayachukua kwa kuyafanyia kazi kwa ukaribu ili kupaa matokeo mazuri mchezo wa marudio.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic