KUNA wakati mgumu ambao mashabiki huwa wanapitia na kipindi hicho huwa ni matokeo mabaya ambayo wanayapata kupitia timu zao wanazozipenda pale ambapo wanaona zinashindwa kupata matokeo chanya.
Wapo ambao wanapenda kujifungia ndani na kuona shida kutoka nje pale ambapo timu yake inashindwa kupata matokeo ambayo alikuwa anayafikiria.
Mashabiki wana hulka moja nzuri na ya ajabu muda mwingine kutokana na kushindwa kuzuia hisia zao pale ambapo timu yao inashindwa kupata matokeo Uwanjani.
Hulka hiyo inawapasa iwe ni chachu ya kujitokeza kwa wingi Uwanjani kuwashuhudia wachezji wakipambana kutafuta matokeo kwenye mechi zote bila kujali timu yao inacheza na nani.
Tunatambua kwamba michuano ya Kombe la Shirikisho inaendelea japo kwa sasa imefika hatua ya 32 na Ligi Kuu Bara pia inaendelea ila bado kumekuwa na mwamko mdogo wa mashabiki kujitokeza uwanjani.
Tunaona kwamba kuna baadhi ya mechi hazina kabisa wale mashabiki ambao walianza kupeperusha bendera za timu zao awali kutokana na kujitoa mwanzo mwisho.
Kwa sasa wamekuwa wakichagua tu aina ya mchezo wanaoutaka kisha wanakwenda wakati huu tuvunje ule utaratibu wa kupuuzia kujitokeza uwanjani kushangilia timu zetu.
Mwaka huu 2020 ambao tumeuanza kwa mapenzi ya Mungu basi tunapaswa tufanye vitu vya tofauti na kuendelea kumshukuru yeye katika kila jambo bila kusahau kwamba tunaendelea kuombeana ili kufikia mafanikio.
Hakuna ambaye anapenda kuona timu yake inaboronga ila wakati mwingine inatokea kutokana na ushindani ambao upo na kila timu inahitaji matokeo uwanjani hivyo mshindi lazima atokee.
Mashabiki wamekuwa na kasumba ya kuumba matokeo mikononi mwao na kuyaweka mfukoni kisha wanaingia nayo uwanjani hili halipo sawa tuachane nalo mwaka 2020 tuanze kufanya mambo kwa utofauti..
Kujitabiria mazuri inaruhusiwa ila kuamini kwamba ulichotabiri kitatokea hilo ni suala lingine inabidi liwe kichwani mwako mwenyewe huku ukifikiria kupambana kwa ajili ya kutoa sapoti kwa timu yako muda wote.
Kuna mengi ambayo wachezaji wanapaswa wayatazame hasa pale wanapopewa nafasi ndani ya uwanja kazi yao inabidi itimizwe ipasavyo kwani wakiboronga wanaharibu mfumo mzima wa kuaminiwa na benchi la ufundi.
Ushindi ambao unazungumziwa kwenye soka hauwezi kubadilika huwa unakuwa ni sare, kupoteza ama kushinda huu ndio ushindi kwani wakati timu moja inaumia ikiwa imepoteza ipo iliyoshinda hivyo yote ni matokeo yanatakiwa yakubaliwe.
Ugumu na kiburi ambacho kilikuwa kwenye mioyo ya mashabiki kwa kushindwa kujitokeza uwanjani mwaka uliopita kiwekwe kando na kila mmoja abadilike na kuanza kufanya mambo kisasa zaidi ya mwaka jana.
Kwenye mpira kuna kanuni kubwa ambayo wachezaji wamekuwa wakifundisha ni kuhusu nidhamu ya mchezo nje na ndani ya Uwanja endapo wachezaji watafanikiwa kufuata hilo watafanikiwa.
Uwezo binafsi wa wachezaji pale ambapo wanashindwa kuzitumia mbinu za mwalimu na kuweza kurejea upya kwenye mfumo wa mwalimu utawasaidia kupata matokeo.
Rai yangu kwa wachezaji wajiamini waache
hofu isiyokuwa na maana kwa kuwa wana weza kufanya makubwa ambayo yataushangaza ulimwengu wa mpira.
Januari 4, 2020 uwanja wa Taifa kutakuwa na mchezo wa kukata na shoka kati ya Simba na Yanga ambao watakuwa wakicheza mchezo wa ligi kwa mara ya kwanza msimu huu watakutana uwanjani.
Hapa kila mmoja ana kazi na kufanya kile ambacho ataelekezwa na mwalimu na sio longolongo mpira ni ndani ya uwanja na sio nje ya uwanja.
Tunahitaji kuona soka la kweli na burudani kwa timu zote mbili tuachane na ile kasumba ya kuleteana fujo ama zama za kuleteana visa na visasi muda wake umwekwisha kwa sasa ni amani tu inapaswa itawale.
Wachezaji ndio ambao wamepewa dhamana ya kukamilisha shughuli uwanjani, mashabiki wajitokeze kwa wingi na kwa utulivu kuzipa sapoti timu zao.
Ushindani mzuri ni ule ambao hata unayeshindana naye ukimshinda hauwezi kumuonea huruma wala huwezi kujibeza unaamini umefanikiwa kupambana, ikiwa tofauti kuna maumivu unayapata.
Tanzania yote na dunia kiujumla itakuwa ikifuatilia ni muda mzuri kwa mashabiki na wachezaji kuutumia mchezo huo kuwa sehemu sahihi ya kujitangaza ndani na nje ya Nchi kitaifa na kimataifa.
Mawakala wengi wanafuatilia soka letu la Bongo itakuwa ni darasa lao la bure kujifunza kitu cha pekee kwa timu zetu zinapopambana uwanjani na kuonyesha kwamba namna gani zina wachezai wazuri ambao wanaweza kupata dili jipya.
Malengo ya mchezaji yanapaswa yawe ni mara mbili zaidi asisahau kwamba kuanza kwa mwaka mpya kunamaanisha kwamba kuna mambo kwake yanaongezeka na majukumu yanakuwa mengi.
Ni muda mzuri kwa wachezaji wote kutambua kwamba maisha yao ni soka, wanachotakiwa kufanya ni kupambana na kucheza soka safi litakalokonga mioyo ya mashabiki na wale wengine ambao si mashabiki ila wanapenda tu kutazama ushindani.
Ushindani ukiwa bora kwenye ligi yetu ya Bongo kutafanya tusipate tabu kubwa kwenye mechi zetu zote za ushindani hasa kwa timu ya Taifa kwa kuwa tutakuwa na jeshi imara lenye nguvu.
Mashabiki wote kwangu ni rai yangu kuona kwamba kila mmoja atakayekwenda uwanjani awe sawa na aamini kwamba timu yake ina matokeo matatu mkononi na sio kitu kingine.
Inabidi atambue kwamba kuna sare, kufungwa ama kushinda hakuna hesabu mpya licha a kwamba mwaka ni mpya kwenye uwanja wa soka.
Akipatia vema kanuni hiyo basi asiwe na presha ya kutafuta matokeo anayoyajua yeye anatakiwa aamini katika matokeo yake yote matatu na baada ya dakika tisini jibu lake atalipata baada ya mechi kuisha.
Ligi yetu inazidi kukua taratibu na kwa kuwa mwaka ni mpya kuna mengi ya kufanyia kazi ikiwa ni pamoja na sehemu ya kuchezea kwani limekuwa ni tatizo kubwa.
Timu nyingi zimekuwa zikipata tabu sehemu ya kuchezea kutokana na miundombinu yetu kutokuwa rafiki kwa muda wote jambo ambalo linafanya viwanja vizuri viwe vichache Bongo na vinahesabika.
Wadau tusapoti timu zetu zifanikiwe kuwa na ushindani pamoja na kupata matokeo ambayo ni chanya kwetu hasa kwa wakati tuliopo na kukumbuka kwamba ni jukumu la timu kuwa na uwanja ambao utakuwa rafiki.
Kufika uwanjani na kushangilia timu zetu ni jambo la faraja kwa wachezaji kwani wanaamini kuna watu nyuma yao ambao wanawafuatilia.
Pia mashabiki napenda niwaambie maana kuna baadhi huwa na hofu juu ya viingilio ambavyo vinapangwa kwenye timu husika ikiwa inacheza.
Suala la viingilio haipangi timu ni bodi ya ligi yenyewe ndio inafanya hivyo ile kasumba ya kufikiria timu zinatafuta faida inapaswa iwe wazi kwamba kila kitu kina utaratibu wake.
Muda ambao tunao kwa sasa ni kutafuta mbinu mbadala hasa wa kuzibeba timu zetu ambazo tunazipenda kwa hali na mali na kutoa sapoti bila kuchoka hali itakayosaidia kufikia malengo ambayo tunahitaji.
Sheria 17 za mpira zinapaswa zifuatwe kwa haki bila upendeleo kwani kama waamuzi watakuwa wanaendesha kwa kufuata hisia kutaumiza timu na maendeleo ya soka letu.
0 COMMENTS:
Post a Comment