Wiki jana uongozi wa Klabu ya Simba ulitangaza ujio wa kocha wao mpya raia wa Ubelgiji, Sven Vandenbroeck ambaye amechukua mikoba ya Mbelgiji mwenzake, Patrick Aussems ambaye alifungashiwa virago vyake hivi karibuni.
Sven atasaidiana na mzawa Selemani Matola ambaye pia amejiunga na timu hiyo hivi karibuni akichukua nafasi ya Denis Kitambi.
Hata hivyo kwa kuanza harakati zao za kuhakikisha Simba inakuwa imara, taarifa ni kuwa kocha huyo amekutana na mapendekezo usajili mezani ya jina la nahodha na kiungo mkabaji wa Polisi Tanzania, Henerico Kayombo.
Inaelezwa kuwa Matola ndiye ambaye amekuwa na ushawishi mkubwa wa kuomba kiungo huyo asajiliwe na kama mambo yakienda vizuri anaweza kuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa chini ya benchi jipya la ufundi.
Kayombo ambaye pia ana uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, anaweza kuiongezea Simba nguvu katika nafasi ya kiungo mkabaji ambayo kwa sasa inamtegemea zaidi Jonas Mkude.
Matola amefikia hatua hiyo kutokana na kuona kuwa nafasi ya kiungo mkabaji katika kikosi cha Simba bado haijapata mtu sahihi tangu alipoondoka Mghana, James Kotei, hivyo anaamini Kayombo ambaye pia ni mwajiliwa wa Jeshi la Polisi anaweza kuliziba pengo hilo kwa ufanisi mkubwa.
“Jina hilo limefikishwa kwa uongozi na kama utaridhia basi unaweza kumsajili Kayombo, kwani ni bonge la kiungo anayejua vilivyo majukumu yake uwanjani,” kilisema chanzo cha habari hiyo.
Hata hivyo alipoulizwa, Matola kuhusiana na hilo hakuwa tayari kusema chochote lakini Ofisa Habari wa Polisi Tanzania, Frank Lukwaro alisema: “Taarifa hizo bado hajafika mezani kwangu ndiyo kwanza nazisikia.”
Lakini kama wanamtaka kweli Kayombo basi wao waje tu tuzungumze, lakini Kayombo amejiriwa na Jeshi la Polisi na ni askari.
“Kama tutakubaliana nao basi na sisi tutawaomba watupatie Said Ndemla
“Kuhusu, Kayombo kuacha kazi ya uaskari kama tutakubaliana nao basi kuna taratibu zitafanyika ili aweze kupata kibali cha kuitumikia timu hiyo na muda wake ukimalizika anaweza kurudi kuendelea na majukumu yake kama kawaida,” alisema Lukwalo.
KIUNGO RASTA NAYE ATAJWA
Wakati huohuo, jina la kiungo mwingine wa Polisi Tanzania, Baraka Majogolo nalo limetajwa katika mipango hiyo ya Simba.
Kwa sasa Majogolo yupo kwenye kikosi cha Kilimanjaro Stars kinachoshiriki Kombe la Chalenji huko Uganda.
Inadaiwa kiungo huyo amefikia katika hatua nzuri ya usajili kutua Simba na kinachosubiriwa ni tamko la kocha mpya wa Simba.
ATINGA MAZOEZINI
Katika mazoezi ya jana ya Simba yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Simba Mo Arena, Bunju jijini Dar, Sven alifika lakini hakushiriki katika mazoezi, badala yake Matola ndiye ambaye alikuwa akiendeleza mchakato wa kuwanoa wachezaji huku kocha huyo mpya akiwa pembeni ameshika kitabu kidogo na kalamu akiandika mambo kadhaa kutokana na mazoezi hayo.
Kila siku viungo wakati timu imejaza viungo timu imejaza maviungo wengi wanakaa benchi huku timu ikiwa haina washambuliaji wa kati. Kama ni kweli basi tunakwama sehemu.
ReplyDelete