December 5, 2019



HAKUNA asiyependa kitu kipya. Mimi napenda. Wewe unapenda. Kitu kipya kina mvuto wake. Wapo wanaotamani kupata mwanamke mpya kila siku. Wapo wanaotamani nguo mpya.

Kwani Patrick Aussems ni nani? Ni Kocha wa zamani wa Simba ambaye mpaka sasa Simba imevunja mkataba wake w jumla na amesepa mazima.

Ni kocha wa zamani aliyesimamishwa kwanza kutekeleza majukumu yake wakati kuni na maji moto vikiendelea kutayarishwa! na vilipokamilika kazi yake ikamalizwa.

Mpira wa Tanzania na hasa ndani ya Klabu za Simba na Yanga kuna muda unaongozwa na tabia za kuchoka watu. 

Wapo wachezaji wengi wanaachwa kwenye timu sio kwa sababu ya kushuka kiwango, hapana, ni sababu za kuchokwa tu.

Umecheza muda mrefu sana inabidi umpishe mchezaji mpya. Makocha nao maisha yao ni hayo hayo. Hata ushinde kombe gani Tanzania, utachokwa tu.

Emmanuel Amunike aliipeleka Tanzania kwenye michuano ya Afcon 2019, lakini alipotua Bongo, tukamchoka. Amissi Tambwe miaka kadhaa nyuma baada ya kuibuka Mfungaji Bora Ligi kuu Tanzania Bara akiwa na Simba, msimu uliofuata alichokwa na kuondolewa. Hakuna cha ajabu.

Simba wamekuwa na Msuguano karibu mwezi mzima na kocha wao mkuu, Patrick Aussems. Sioni chochote cha kushangaa hapa. Sioni maajabu yoyoye. Kiufupi Simba wamemchoka Aussems. Hakuna jambo lingine.

Kwani Patrick Aussems ni nani pale Msimbazi? Jibu ni rahisi tu. Ni kocha aliyeipa Simba mafanikio ndani ya kipindi kifupi lakini amechokwa kwa sasa. Muda wa kukusanya virago umewadia na yametimia.

Hizi timu za Kariakoo hata kama ukiwapa ubingwa wa dunia, wakikuchoka utaenda tu. Kocha Mcameroon, Joseph Omog aliwapa Simba ubingwa wa Azam Sports Federation Cup na kuwarejesha kwenye michuano ya kimataifa baada ya kukosa kwa miaka mitano, lakini ilifika wakati alichokwa. Muda wa Omog ulipofika mwisho aliondoshwa pamoja na kuwa Simba ilikuwa inaongoza ligi.

Hakuna sababu hata moja yenye mashiko ambayo Simba wameitoa mpaka sasa juu ya hiki kinachoendelea baina ya klabu na kocha wao.

Nimemsikiliza mtendaji mkuu wao, Senzo Mazingisa, sijasikia kitu. Nimemsikiliza Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda, nako hakuna jipya.

Patrick Aussems kwa muda wa mwaka na kidogo sasa ni kocha mwenye mafanikio ndani ya klabu hiyo na kwangu naona anaondoka kama mshindi baada ya Simba kutangaza rasmi kuachana naye.

Ni kocha aliyefanikiwa kuipa Simba ubingwa wa Tanzania Bara na kuipeleka timu hatua ya robo fainali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita. Hii kazi haijawahi kuwa jambo jepesi.

Ni kweli Simba msimu huu wameshindwa kutamba kimataifa, lakini bado walikuwa na nafasi ya kuanza kujipanga upya kuelekea msimu ujao. Ukiniuliza kwani Patrick Aussems ni nani pale Msimbazi? Jibu langu ni fupi tu. Ni kocha aliyefanikiwa na Simba lakini amechokwa.

Baada ya kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba leo hii wanasahau mchango na Aussems! Sina tatizo na kocha kuondoka kwa sababu hatokuwa na kwanza wala wa mwisho.

Makocha wanafukuzwa kila siku, lakini kuna namna timu za Tanzania zinapaswa kubadilika. Wakati mwingine zinajichelewesha zenyewe!

Azam FC wametimua makocha wengi sana pengine kuliko  Simba na Yanga katika Kipindi cha miaka 10 ya hivi karibuni, lakini hakuna kubwa lolote walilopata. Mchezo wa soka wakati mwingine unahitaji muda kwa walimu na wachezaji kupata mafanikio.

Mabadiliko ya Mara kwa Mara ya wachezaji na makocha hufanya timu kuwa mpya kila siku. Simba mpaka sasa  wamemchoka tu Aussems. Bado sijasikia sababu yoyote ya msingi kutoka kwenye uongozi inayojitosheleza kuachana na kocha.

Muda wa kutamani kocha mpya umefika. Ni kweli Simba wana fedha na watamleta kocha mwingine tena huenda akawa na rekodi nzuri kuliko Aussems, lakini wakubali kuanza upya.

Kila kocha ana mbinu zake, kila kocha ana aina ya wachezaji wake anaowahitaji. Simba inataka kurudi tena nyuma wakati ilikuwa imeanza kukaa sawa. Kutofanya vizuri msimu huu kwenye michuano ya Afrika bado sioni pia kama Simba tayari wamefikia ubora wa kucheza hatua ya makundi kila msimu.

Simba ni kubwa sana Tanzania, lakini Afrika bado wanatakiwa kuwa na subira. Aussems bado angeweza kubaki na Simba kupigania ubingwa mpaka mwisho wa msimu, kisha Simba wangekuwa na uwanja mpana wa kufanya tathimini na maamuzi.

Bado Aussems angeweza tu kuivusha Simba. Sina tatizo na wao kuachana na kocha lakini nina tatizo na muda na sababu zao.

4 COMMENTS:

  1. Bila shaka baada ya kumsikiliza CEO wa zamani wa Simba, Crescentius Magori, kuhusu Aussems sasa utaandika upya makala yako.

    ReplyDelete
  2. Hakuna bongo hapa siasa tu zimejaa unafukuza kocha halafu akija mwingine wachezaji walewale ndio nini jibu wachezaji awasajiliwi na kocha bali ni viongozi

    ReplyDelete
  3. Taabu yako Saleh umekuwa mwandishi wa matukio .Simba ndio wamemuajiri Aussems na ndio waliomfukuza kazi.Ukubali wewe nani?Unajipa ujiko usiokuwa nä maana.Magori ameelezea kwa upana nataraji pamoja na uwezo wako mdogo wa kuandika makala ya uchambuzi kwani unarudia rudia tu hoja zako.
    Simba ni taasisi huru nä Ina uwezo wa kufanya maamuzi kwa manufaa yao bila kungoja eti watu waridhike.
    Unapojaribu jaribu kujifanya kwamba unahodhi ukweli na weledi nä wengine wote wanafanya makosa basi inabidi utafakari na kuangalia upya uwezo wako wa kuchanganua mambo. Kukosoa huku hujui ukweli wote ni ujahili na kujipa uwezo usiokuwa nao.

    ReplyDelete
  4. Kwenye kila jambo kuna two sides of the coin .Wacha kujudge maamuzi ya Simba bila kusikiliza na kuelewa .Umejaribu kusikiliza ukweli wa pande zote.Su ba wewe ni kanjanja kama yule mtangazaji wa EFM aliyesema Aussems "ni mzungu bwana hawezi kufanya hayo anayodaiwa kufanya"?
    Uandishi wa michezo na uchambuzi una safari ndefu Tanzania.Mungu tusaidie .

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic