November 27, 2019


Yanga inasaka wachezaji kwa ajili ya kuboresha safu yao ya ushambuliaji na sasa mpango wa kumnasa straika wa Biashara United, Innocent Edwin, raia wa Nigeria, unakwenda vizuri wakiwa wamemtengea kitita cha Sh milioni 30 ili asaini mkataba katika usajili wa dirisha dogo unaoanza wiki tatu zijazo.

Mnigeria huyo anatajwa kwenye usajili huo katika kukiimarisha kikosi hicho kilichopanga kuimarisha safu ya ushambuliaji kwenye usajili huo utakaofunguliwa Desemba 16, mwaka huu.

Yanga wanataka kusajili straika huyo aliyewahi kuzifunga Simba na Yanga msimu uliopita na Azam FC msimu huu. Hiyo inakuja baada ya safu yao ya ushambuliaji waliyokuwa nayo kuonekana butu.

Katika usajili mkubwa waliosajiliwa ni Juma Balinya, David Molinga, Sadney Urikhob, Issa Bigirimana, Patrick Sibomana na Maybin Kalengo. Wote hao wameshindwa kufikia katika kiwango ambacho Yanga walitarajia.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya Benchi la Ufundi la Yanga, uongozi huo umepanga kumsajili mshambuliaji huyo kutokana na kuimudu vizuri ligi ya ndani na kikubwa wao nguvu na akili zao wamezielekeza kwenye ubingwa wa msimu huu.

Chanzo hicho kilisema mabosi hao tayari wamemfuata kwa siri mshambuliaji huyo aliyebakiza miezi sita kwenye mkataba wake na Biashara.

Kiliongeza kuwa tofauti na jina hilo, yapo mengine manne, wote wanaocheza nafasi ya ushambuliaji, kati ya hao wengine ni kutoka nje ya nchi, yupo Michael Sarpong anayeichezea Rayon Sports ya Rwanda, wengine wazawa ni Cleophas Mkandala (Prisons), Ayoub Lyanga (Coastal Union) na Ditram Nchimbi (Polisi Tanzania).

“Tayari kaimu kocha mkuu Boniphace Mkwasa alishaikabidhi ripoti yake ya usajili kuelekea dirisha dogo kabla ya usajili wenyewe kuanza, kati ya mapendekezo yake ya kwanza ni kuhakikisha wanamsajili mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao.

“Kama uongozi tayari tumeanza kuwafuatilia baadhi ya washambuliaji kati ya hao yupo huyo Innocent anayeichezea Biashara katika msimu huu na lengo ni kuimarisha safu yetu ya ushambuliaji.

“Kikubwa kinachotufanya tumfuate Innocent ni kutokana na kuzoea kucheza ligi ya ndani yenye miundombinu mibovu ya uwanja, hivyo ninaamini tukimpata kikosi chetu kitaimarika zaidi,” alisema mtoa taarifa huyo. Chanzo hicho kilisema Yanga imemtengea straika huyo Sh milioni 30 za usajili.

Alipotafutwa mshambuliaji huyo kuzungumzia hilo alisema: “Mimi bado mchezaji halali wa Bisahara kama Yanga wakinihitaji, hamna shida wao wafuate taratibu za usajili tu, hakuna mtu anayekataa kuchezea klabu kubwa Afrika.”

Kwa upande wa Yanga, Kaimu Mwenyekiti wa timu hiyo, Frederick Mwakalebela, alisema: “Muda wa usajili bado haujafika, hivyo tusubirie muda ufike.”

1 COMMENTS:

  1. Kama Yanga wakifanikiwa kumpata Innocent Edwin atawasaidia sana..He is a good player

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic