HAKUNA asiyependa
kitu kipya. Mimi napenda. Wewe unapenda. Kitu kipya kina mvuto wake. Wapo
wanaotamani kupata mwanamke mpya kila siku. Wapo wanaotamani nguo mpya.
Kwani
Patrick Aussems ni nani? Ni Kocha wa zamani wa Simba ambaye mpaka sasa Simba imevunja mkataba wake w jumla na amesepa mazima.
Ni kocha wa zamani
aliyesimamishwa kwanza kutekeleza majukumu yake wakati kuni na maji moto
vikiendelea kutayarishwa! na vilipokamilika kazi yake ikamalizwa.
Mpira wa
Tanzania na hasa ndani ya Klabu za Simba na Yanga kuna muda unaongozwa na tabia
za kuchoka watu.
Wapo wachezaji wengi wanaachwa kwenye timu sio kwa sababu ya
kushuka kiwango, hapana, ni sababu za kuchokwa tu.
Umecheza
muda mrefu sana inabidi umpishe mchezaji mpya. Makocha nao maisha yao ni hayo
hayo. Hata ushinde kombe gani Tanzania, utachokwa tu.
Emmanuel
Amunike aliipeleka Tanzania kwenye michuano ya Afcon 2019, lakini alipotua
Bongo, tukamchoka. Amissi Tambwe miaka kadhaa nyuma baada ya kuibuka Mfungaji
Bora Ligi kuu Tanzania Bara akiwa na Simba, msimu uliofuata alichokwa na
kuondolewa. Hakuna cha ajabu.
Simba
wamekuwa na Msuguano karibu mwezi mzima na kocha wao mkuu, Patrick Aussems.
Sioni chochote cha kushangaa hapa. Sioni maajabu yoyoye. Kiufupi Simba
wamemchoka Aussems. Hakuna jambo lingine.
Kwani
Patrick Aussems ni nani pale Msimbazi? Jibu ni rahisi tu. Ni kocha aliyeipa
Simba mafanikio ndani ya kipindi kifupi lakini amechokwa kwa sasa. Muda wa
kukusanya virago umewadia na yametimia.
Hizi timu za
Kariakoo hata kama ukiwapa ubingwa wa dunia, wakikuchoka utaenda tu. Kocha Mcameroon,
Joseph Omog aliwapa Simba ubingwa wa Azam Sports Federation Cup na kuwarejesha
kwenye michuano ya kimataifa baada ya kukosa kwa miaka mitano, lakini ilifika
wakati alichokwa. Muda wa Omog ulipofika mwisho aliondoshwa pamoja na kuwa
Simba ilikuwa inaongoza ligi.
Hakuna
sababu hata moja yenye mashiko ambayo Simba wameitoa mpaka sasa juu ya hiki
kinachoendelea baina ya klabu na kocha wao.
Nimemsikiliza
mtendaji mkuu wao, Senzo Mazingisa, sijasikia kitu. Nimemsikiliza Kaimu Mwenyekiti
wa Simba, Mwina Kaduguda, nako hakuna jipya.
Patrick
Aussems kwa muda wa mwaka na kidogo sasa ni kocha mwenye mafanikio ndani ya
klabu hiyo na kwangu naona anaondoka kama mshindi baada ya Simba kutangaza rasmi kuachana
naye.
Ni kocha
aliyefanikiwa kuipa Simba ubingwa wa Tanzania Bara na kuipeleka timu hatua ya robo
fainali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita. Hii kazi
haijawahi kuwa jambo jepesi.
Ni kweli
Simba msimu huu wameshindwa kutamba kimataifa, lakini bado walikuwa na nafasi
ya kuanza kujipanga upya kuelekea msimu ujao. Ukiniuliza kwani Patrick Aussems
ni nani pale Msimbazi? Jibu langu ni fupi tu. Ni kocha aliyefanikiwa na Simba
lakini amechokwa.
Baada ya
kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba leo hii
wanasahau mchango na Aussems! Sina tatizo na kocha kuondoka kwa sababu hatokuwa
na kwanza wala wa mwisho.
Makocha
wanafukuzwa kila siku, lakini kuna namna timu za Tanzania zinapaswa kubadilika.
Wakati mwingine zinajichelewesha zenyewe!
Azam FC
wametimua makocha wengi sana pengine kuliko Simba na Yanga katika Kipindi cha miaka 10 ya
hivi karibuni, lakini hakuna kubwa lolote walilopata. Mchezo wa soka wakati
mwingine unahitaji muda kwa walimu na wachezaji kupata mafanikio.
Mabadiliko
ya Mara kwa Mara ya wachezaji na makocha hufanya timu kuwa mpya kila siku.
Simba mpaka sasa wamemchoka tu Aussems. Bado sijasikia sababu yoyote ya
msingi kutoka kwenye uongozi inayojitosheleza kuachana na kocha.
Muda wa
kutamani kocha mpya umefika. Ni kweli Simba wana fedha na watamleta kocha
mwingine tena huenda akawa na rekodi nzuri kuliko Aussems, lakini wakubali
kuanza upya.
Kila kocha
ana mbinu zake, kila kocha ana aina ya wachezaji wake anaowahitaji. Simba
inataka kurudi tena nyuma wakati ilikuwa imeanza kukaa sawa. Kutofanya vizuri
msimu huu kwenye michuano ya Afrika bado sioni pia kama Simba tayari wamefikia ubora
wa kucheza hatua ya makundi kila msimu.
Simba ni kubwa
sana Tanzania, lakini Afrika bado wanatakiwa kuwa na subira. Aussems bado
angeweza kubaki na Simba kupigania ubingwa mpaka mwisho wa msimu, kisha Simba
wangekuwa na uwanja mpana wa kufanya tathimini na maamuzi.
Bado Aussems
angeweza tu kuivusha Simba. Sina tatizo na wao kuachana na kocha lakini
nina tatizo na muda na sababu zao.







Bila shaka baada ya kumsikiliza CEO wa zamani wa Simba, Crescentius Magori, kuhusu Aussems sasa utaandika upya makala yako.
ReplyDeleteHakuna bongo hapa siasa tu zimejaa unafukuza kocha halafu akija mwingine wachezaji walewale ndio nini jibu wachezaji awasajiliwi na kocha bali ni viongozi
ReplyDeleteTaabu yako Saleh umekuwa mwandishi wa matukio .Simba ndio wamemuajiri Aussems na ndio waliomfukuza kazi.Ukubali wewe nani?Unajipa ujiko usiokuwa nä maana.Magori ameelezea kwa upana nataraji pamoja na uwezo wako mdogo wa kuandika makala ya uchambuzi kwani unarudia rudia tu hoja zako.
ReplyDeleteSimba ni taasisi huru nä Ina uwezo wa kufanya maamuzi kwa manufaa yao bila kungoja eti watu waridhike.
Unapojaribu jaribu kujifanya kwamba unahodhi ukweli na weledi nä wengine wote wanafanya makosa basi inabidi utafakari na kuangalia upya uwezo wako wa kuchanganua mambo. Kukosoa huku hujui ukweli wote ni ujahili na kujipa uwezo usiokuwa nao.
Kwenye kila jambo kuna two sides of the coin .Wacha kujudge maamuzi ya Simba bila kusikiliza na kuelewa .Umejaribu kusikiliza ukweli wa pande zote.Su ba wewe ni kanjanja kama yule mtangazaji wa EFM aliyesema Aussems "ni mzungu bwana hawezi kufanya hayo anayodaiwa kufanya"?
ReplyDeleteUandishi wa michezo na uchambuzi una safari ndefu Tanzania.Mungu tusaidie .