November 12, 2019



Mkwasa amerejea Jangwani kama kocha ikiwa imepita miaka 18 tangu akinoe kikosi hicho mara
ya mwisho mwaka 2001, na pia anakuwa kocha wa kwanza mzawa tangu miaka 14 iliyopita wakati
Kennedy Mwaisabula alipoinoa timu hiyo.

Tangu Mwaisabula alipoondoka, Jangwani wamekuwa wakifundishwa na makocha wa kigeni
kutoka nchi za Ulaya na Afrika, kabla ya Zahera kutimuliwa siku chache baada ya Yanga
kufurushwa kwenye michuano ya kimataifa walikong’olewa na Pyramids katika Kombe la
Shirikisho barani Afrika.

Wamisri hao waliitoa Yanga kwa ujumla ya mabao 5-1 baada ya awali kushinda jijini Mwanza 2-1
kisha kuifumua tena 3-0 mjini Cairo, na ndipo mabosi wakamchomoa Zahera na kumvuta
Mkwasa asaidiane na Said Maulid ‘SMG’ wakati wakisaka kocha mkuu mpya.

Hata hivyo, kuna majina kadhaa ya makocha wanaweza kuchukua nafasi ya Zahera akiwamo
Hans Pluijm, Ernie Brandts na Kim Poulsen, lakini Mwanaspoti limewaangalia baadhi ya
makocha wa ndani na nje ya nchi na kuona mmojawapo akipewa mzigo itakuwa freshi tu.

Ikumbukwe awali tetesi zilimtaja nyota wa zamani wa kimataifa wa timu hiyo na kocha wa sasa
wa Bandari Kenya, Ben Mwalala, lakini Mkenya huyo amekanusha na kudai kuwa ana mkataba na
klabu ya Bandari, na anajisikia fahari kuendelea kuifundisha.

Kwa hali iliyopo Yanga ni kwamba, makocha wanaohitajika ni wale ambao wanaifahamu vyema
klabu hiyo na soka la Tanzania kwa ujumla, lakini hata uzoefu wa soka la Afrika sambamba na
kuhimili presha ya timu zenye mashabiki wenye mihemko kama Yanga.

Hapa chini ni orodha ya makocha sita ambao kila mmoja anaweza kuwa mtu sahihi kurithi moja kwa moja mikoba iliyoachwa na Zahera sambamba na kauli za wadau wanavyowaangalia na kuiangalia Yanga ya sasa.

Raoul Shungu

Kwa sasa ni kocha msaidizi wa AS Vita ya DR Congo, akiwa na leseni daraja ‘A’ ya Shirikisho la
Soka Afrika (CAF) inayompa uhalali wa kuwa kocha mkuu wa klabu yoyote Afrika.

Shungu aliwahi kuinoa Yanga kati ya 1998-2001 na kutwaa nao ubingwa wa Ligi Kuu mara moja,
1998, kabla ya kutimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Mkwasa. Ndiye aliyeiongoza Yanga
kwenye mechi tano za makundi ya Ligi ya Mabingwa 1998 akimpokea Tito Mwaluvanda aliyekuwa
amempokea Mwingereza Steve McLennan aliyeiwezesha kutinga makundi akisaidiana na
Mwaluvanda ambaye kwa sasa ni marehemu. Shungu anayetokea DR Congo ni kocha anayepewa
nafasi kubwa kuliongoza benchi la ufundi la Yanga na inadaiwa kuwa viongozi wa timu hiyo wamekuwa wakiwasiliana naye mara kwa mara.Changamoto kubwa ambayo inaweza kuikabili
Yanga kwa Shungu ni fedha kwani huenda akahitaji dau kubwa ili aweze kung’oka AS Vita.

Hans Pluijm

Ni kocha aliyepata mafanikio makubwa kipindi akiinoa Yanga kabla hajaachana nayo na
kutimkia Singida United, kiska Azam FC. Aliipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili, taji la
Kombe la FA na kuiongoza kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Kwa sasa
hana timu na hiyo inaweza kuwapa urahisi Yanga kumrudisha kundini ikizingatia pia ni
mwanachama wa klabu hiyo na anaifahamu vyema. Pluijm ana uzoefu wa kutosha wa soka la
Afrika akiwa amefundisha na kuishi kwa takriban miaka 20 katika nchi za Ghana, Ethiopia na
Tanzania, lakini umri mkubwa alionao na kuzoweleka kwa mbinu zake za ufundishaji akiwa na
timu tatu tofauti nchini kunampa wakati mgumu kurejeshwa Jangwani.

Boniface Mkwasa

Kwa sasa ndiye anayekaimu ukocha mkuu wa Yanga, lakini halitakuwa jambo la kushangaza ikiwa
baadaye uongozi wa timu hiyo utaamua kubaki naye moja kwa moja kwa kumpa mkataba wa
kudumu. Mkwasa ana leseni ya juu ya ukocha kutoka CAF na pia ni mkufunzi wa ndani wa
makocha, hivyo anaweza kuwa msaada kwa wasaidizi wake kukua na kupandisha viwango vyao
akiwa pia amewahi kuinoa mara kadhaa Taifa Stars. Faida ya Yanga ikimpa Mkwasa mkataba wa
kudumu ni kwamba, hawatatumia kiasi kikubwa cha fedha kugharamia malipo yake, na pia ni
mtu anayeijua Yanga nje ndani kwani mbali na kuichezea na kuinoa, pia hivi karibuni alikuwa
katibu mkuu wa klabu hiyo kabla ya kujiuzulu.

Beston Chambeshi

Nkana FC ilitinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita huku
ikionyesha kiwango bora katika michezo ya nyumbani na ugenini. Nyuma ya mafanikio hayo kuna
mtu anaitwa Beston Chambeshi, ambaye ni kocha mkuu wa timu hiyo aliyefanya kazi kubwa ya
kujenga muunganiko mzuri na kuimarisha kiwango cha mchezaji mmojamoja. Inawezekana
hayupo katika hesabu za Yanga, lakini ni kocha anayeweza kuwa chaguo sahihi kwao ikiwa
atapewa fursa ya kuinoa timu hiyo. Mbali na kuinoa Nkana FC pia ni kocha mkuu wa timu yake ya
Taifa ya Zambia akiwa na leseni ya juu ya ukocha inayotambulika na CAF.

Kim Poulsen

Jina lake linafahamika na mashabiki wengi wa soka nchini kutokana na kukoshwa na soka
alilofundisha pindi akifanya kazi Tanzania. Poulsen ana uzoefu wa soka la Tanzania na Afrika kwa
ujumla, kwani amefundisha hapa nchini kwa takribani miaka mitano.

Hata asilimia kubwa ya
nyota wa Stars wa sasa ni zao la mikono yake enzi akinoa timu za taifa za vijana, kabla ya kuwa
kocha mkuu wa Stars na baadaye kurejeshwa kama mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF). Kwa sasa ni mkufunzi wa FIFA, jambo ambalo linaweza kuwa gumu kwa Yanga
kumnasa muumini huyo wa soka la kuvutia na anayependa zaidi kuwatumia vijana, jambo
lingeweza kuipa faida Yanga kwani kikosi chake cha vijana kinaweza kuimarika.

Ernie Brandts

Huyu ni mmoja wa makocha waliowahi kuinoa Yanga, alipita msimu wa 2012-2013 na kuifanya
kucheza soka la kuvutia zikiwemo pasi fupifupi jambo ambalo hapo nyuma halikuwepo. Soka hilo
liliwavutia mashabiki wengi ambao walikuwa wakiridhika hata pale timu yao ilipopata matokeo
mabaya. Hata hivyo, kocha huyo Mholanzi hakudumu sana Jangwani kwani alitupiwa virago
baada ya Yanga kupokea kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Simba katika mchezo wa Nani Mtani
Jembe uliofanyika Desemba 23, 2013. Baada ya kuondoka Brandts alizinoa timu za Uholanzi
ikiwemo FC Dordrecht, RKW DIA, NEC na sasa FC Eindhoven inayoshiriki Ligi Kuu, na inaelezwa
mshahara mnono anaolipwa huko unaweza kuwa kikwazo kukubali kuja Tanzania.

WASIKIE WADAU

Wadau wa soka ambao pia ni wachambuzi wa mchezo huo, Kennedy ‘Mzazi’ Mwaisabula na
Mwalimu Alex Kashasha wanaeleza kocha yupi anastahili kuinoa Yanga kwa sasa.
Mwaisabula anasema anaamini mtu wa kuendelea na Yanga ni Mkwasa, baada ya kuanza
kurejesha morali ya wachezaji katika mchezo wake wa kwanza.

“Mkwasa anaujua vizuri mpira wa Bongo vizuri kuliko hao ambao wanataka kuja, kwa hiyo naona
ni bora aongezewe mkataba na kupewa timu moja kwa moja,” anasema Mwaisabula.
“Mkwasa ameweza kuwarejesha wachezaji katika namba zao kama ilivyokuwa kwa (Ally) Sonso na
Mapinduzi (Balama) na wamecheza vizuri.”

Kwa upande wake, Kashasha anasema makocha wote wanaotajwa wanafaa, lakini uongozi
unatakiwa usiangalie rekodi na wasifu pekee, huku akimtaja Kim na Brandts sambamba na
Mkwasa kuwa ni watu sahihi kwa mustakabali wa Yanga.

“Tusiangalie sana CV wala rekodi, bali waangalie aina ya soka ambalo mwalimu husika
anafundisha, kwani inabidi wajue anakuja kukutana na wachezaji wa aina gani, lakini pia soka
letu lina matatizo mengi,” anasema.

Kashasha anasema katika sheria ya ukocha kuna vitu vingi nyuma yake, kwanza ikiwa ni wasifu,
rekodi zinazoonyesha mafanikio na aina gani ya soka ambalo anatumia, hivyo vinasaidia kujua
kocha wa aina gani anafaa. “Timu ikishindwa tunashuka moja kwa moja kwa kocha, lakini
wachezaji waliopo wanaendana na mfumo wa kocha husika? Hatuwezi kujua Yanga hii tatizo ni
lipi kwani kuna usajili mwingi umefanyika, hata dirisha dogo unaweza ukafanyika tena halafu
akaja kocha mwingine pia,” anasema.

CHANZO: MWANANCHI

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic