Na Saleh Ally
WAKATI mwingine inakuwa ni vigumu sana watu wengi kuwaeleza wakaamini kwamba Bundesliga ni ligi ngumu sana.
Bundesliga ya Ujerumani ambayo hapa nyumbani inaonekana katika King’amuzi cha StarTimes ni moja ya ligi ngumu ambazo zimekuwa zina mambo mengi yenye mvuto na yanayokulazimisha kuangalia karibu kila mechi hadi mwisho.
Wadau wengi wa mpira wamekuwa wakilia na Bundesliga kwamba timu inayokuwa bingwa ni ileile, huenda hii ni kutokana na nguvu kubwa ya Bayern Munich.
Munich si Ujerumani tu, hawa ni vigogo wa Ulaya na moja ya timu kubwa na imara duniani kote pale unapozungumzia mchezo wa soka. Nguvu yao, imekuwa ikisumbua sana katika Bundesliga lakini kuna vipindi huwa wanakwama.
Tofauti ni moja, kukwama kwao mfano wakati wakitawala Borussia Dortmund au kile kipindi cha Hamburg na timu nyingine zilizowahi kufanya vizuri, huwa si kipindi kirefu kama inavyokuwa England au Italia.
Mfano Italia, angalia sasa ni wakati mgumu sana kwa AC Milan ambao ni vigogo hasa na Juventus wametawala kwa kipindi kirefu baada ya kuburuzwa pia kwa kipindi kirefu na unaona Inter Milan nao wanaanza kuamka kurejesha ufalme wao.
England, kulikuwa na kipindi kirefu cha Manchester United chini ya Alex Ferguson baada ya Liverpool kusumbua kwa muongo mzima na zaidi. Lakini sasa unaanza kuona Arsenal ilipita, Chelsea ikasumbua na sasa wababe zaidi ni Liverpool na Manchester City. Lazima kuna vipindi vya kuhama kutokana na wakati fulani.
Kwa sasa katika Bundelisga kuna hali inayojitokeza ambayo inaonyesha wazi kuwa unaweza kuwa wakati si mzuri sana kwa vigogo au watalazimika kufanya kazi ya ziada ili kurejea katika njia yao kuu.
Bayern na Dortmund bado hawajatulia na mambo yanaonekana si mazuri kwao, maana pamoja na ukubwa wao, si vinara wa ligi tena.
Ndani ya mechi kumi na moja tu, wamepoteza hadi mechi mbili. Unaona Bayern wako katika nafasi ya tatu, Dortmund wako katika nafasi ya sita.
Kumbuka wiki chache zimepita, Bayern walichapwa kwa mabao 5-1 na Frankfurt na mwisho wakalazimika kumfukuza kocha wao.
Unaona ni mikasa ya hali mbaya inazidi kuwaandama ingawa ligi bado ni mapema. Katika mechi 11, Dortmund wamepoteza mbili, wameshinda tano na hii ni dalili kwamba lazima wabadili gia.
Bayern wao katika mechi hizo 11, wamepoteza mechi mbili, wameshinda mechi sita. Kimwendo hadi sasa, si timu zenye nafasi kubwa ya kuwa bingwa na inakuwa kuna ulazima wa wao kupambana vilivyo.
Nimeona ni vizuri kuandika makala haya katika kipindi hiki ili kuwakumbusha wapenda soka nchini kwamba Bundesliga si ligi nyepesi na hata kama Bayern au Dortmund watajitutumua, basi ni lazima watapambana vilivyo kubadili mambo.
Si kweli huwa kila kitu kinakuwa laini tu kwao. Badala yake, hulazimika kujipanga na kujiweka sawa ili kufanya mambo yao yaende katika mstari ulio sahihi.
Angalia ndani ya mechi sita, Bayern Munich wamepoteza mbili na sare moja. Yaani wana ushindi wa mechi tatu tu, hii ni hali mbaya ya kimwenendo na inaonyesha lazima wafanye kazi ya ziada ili kujikomboa huku walipo.
Katika mechi hizo sita, Dortmund wamepoteza moja, wana sare tatu, maana yake wameshinda mbili tu. Utajifunza jambo pia.
Achana na vigogo hawa wawili waliozoeleka, vigogo wengine wanaonekana kuwa hoi zaidi hata zaidi ya Bayern na Dortmund.
Schalke 04, moja ya timu bora na tajiri, iko katika nafasi ya saba baada ya mechi 11 ikiwa imeshinda tano, imepoteza mechi mbili na sare nne. Utaona kuwa Bundesliga hadi sasa ni tatizo kwa vigogo.
Kigogo mwingine ni Bayer Leverkusen, ninaamini unawakumbuka hawa wakati ule wa akina Barrack, wanafika hadi fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid na baadaye wakawa tishio hata kwa Bayern.
Kwa sasa wako katika nafasi ya nane, maana katika mechi 11, wameshinda tano, wamepoteza tatu na wana sare tatu pia.
Unaweza kijiuliza nani anawafunga hawa vigogo? Pia jiulize tuendelee kuwaita wadogo wanaowatumbua vigogo wa Bundesliga? Maana yake kwa sasa waliokaa kileleni si vigogo sana.
Borussia Monchedgladbach ndio wanaongoza ligi wakifuatiwa na RB Leipzig. Ingawa tofauti ya pointi si kubwa sana, maana yake kuna jambo linaendelea ndani ya Bundesliga na vigogo wanapaswa kusimama hasa ili kurudi katika nafasi walizozizoea.
Ndio maana nikasisitiza, unaweza kuendelea kuangalia kupitia StarTimes ili uone utamu wa Bundesliga na namna vigogo wanavyohangaika kwa kuwa mambo si lainilaini kama ambavyo imekuwa ikionekana.
MSIMAMO KABLA YA MECHI ZA JUZI JUMAMOSI BUNDESLIGA
P W D L GF GA Pts Form
1.M.Gladbach 11 8 1 2 24 11 25 WWLWWW
2.Leipzig 11 6 3 2 29 12 21 LDDLWW
3.Bayern 11 6 3 2 29 16 21 WLDWLW
4.Freiburg 11 6 3 2 20 12 21 WDLWDW
5.Hoffenheim 11 6 2 3 16 14 20 LWWWWW
6. Dortmund 11 5 4 2 23 15 19 DDWDWL
7.Schalke 04 11 5 4 2 20 14 19 WDLDWD
8.Leverkusen 11 5 3 3 17 15 18 WDLDLW
0 COMMENTS:
Post a Comment