February 6, 2020


HATIMAYE kiungo Bruno Fernandes amekamilisha usajili wake Manchester United kwa dau la pauni milioni 68 (Sh bilioni 203) akitokea Sporting Lisbon ya nyumbani kwao Ureno.

Januari yote iliyopita, tetesi zilikuwa ni nyingi kuhusu Manchester United kumwinda kiungo huyo lakini hatimaye mambo yametimia.

Sasa baada ya kumpata mtu wao, mashabiki wa Manchester United watarajie nini kutoka kwa kiungo huyu mchezeshaji?

Hapa chini tumekuchambulia mambo 6 yanayoonyesha ubora wa Fernandes uwanjani.

MKALI WA MASHUTI YA MBALI
Moja ya sifa kubwa za Fernandes ni uwezo wake wa kupiga mashuti ya mbali, wakati mwingine anachungulia nafasi hata akiwa katikati ya uwanja.

Mreno huyu huwa hasiti linapokuja suala la kupiga mashuti ya mbali akitumia guu lake la kulia lenye nguvu.

Moja ya klabu ambazo alifanikiwa kuzifunga mabao ya mbali ni Liverpool katika sare ya 2-2 mwanzoni mwa msimu.

MTAALAM WA MIPIRA ILIYOKUFA

‘Maia’s Cannon’, hilo ndilo jina analojulikana Fernandes kwa mashabiki wake wa Ureno kutokana na uwezo wake wa kupiga mashuti ya nguvu na sahihi. Lakini pia jamaa huyu ni mtaalam wa mipira iliyokufa, kwa maana ya faulo na penalti.

Fernandes amekuwa akifurahia kupiga mipira ya faulo na ni mbunifu katika kuipiga mipira ya aina hiyo.

Kila baada ya kumaliza mazoezi na timu, amekuwa akijifua kivyake namna ya kupiga mipira ya faulo kama ambavyo amekuwa akifanya Mreno mwenzake, Cristiano Ronaldo.

ANAKABA KUANZIA MBELE
Fernandes mara nyingi amekuwa mmoja wa wachezaji wa kwanza kukaba na amekuwa akikabia kuanzia kwenye boksi la wapinzani wao.

Amekuwa akikaba kwa kufuata mkakati wa timu yake au kocha. Ni imara sana katika kuwatia presha wapinzani ambao wanapenda kuchezea mipira kwenye eneo la kiungo.

Katika nyakati kadhaa, akiwa na Sporting pamoja na timu ya taifa ya Ureno, alifanikiwa kupoka mipira, kumiliki na kutengeneza nafasi nzuri za kufunga kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya wachezaji wenzake.

ANATISHA KWA KONA
Ikiwa inapigwa mipira ya kona, utamuona Fernandes yupo makini mbele akisubiri mpira uangukie mguuni mwake apige shuti kuelekea kwenye lango la wapinzani.

Amekuwa akifanya hivi kwa maisha yake yote ya soka, hasa Italia alipokuwa katika kikosi cha Sampdoria.

Akiwa na Sporting, ambako amecheza kwa miaka mitatu iliyopita, alifunga mabao mengi kwa aina hii. Kwa hiyo, tarajia kumuona akizunguka zunguka katika eneo la hatari wakati mipira ya kona ikipigwa.

ANA KASI KUBWA
Moja ya sifa zake nyingine ni kasi ambayo amekuwa akiionyesha baada ya kuusoma mchezo.

Fernandes ana akili nyingi na anatambua kuwa kasi aliyonayo inaweza kusababisha mabeki wa upinzani wakajichanganya na akawasababishia matatizo wakati timu ikifanya mashambulizi ya kushtukiza.

Amehusika katika mabao mengi sana ya mashambulizi ya kushtukiza kwenye Ligi Kuu ya Ureno (Primeira Liga) na Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

MZURI KATIKA MIPIRA YA KICHWA
Licha ya kuwa siyo mmoja wa wachezaji warefu sana akiwa na urefu wa futi 5 na inchi 8, Fernandes ni bora sana kwa kupiga kichwa na amefunga mabao mengi kwa staili hiyo.

Ni wazi kwamba amekuwa akipata ugumu kwa mipira ya juu anapokutana na mabeki warefu, lakini anaweza kusoma na kuelewa eneo sahihi la kujiweka katika nafasi ya kupiga kichwa mgongoni mwa mpinzani wake.

Ni kawaida kumuona katikati ya eneo la hatari akisubiri makosa ya mabeki wa kati katika kumaki mipira ya juu, hasa wakati timu ikifanya mashambulizi ya kushtukiza.

MANCHESTER, England

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic