MAMBO yanazidi
kupamba moto ambapo kwa sasa kombe la Shirikisho linazidi kuchanja mbunga kwa
kila timu kuvuna kile ilichokipanda ndani ya dakika 90 jambo ambalo linaongeza
utamu wa soka ndani ya uwanja.
Tunaona
kwamba kuna timu ambazo zimeingia kushiriki zikiwa hazijui zinataka nini jambo
ambalo linafanya ziambulie kichapo kikubwa kutokana na kushindwa kujiandaa vema
huku zile zilizojiandaa zikipata ushindi.
Ukweli
kwenye mpira huwa haubadiliki timu iliyojiandaa vema ndiyo inapata matokeo ila
ile ambayo inajiingiza kwenye propaganda na maneno kibao ni maumivu hupokea
mwisho wa siku.
Tumeona
kwamba kuna timu ambazo hazijui utamu wa Ligi Kuu zinawapa taabu wakubwa ambao
wanashiriki ligi hii sio miujiza bali ni maandalizi ya timu husika mwisho wa
siku inapata matokeo chanya.
Tukuyu Stars
imeonyesha umwamba na ufahari wa kujiandaa bila kujali inacheza na timu iliyo
kwenye hatua gani bali ilijikubali na ikajipanga mwanzo mwisho.
Baada ya
dakika 90 iliibuka na ushindi wa mabao 4-3 mbele ya Singida United ambayo
inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara jambo ambalo linaonyesha kwamba vijana
walijipanga na walikuwa na nia ya kile wanachokifanya.
Kujipanga
kwao nje na ndani ya uwanja kumewapa matokeo chanya na wanasonga mbele huku
wakiwaacha Singida United wakitafuta pale ambapo walikwama wanastahili pongezi
katika hilo.
Sio Tukuyu
tu hata Coastal Union nao walionja joto ya jiwe kwa kutolewa na timu ambayo
haishiriki ligi kuu jambo linalomaanisha kwamba kila mmoja anaweza, African
Sports nao wanastahili pongezi licha ya kushinda kwa changamoto ya penalti.
Kwa timu
ambazo zimepewa zigo la mabao sio jambo la kufurahisha kwani mchezo wa mpira
sio sawa na rede timu ifungwe mabao mengi inamaanisha udhaifu kwa timu ni
mkubwa na hazijachukulia umakini mashindano haya.
Ukianza na Iringa United pamoja na Arusha FC hizi kwa sasa inaonyesha zimefungwa mabao mengi zaidi kuliko timu nyingine ambazo zinashiriki michuano ya kombe la Shirikisho.
Licha ya
kufungwa na timu ambazo zinaitwa kubwa na kongwe bado zinastahili kuonyesha
ushindani na ukomavu kwa kile ambacho wanacho kwenye mashindano haya kwani
fainali kila timu ina nafasi ya kushinda.
Yanga ambayo ilipata ushindi wa mabao 4-0 mbele ya Iringa United kabla ya watani zao Simba kushinda mabao 6-0 mbele ya Arusha FC wanastahili pongezi ila hawa waliofungwa nao wanastahili kujitathimini wapi walikwama.
Ikumbukwe kuwa Simba iliyoshinda mabao 6-0 ni ile iliyofungwa mabao 3-2 na Mashujaa ambao nao walikuwa ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita jambo ambalo linamaanisha kwamba hata timu zinazoitwa kubwa zinafungika.
Kuna umuhimu mkubwa kwenye michuano ya Shirikisho kwa timu kucheza kwa kujituma na kutumia tahadhari kubwa hasa zinapocheza na wale ambao wanaona wamewazidi uwezo kwa kutumia akili nyingi na mbinu.
Timu nyingi
zimekuwa zikishiriki michuano katika hali ya ukawaida bila ya kuwa makini jambo
ambalo linawafanya wapoteze ushindi mapema kabla ya mechi kuisha.
Tumeona
Simba wenyewe wamekiri kwamba msimu uliopita walishindwa kuyapa uzito mashindano
haya jambo lililowapa chati Mashujaa ambao nao msimu huu wamepoteza mapema
kwenye hatua ya 62.
Wakati
uliopo kwa sasa kwa timu ambazo zinashiriki michuano ya kombe la Shirikisho
kuona namna gani zinapata matokeo chanya kwani siri ya ushindi kwenye mpira ni
kujiandaa.
Timu zilizopata nafasi ya kusonga mbele zinatakiwa kujipanga upya zisipate vichapo vya aibu kwa kuwa ukubwa wa mashindano hauchangiwi na idadi ya mabao bali umakini wa wachezaji.
Kila timu ambayo itajipanga vema ina nafasi ya kushinda bila kujali aina ya timu ambayo inacheza nayo endapo itaamua kuongeza nguvu mwanzo mwisho ina nafasi ya kupata matokeo chanya.
Kila
mchezaji anatakiwa atumie nguvu zake zote na akili kutafuta matokeo na sio
kujidanganya kwamba hayana faida mashindano haya ambayo yanaendelea kushika
kasi.
Tunahitaji
kuona bingwa anakuwa ni yule aliyestahili kwa kupambana mchana hata usiku
kupata matokeo chanya kwa kuwa mshindi ana nafasi ya kupeperusha bendera ya
taifa kwenye michuano ya kimataifa.
Hatua nzuri
ambayo ipo kwa timu shiriki zile za ligi daraja la kwanza na la pili ni muda
wao kujipanga vema kupambana kwa ajili ya mechi za ushindani ambazo
zinaendelea.
Kila siku wachezaji wanastahili kujiuliza ni kazi gani ambayo wanaifanyia timu yao bila kujali aina ya michuano ambayo wanashiriki kwa sasa.
Imani yangu
ni kwamba waamuzi watafuata sheria 17 za mpira kuendeleza ule ubora na utamu wa
mechi ambazo unaendelea kwa sasa.
Mashabiki ni
wakati wenu kuendelea kujitokeza kwa wingi kuzipa sapoti timu zenu
zinapobambana ili zipate matokeo chanya ambayo mnayahitaji.
0 COMMENTS:
Post a Comment