December 2, 2019





Na Saleh Ally
NILIFANIKIWA kujua mapema sana kuhusiana na uamuzi wa Klabu ya Simba kutaka kuachana na kocha wake mkuu, Patrick Aussems raia wa Ubelgiji.


Nafikiri hadi leo ni takribani wiki tatu hivi, baada ya wiki moja baada ya kujua Simba walishapitisha nikashea mtandaoni nikisema Aussems ametufundisha mengi wakati akiwa Simba na atakuwa sehemu ya mchango wa kukuza soka nchini.


Kilichofuatia kama ilivyo, wehu wa mtandaoni ambao wana uwezo mdogo wa kujenga hoja wakaanza kutukana. 

Kawaida, ninapoona mtu anatukana matusi hata katika kitu cha kawaida kabisa ambacho kinachotakiwa ni kujenga hoja tu, yeye anatukana naachana naye.

Nafikiri kama ninavyosema aina ya watu hao ni wehu au wendawazimu, ninaamini baada ya kuona Aussems amefukuzwa, sasa wataelewa uwezo wao wa kufikiri na kujifunza kuacha kukurupuka kwa kila jambo.

Mafunzo yanatokana na ujenzi wa hoja, mnajadili na kupata kitu chanya, watu wa aina hii ni watu wanaojitambua. Wapo pia mitandaoni.

Hii si hoja hasa ya msingi niliyotaka kuzungumzia, acha nianze. Ishu ya kufukuzwa Aussems, ilijulikana takribani wiki tatu zilizopita lakini nikaelezwa uamuzi ulipitishwa mwezi uliopita na baada ya hapo, propaganda ikaingia katikati tena bila sababu za msingi.




Ukiangalia zilianza kuzungumzwa hoja kadhaa kuhusiana na Aussems, kwamba aliondoka katika kituo chake cha kazi, alishindwa kujibu kwa nini aliondoka, alikataa kutoa tiketi aliyosafiria, anaingilia mambo yasiyomhusu (hayakutajwa) na kadhalika na hizi ndizo siasa.

Inaonekana wazi uongozi wa Simba haukuwa umefurahishwa katika mambo kadhaa ya kinidhamu na kiwango cha kikosi baada ya kuonekana kama Aussems ameshindwa kuyadhibiti.

Kutokana na hilo, kukawa na muingiliano kwa maana ya CEO wa Simba, Senzo Mazingisa akiamini si sahihi na kocha huyo akiendelea kufanya anachoona sahihi.

Nidhamu mfano, ilionekana kuna wachezaji wameporomoka viwango, mfano Cleotus Chama, Sharaf Eldin Shiboub na Jonas Mkude na bado Aussems akaendelea kuwatetea licha ya kwamba walikuwa “wanaharibu”.

Suala la kiwango, Simba haijashuka kwa kiwango cha kutisha ingawa imekuwa ni kupanda na kushuka. Sababu ya kwamba alishindwa kusonga hadi Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, ikizungumzwa sasa hivi inakuwa ni kitu cha kushangaza kidogo kwa kuwa tulitarajia isikike kipindi kile cha UD Songo, Simba ikitolewa kiulaini kabisa.


Kwa kifupi kwa maana  ya ushindani wa ligi, bado Aussems alikuwa ni kocha saizi ya Simba na anayewafaa kabisa. Lakini kwa uhalisia kwamba tayari chemistry ya ndani ya Simba katika suala la utendaji, ilikuwa tayari imevurugika.

Hivyo, Simba kumuondoa Aussems kwa maana ya kuangalia mbele na kutengeneza mipango madhubuti ni sahihi kabisa lakini hakukuwa na haja ya kuingiza siasa ndani yake.

Kunapoingia siasa, kunaonyesha bado viongozi wa Simba wana mwendo wa kizamani wa wale viongozi wanaowaogopa wanachama hata wanapokuwa wanataka kufanya kitu sahihi.

Kama unawahofia wanachama kwa kipindi hiki maana yake kuna walakini katika lile unalotaka kuliamua. Kama unaona uko sahihi, chukua uamuzi, fanya mabadiliko watu wakijua kabisa viongozi wamechukua hatua. Ndio maana wanachama na mashabiki wakawaamini kuwa pale katika nafasi hizo muhimu.

Mpira wetu ukianzia Chama cha Soka Tanzania au Fat wakati huo, hadi sasa TFF, klabu za Simba na Yanga na nyingine zenye watu wengi, siasa ndani ya soka imekuwa adui mkubwa wa mabadiliko na maendeleo ya mchezo huo.

Vizuri zaidi ni kubadilisha huu mwelekeo na siasa ibaki kwa wanasiasa, huku katika michezo mambo yaende ‘fast and accurate’, yaani haraka na uhakika na bila kupindisha mambo.








FIN.

9 COMMENTS:

  1. Unakaripia kutukana na wewe unatukana. Siasa zipi zitaje?Wacha kuandika sweeping statements zisizo na ushahidi.Kujipa ujiko nä kujisifu kwamba ulijua uamuzi huu wiki tatu zilizopita!
    Kwa ushahidi gani?

    ReplyDelete
  2. Pilpili usizozila zinakuwashia mini. Waachie wenye kujuwa masilaha yak

    ReplyDelete
  3. WAPENZI WA SIMBA NI MAMBUMBUMBU!

    ReplyDelete
  4. Mbumbumbu ni wewe na yule aliwaita wapuuzi.Wewe ni mpuuzi tu.

    ReplyDelete
  5. Salehe wakati mwengine acha upumbavu. Tena unatakiwa kuheshumu maamuzi ya viongozi amabao ndio wanaogharamika kuendesha timu zao.Mfano Horoya ya Guiene wao hawakuwa na subira kumfukuza kocha wao baada ya kufanya vibaya klabu bingwa Africa. Na ni kocha huyohuyo aliewafikisha robo fainali klabu bingwa Africa msimu uliopita. Siasa gani unazozingumzia zilizotumika katika kuachishwa kazi kocha wa Simba? Siasa ni huu ujinga wa kukariri yakwamba mazali Ausems kaifikisha Simba robo faianli basi hata akifanya vibaya aachiwe tu? Hata Tottenham spurs nao ni siasa tu zilizomuondosha kocha wao. Hata Yanga nao ni siasa tu ndizo zilizomuondosha kocha wao,hata Arsenal nao ni siasa tu ndizo zilizomuondosha kocha wao, hata KMC nao ni siasa tu ndizo zilizomuondosha kocha wao, hata mbeya city nao ni siasa tu ndizo zilizomuondosha kocha wao na orodha ya timu zilizofanya hivyo ni nyingi tu sio rahisi kuzitaja zote na kwanini Simba? Kama siasa au sio siasa Simba na uongozi wake ni klabu ya Tanzania yenye usubutu wa kufanya mambo mengi ya kuleta maendeleo ili kuinua soka la Tanzania lakini watanzania mara nyingi hasa tunaojifanya watu wa mpira hasa kwa upande wa uandishi hutafuta sababu zisizo za msingi wala za kiuweledi ili kujenga dhana kwa umma labda uongozi timu fulani hasa timu zetu hizi Simba na Yanga yakuwa viongozi hufanya maamuzi bila ya uweledi kitu ambacho ni upuuzi mtupu.Masoud Djuma alipoondoshwa Simba watu waliponda na kuchonga sana ila baada ya kuondoka Simba ilianza kufanya vizuri.Nnachotaka kusema tuheshimu maamuzi ya viongozi wa Simba na kama kuna hoja za msingi ni zile zinazolenga kuifanya Simba na wana Simba kusonga mbele na kuacha kuleta hoja mfu kama za kufukuzwa kwa Ausems ambae hata iwe vipi ndio keshamalizana na Simba so what? Na kwanini tusilete orodha na mjadala wa makocha ambao tunaamini wataipeleka Simba mbele zaidi alipofikia Ausems?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Umempasha na ukweli yeye Saleh Jembe ndio mleta siasa ktk mpira.Ina maana uamuzi uliopitishwa na jopo la wajumbe ndani ya bodi hawana weledi ila tukuamini wewe pekee yako Saleh?Amefukuzwa Pochettino itakuwa Aussems.Muhimu Simba ihakikishe inapata kocha bora zaidi ya Aussems

      Delete
  6. Well said Mkuu.Natamani sheria za kuzuia waandishi wa mazoea zianze kufanya kazi.Bofi nzima ya Simba na CEO wao ni wapumbavu nä wewe ndio mwerevu Saleh Ally?Wakati mwingine ficha ujahili wako kwa kukaa kimya.

    ReplyDelete
  7. Ni kweli @Saleh Ally, ulichokiandika hapa ni ukweli huyu kocha hajafanya kitu cha kutushawishi kuwa ni kitu cha kumfukuza bali kama ni kosa lilikuwa ni jambo la kumwonya na kuendelea, Mwenendo wa Simba ulikuwa mzuri sana

    Timu zetu hizi zimejaa wanasiasa na watukanaji wa mitandaoni tu ila uhalisia huu , kama timu inataka mabadiliko lazima kufanya maamuzi bila kuogopa wanachama na ukuangalia wote wanaopiga kelele mitandaoni ni wale ambao siyo wanachama wa kweli maana hawachangii pato la timu , hawana kadi, timu haiwezi kuendeshwa na wapiga kelele, hatutafika kwenye malengo

    ReplyDelete
  8. Ila timu ziendeshwe na siasa za uuzaji wa magazeti? Ahsante Tanzania.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic