KUELEKEA kufunguliwa kwa dirisha la usajili mdogo mwezi huu Januari, kulikuwa na tetesi nyingi za usajili zinazomuhusu Erling Haaland ambaye aliuwasha moto kweli akiwa anaitumikia Red Bull Salzburg.
Ubora wake hasa wa kufunga mabao na kujua wapi asimame ili aweze kutupia mpira wavuni iliongeza thamani yake na kuwa straika chipukizi mwenye thamani kubwa aliyekuwa akiwindwa na vigogo wa Ulaya.
Manchester United ya England ndiyo timu ambayo iliaminika itamsaji kutokana na kuhusishwa kwa ukaribu lakini badala yake Haaland akaibukia Borussia Dortmund inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga’.
Usajili huo ni kama uliwashtua watu wengi kwa kuwa haikutegemewa lakini mwisho wa siku huo ndiyo ukweli halisi, sasa imebaki kazi moja tu kuona straika huyo akifanya kile ambacho kilisababisha dunia ikawa inamtazama kwa jicho la utofauti.
Nahodha wa Dortmund, Marco Reus anaamini ujio wa Haaland katika kikosi hicho unaweza kuwa na faida kubwa kwa kuwa anafiti katika mfumo wa timu hiyo kama ilivyokuwa kwa Robert Lewandowski.
Ni miaka sita sasa imepita tangu Lewandowski alipoondoka Dortmund kwenda Bayern Munich lakini kwa muda mrefu Dortmund wamekuwa wakipata wakati mgumu kupata straika ambaye anaweza kufiti aina ya uchezaji wao kama ilivyokuwa kwa huyo waliyempoteza akaenda kwa wapinzani wao wa jadi, Bayern.
Baadhi ya mastraika waliofuata baada ya Lewandowiski kuondoka ni Adrian Ramos, Ciro Immobile na Michy Batshuayi lakini bado walishindwa kwenda sambamba na staili ya uchezaji ya Dortmund, hata ule uchezaji ambao ulikuwa ukipendelewa kutumiwa na kocha wao wa zamani, Jürgen Klopp nao ulipotea.
Hivyo sasa, Marco Reus anaamini Bundesliga ambayo unaweza kuishuhudia kupitia king’amuzi cha StarTimes kwa kulipia kifurushi cha Uhuru kwa Sh 18,000 tu, inaweza kunogeshwa na Haaland kama ilivyokuwa enzi za Lewandowski alipokuwa Dortmund.
Mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang aliyefunga mabao 98 katika Bundesliga akiwa Dortmund alikuwa mkali na bora lakini hakuwa akicheza katika aina ya uchezaji wa timu hiyo kwenye eneo la ushambuliaji.
Lewandowski akiwa Dortmund alikuwa ni mtu wa kati anayeweza kuwavuruga walinzi lakini Auba alikuwa akitokea pembeni na alisaidiwa na kasi yake, ndiyo maana alipata mabao mengi.
Reus anaamini sasa namba tisa mpya wa Dortmund anaweza kufiti vizuri katika mfumo wao kutokana na umbo lake, urefu, lakini tofauti yao kubwa labda ni katika namba ya jezi atakayovaa kwa kuwa ‘dogo’ mpya kwa sasa anavaa jezi namba 17 wakati mkongwe ambaye yupo Bayern alikuwa akivaa namba tisa.
“Sijui kama tumewahi kuwa na straika wa aina ya Robert Lewandowski tangu alipoondoka,” anasema Reus na kuongeza:
“Haaland anatupa nafasi ya kuwa na machaguo mengi uwanjani, tunaweza kucheza katika staili tofauti.
“Ni mtu ambaye yuko wazi, muhimu kwanza ni kumfahamu, baada ya kumjua ametutengenezea njia nzuri ya kujua na jinsi ya kufanya naye kazi, najua mambo mazuri yatakuja taratibu.”
Kuonyesha kile anachokisema Reus kinaweza kuwa na maana ni kwa kuwa tangu Lewandowski alipoondoka kwao akiwa mfungaji bora wa Bundesliga mwaka 2014, Dortmund ilitoa mfungaji bora mara moja tu.
Mfungaji huyo ni Aubameyang ambaye wao wenyewe wanakiri kuwa alikuwa mshambuliaji mzuri lakini mwenye staili tofauti ya uchezaji, alikuwa mfungaji bora wa ligi hiyo mwaka 2017.
Lakini tofauti na hapo, Dortmund wamekuwa wakipata wakati mgumu katika kufunga mabao mengi kwa kuwa hawajapata kile ambacho wamekuwa wakikihitaji.
Hata msimu huu napo wamekuwa na wakati mgumu, wameyumba kwa kiasi fulani, wanashika nafasi ya nne hadi sasa baada ya mechi 17, wakiwa wameshapotea mechi nne.
Wamezidiwa pointi tatu na wapinzani wenzao, Bayern Munich, nafasi mbili za juu zikiwa katika timu ambazo hazikufikiriwa, RB Leipzig na Borrusia M’gladbach, hivyo sasa ujio wa Haaland unategemewa na wengi kuiamsha timu hiyo ilipo.
“Ukitazama kikosi chetu kina ubora mzuri na kinahitaji mataji, hilo ndilo jambo la muhimu kutoka kwetu,” anasema Reus.
0 COMMENTS:
Post a Comment