Baada ya tetesi za muda mrefu za aliyewahi kuwa kiungo mkabaji wa Simba, James Kotei, kutakiwa na Yanga, hatimaye uongozi wa timu hiyo, umefunguka juu ya dili la mchezaji huyo kusajiliwa na Yanga.
Kotei aliitumikia Simba kwa misimu mitatu na kufanikiwa kuipa ubingwa wa ligi mara mbili kabla ya msimu mpya wa 2019/20 kutimkia katika timu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambako huko mambo yake hayajakaa vizuri.
Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz, aliliambia Championi Jumatatu kuwa timu hiyo bado haijafunga usajili wa wachezaji, hivyo muda ukifika wa kutaja wachezaji watakaowasajili basi wataweka wazi kila mmoja afahamu, kama atakuwa Kotei basi watafahamu pia.
“Yanga bado hatujafunga usajili wa wachezaji hivyo tunaweza kuongeza wachezaji wengine, kuhusu James Kotei kusajiliwa na Yanga ni suala la muda tu kwani mambo yakiwa tayari, tutawatangazia mashabiki wetu,” alisema Nugaz.
Endapo Yanga itakamilisha usajili wa mchezaji huyo, itakuwa na idadi ya viungo nane ambao saba waliopo hadi sasa ni Haruna Niyonzima, Feisal Salum, Papy Tshishimbi, Abdulaziz Makame, Balama Mapinduzi, Mohamed Banka na Said Juma Makapu.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment