November 17, 2019









Na Saleh Ally aliyekuwa Johannesburg

JANA Ijumaa, katika mahojiano yaliyofanyika nyumbani kwake nchini Afrika Kusini, Abdi Banda alieleza namna ambavyo amekuwa na wakati mgumu kuhusiana na mfumo wa kikosi chake kipya.


Highlands Park ni timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini maarufu kama PSL. Ni moja ya ligi bora barani Afrika, lakini Banda ambaye amejiunga nayo akitokea Baroka FC anaona kuna ugumu kwake licha ya kwamba sasa yuko fiti.


Alikuwa akifikiria kuendelea kupambana hadi atakapopata namba lakini kama itashindikana atachukua uamuzi wa kuondoka na kujiunga na timu nyingine hata kama itakuwa ni daraja la kwanza.


Endelea naye...
“KIASI fulani bado nina matumaini kwamba inawezekana siku moja mambo yatabadilika na mfumo ukabadilika. Lakini kama itashindikana kabisa, basi mara moja nitawaomba wanipeleke kwa mkopo ili nikacheze pia nicheze katika mfumo ambao nauona ni wa soka hasa.


“Unajua hapa bado sijapata nafasi lakini nikipata bado naona kama kuna ugumu pia kutokana na mfumo wenyewe,” anasema Banda na kuongeza:


“Kama ikifikia sasa naondoka, ningependa niondoke kwa ruhusa yao kwa kuwa wao wakiniruhusu bado nitakuwa mchezaji wao na inawezekana wakaona kiwango changu kwa upana zaidi nikiwa nje au naweza kupata nafasi ya kujitangaza zaidi kwa klabu nyingine kwa kuwa ninajiamini ninapopata nafasi ya kucheza, basi lazima nitafanya kazi yangu kwa ubora wa juu kabisa.


“Kuna timu kadhaa tayari zilinitaka kwa kuwa wananijua na wanajua kiwango changu tokea nikiwa Baroka FC. Walinitaka niende lakini nikaona ninaweza kusubiri kwa kuwa ninaheshimu na kukumbuka kuwa Highlands wamenitibu, wameonyesha uvumilivu kwangu.


“Kawaida mimi katika suala la uvumilivu niko vizuri sana. Nakumbuka Simba ile ya kipindi kile cha kina Amissi Tambwe, sikucheza karibia msimu mzima. Maana raundi ya kwanza yote nilikuwa benchi. Lakini nilipambana hadi nikafanikiwa kuingia katika kikosi cha kwanza licha ya kwamba nilibadilishwa namba kutokea pembeni na kuingia kati,” anasisitiza Banda.


Mitandao ya kijamii:
Banda kama staa lazima anahusika na mitandao ya kijamii. Je, anaishi nayo vipi?


“Kwangu wanaoweka ‘comment’ mbaya, ni msaada kwangu, wananisaidia kujituma zaidi. Hali kadhalika na wale wanaonionyesha wananikubali pia naona nisiwaangushe, napambana zaidi.


“Mfano nilikaa nje muda, hakuna aliyejua na badala yake utaona watu wanakusema mtandaoni kuwa mpira umekushinda, umekwenda kufanya starehe, wakati mwingine unaangalia hivi halafu unasema hauwezi kumjibu.


“Unajua ninacheza mpira kwa maisha yangu, hakuna mtu ataanza kukuchanganya kwa ajili ya maneno yake tu. Ni kweli, wakati mwingine hasa kipindi cha nyuma, mtu anaweza kuandika hadi kukutukania wazazi. Mimi naita huwa nafanya usafi, nampiga block.


“Unajua anayefikia mbali anatukana hadi wazazi na familia sababu ya mpira, siyo sawa. Basi ndiyo nafanya hivyo usafi, wanaweza kufika hata watu mia hivi. Ingawa kuna wakati naweza kuwaachia na kuangalia kama wamejirekebisha,” anaelezea Banda.


FAMILIA:
Sasa yuko Afrika Kusini lakini amekuwa akifanya shughuli za kujipikia mwenyewe, wakati ni mtu aliyeoa.


“Kwa hilo namshukuru mama yangu kwa kuwa wakati tukiwa wadogo licha ya kuwa ni watoto wa kiume alikuwa akitufundisha kupika.


“Kama ambavyo umeona, kwa sasa nyumba ipo tupu kwa kuwa mke wangu yuko nyumbani Tanzania, ameamua kunipa nafasi niendelee na suala la kusaka timu. Mwakani Mungu akipenda atarejea nyumbani.


KUPATA MTOTO:
Kumekuwa na taarifa kwamba Banda na mkewe Zabibu Kiba wamejaaliwa kupata mtoto.


“Kupata mtoto ni jambo jema, lakini uhalisia hilo suala si kweli kwa sasa, nafikiri ni watu waliandika tu mtandaoni,” anasema.


“Ushauri wangu kwa watu wa mitandaoni kuwa makini, kuachana na maneno ambayo si sahihi kwa faida ya jamii. Kuna mtu akipata skendo, basi ujue anafurahia sana. Lakini wengine hatupendi hiyo tabia na kama kuna kitu nataka Watanzania, basi nitawapa taarifa kwenye ukurasa wangu au sehemu sahihi za kutoa habari.”


MUZIKI:
Hakuna mchezaji asiyependa muziki hata kama atakuwa anapenda mpira kiasi gani. Kwake Banda ambaye shemeji yake Alikiba ni mwanamuziki maarufu, anasikiliza zaidi aina ipi ya muziki. Je, anasikiliza muziki wa Wasafi inayoongozwa na Diamond?


“Ninasikiliza aina zote za muziki, mfano Wasafi, King Music, kina Mario na wengine nasikiliza. Huwa siangalii huyu ni msanii gani, naangalia kitu kizuri kilichoimbwa. Nasikiliza hadi za wale underground, kama wimbo unanivutia, basi nasikiliza.


“Siwezi kusema kila kinachoimbwa, mfano kitu alichoimba Diamond kinaweza kikawa hakigusi au sijakipenda, naweza kuona si mzuri. Lakini wako wanaovutiwa nacho kutokana na kuguswa au kukifurahia.


“Wakati mwingine naweza kuwa naguswa kupitia jamii. Kiukweli pia navutiwa sana na King Music.


“Kinachonivutia kwa Diamond, zaidi ni jinsi anavyojiamini na kupambana na maisha. Lakini pia nimevutiwa zaidi na Konde Boy (Harmonize), kweli ameonyesha ni mtu wa kujaribu, si mwoga na uamuzi wake wa kuamua kupambana mwenyewe umenivutia hata kuweka nyimbo zake zaidi katika simu yangu. Hii tabia ya uthubutu ninayo mimi na mtu anayejaribu hivyo, ananivutia zaidi.”


TAIFA STARS:
“Ni timu ninayoitakia kila la kheri, nimekuwa nje kutokana na matatizo kadhaa lakini ninaamini siku moja nitarudi na nitacheza kwa mafanikio.


“Nataka kulipigania taifa langu na ninajua umuhimu wa kuitumikia timu ya taifa. Hivyo kuna siku nitarejea na ninajiamini katika hili. Kwa sasa ni suala la subira tu, kwa kuwa sipo, ninawatakia kila la kheri wenzangu ambao sasa wamepata nafasi.”



MWISHO. 

2 COMMENTS:

  1. Hakuna kitu hapo ubishoo tu kazi kumfanyia mahojiano tu kila wakati hana lolote huyo aende biashara akacheze

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic