RWANDA SASA KUTUMIA SINDANO KWA WAATHIRIKA WA UKIMWI, ITADUMU KWA WIKI NANE
TIBA ya sindano badala ya vidonge vya kila siku kwa wagonjwa wa ukimwi nchini Rwanda imeshika kasi na sasa iko katika awamu ya mwisho.
Wizara ya afya ya Rwanda imetangaza kwamba mnamo miaka michache ijayo, wagonjwa wanaotumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi hawatalazimika tena kutumia dawa za kila siku ikiwa sindano ambayo imekuwa ikifanyiwa majaribio itafanikiwa.
Rwanda ni mojawapo ya nchi zinazohusika na mpango wa jaribio la dawa ya sindano ya virusi vya ukimwi ambayo inachukuliwa kuwa njia bora zaidi ya matibabu.
Ofisa mkuu wa mamlaka ya afya nchini Rwanda, Daktari Sabin Nsanzimana, ametangaza kwamba majaribio ya matumizi ya sindano badala ya vidonge vya kila siku kwa wagonjwa wa ukimwi yameshika kasi na sasa yako katika awamu ya mwisho.
“Ni mwaka mmoja sasa tukiwa tunafanya haya majaribio ya kutumia sindano ambayo itakuwa ni moja kwa wiki nane badala ya mgonjwa kumeza kidonge kimoja kila siku. Kuna dawa aina mbili zilizochanganywa kwenye sindano.,’ amesema.
Daktari huyo ameongeza kusema kwamba majaribio ya njia ya matumizi ya sindano ndiyo ya kisasa kabisa katika utoaji wa matibabu na mapambano siyo tu dhidi ya ukimwi bali pia maradhi ya kudumu.
Hii ni habari iliyopokelewa vyema na baadhi ya wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini Rwanda ambao hutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.
Mwanamke ambaye hakutaka jina lake litajwe, anasema alijua kwamba aliambukizwa ukimwi mwaka 2012 na kuanza kutumia dawa ya kufubaza ugonjwa huo.
”Habari ya majaribio ya sindano nimeipokea vizuri kabisa kwa sababu natumia kidonge kimoja kila usiku. Kuna hatari hata ya kusahau kutumia kidonge kwa wakati mwafaka. Sindano ya kila miezi miwili ni afadhali kinachobaki tu najiuliza ni lini sindano hizo zitaanza kutufikia?”
Wizara ya afya ya Rwanda inasema kwamba majaribio yamefika katika awamu ya nne ya utafiti ambayo ndio ya mwisho kabla ya dawa kusambazwa sokoni na kwamba hatua hiyo inaweza kuchukua muda usio chini ya mwaka mmoja kuanzia sasa.
Ripoti ya utafiti wa hivi karibuni kuhusu maambukizi ya ukimwi nchini Rwanda imebainisha kwamba ni asilimia tatu tu ya wananchi walioambukizwa virusi vya ugonjwa huo. Pia ripoti hiyo ilisema kuwa wanaotumia dawa za kupunguza makali ya ukimwi ni asilimia 94.
0 COMMENTS:
Post a Comment