February 21, 2020









Na Saleh Ally
KUNA mambo mazuri yanayouma ambayo wakati mwingine unapaswa kuyasikia ili uweze kubadili jambo ili kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.

Yanga ni klabu kongwe zaidi nchini na yenye mashabiki wanaoipenda kweli. Kufanya kwake vizuri kunakuwa ni furaha ya wengi, hali kadhalika isipofanya vizuri, wanaoumia ni wengi sana.

Wataumia kama tu mambo yatakuwa hayaendi vizuri na hili litasababishwa na wale ambao wamekabidhiwa dhamana katika nyanja kadhaa.

Viongozi, wakishindwa kutimiza majukumu yao, basi mambo yanakwenda vibaya na mwisho wanazalisha maumivu. Hii inakwenda inashuka taratibu kwa makocha na baadaye wachezaji ambao wanakuwa askari wa mwisho kuipigania timu uwanjani.

Wakati mwingine unaweza kubadilika na kufanya vizuri kutokana na deni ambalo unaliona. Mfano kuwaangusha watu fulani wanaokutegemea, kuwakatisha tamaa wanaokutegemea na kadhalika.

Hii inatokea sana kwa wachezaji wengi wanaocheza katika timu za Ulaya. Mashabiki wao wamekuwa wakiwaunga mkono kwa nguvu sana. Hali inayowafanya kucheza kwa juhudi kubwa kuhakikisha wanafanya vizuri.

Wachezaji wanalazimika kujituma zaidi wakijua ni jukumu lao kuhakikisha timu inafanya vizuri ili kuepusha maumivu kwa wale ambao wanawaunga mkono.
Faida ya mashabiki si kushangilia pekee kama ambavyo wengi wanaamini. Mashabiki ni watu ambao wanakuwa msaada katika kushangilia timu inapokuwa uwanjani, bado kuna faida nyingi na ambazo zimo ndani yao na wao ni msaada mkubwa katika timu ndani ya klabu.

Anza kujiuliza klabu bila mashabiki, bila shaka inakuwa haina maana yoyote, si vibaya kusema ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Hivyo mashabiki wanaweza kuwa msaada uwanjani kweli lakini kuna mengi.

 Mashabiki wanalipa viingilio magetini, timu inapata kipato. Sasa wanategemewa kununua jezi, fedha inaingia kuwa msaada katika klabu lakini wao ndio kama nilivyosema mwanzo, tegemeo pale uwanjani timu inapocheza.

 

Mashabiki wana faida kubwa na wanapaswa kupewa vitu vizuri hasa ambavyo vimo ndani ya uwezo wa wachezaji ambao wanakuwa wawakilishi wao.

Binafsi naona wachezaji wengi wa Yanga bado hawajaonyesha uwezo wao katika kiwango chao hasa au kinachostahili na mawili tu katika hili, yanaweza kuwa sahihi.

Kwanza, wakubali kwamba hawana uwezo ulio sahihi kuipigania Yanga na kuhakikisha inafika kwa usahihi. Lakini pili, ni kuwa hawajajituma katika kiwango sahihi kinachoweza kuifanya Yanga kuwa katika kiwango bora na kufanya vizuri.


Nasema haya mawili, mfano wapo ambao wanapaswa kusema hawana uwezo sahihi kama walivyotarajiwa. Lakini wapo wanaopaswa kukubali kwamba hawajajituma na Yanga haipaswi kuteseka au kuyumba kama hali ilivyo sasa.

Angalia, katika mechi zake 21 za Ligi Kuu Bara, Yanga imeshinda 11, hii ni kama 55% tu ya mafanikio ya ushindi. Kati ya hizo ina sare saba ambazo ni zaidi ya 39% ya mechi zake na imepoteza mechi tatu.

 Unaona bila ya ubishi kwamba Yanga haipo katika hali nzuri na ndani ya mechi hizi 21, hali inaonyesha wazi kuwa hawana nafasi ya kubeba ubingwa labda miujiza.


Itakuwa miujiza kama watabeba ubingwa kwa kuwa watalazimika kuiona Simba ikiharibu mfululizo angalau mechi tano na baada ya hapo, wasubiri kuona Azam FC inaboronga hadi kufikia nafasi wao wanaweza kupita.

Wachezaji wa Yanga bado hawaonyeshi hali ya kujituma ambayo inaonyesha mwanga kwamba wachezaji hawa watafia uwanjani kutokana na namna wanavyocheza.

Mchezaji anayetaka kushinda, mwenye hamu na aliyepania kuona timu yake inashinda, utamuona kimbia yake, anapokuwa na mpira au timu inaposhambuliwa. Mara nyingi, wachezaji wa Yanga wanacheza utafikiri timu imeshinda.

 Mechi tatu zilizopita Yanga imetoka sare. Angalia timu imeambulia pointi tatu katika mechi tatu, imefunga mabao mawili tu katika mechi tatu lakini imefungwa mawili pia. Maana yake, GD yao ni 0!

 Hii haiwezi kuwa timu inayoweza kusema itagombea ubingwa labda kama Yanga wanataka kujidanganya kwa kujipaka mafuta kwa mgongo wa chupa. Lakini kwa mwendo huu, uhalisia unaonyesha hakuna nafasi ya ubingwa kwa Yanga.

 David Molinga na Yikpe Gnamien hawana cha kusingizia, lazima wafunge ili timu yao ifanye vema kwa kuwa hilo ndilo jukumu lao, kama hawafungi, basi watengeneze mabao.

 

Viungo lazima wafanye kazi yao vizuri kuchezesha timu, kutoa pasi za mwisho lakini wa ukabaji washirikiane vizuri na safu ya ulinzi na kuhakikisha makosa yanapungua.

Kuna kitu kinasema hivi, thamani ya kitu. Wachezaji wawe wazalendo au wa kigeni, lazima wajifunze kuhusiana na thamani ya Yanga. Iko ndani ya mioyo ya watu wengi sana na wao ndio wameishikilia mioyo hiyo na wana uwezo wa kuchagua kuiachia maumivu au furaha.

Sare tatu mfululizo, mechi mbili za nyumbani. Tayari ni tatizo na hakuna mjadala, waliopewa jukumu la kuhakikisha kuna utendaji sahihi, hawafanyi majukumu yao sahihi na inavyotakiwa ni kubadilika au kutafuta njia nyingine na mlango wa kutokea itakuwa sahihi. Wasibane nafasi za wale ambao wangeweza kuwa hapo na kusaidia. Waoneeni huruma mashabiki wengi wakiwemo wale ambao wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kuona timu hiyo ikicheza.





1 COMMENTS:

  1. Kazi yao ni kuifikiria Simba kila siku ya mungu,utawaweza hawa jamaa?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic