February 21, 2020





NA SALEH ALLY
MOJA ya sifa kubwa ya Ligi Kuu England ni soka la ushindani, waamuzi safi, viwanja safi na kadhalika. Hii pia ni sifa ya ligi nyingine zinazoitwa kubwa kama La Liga, Bundesliga.

Kunaweza kuwa na sababu nyingi sana zinazoweza kuifanya ligi kuwa kubwa, maarufu na inayoheshimika na waamuzi ni sehemu yake.

Waamuzi wanapocheza katika kiwango bora kabisa, bila ya shida mechi zitaisha kwa usalama, hakuna rundo la malalamiko yanayofuatana.

Kunapokuwa na uaminifu, maana yake watu wengi wanaanza kutamani nao kuwa sehemu ya ligi hiyo kwa mambo kadhaa, mfano kushuhudia mechi uwanjani au kuwa wadhamini.
Timu kuwa tajiri lazima ifanye biashara na biashara yenyewe itatokana na mpira lakini lazima wanaofanya nao biashara waanze kuwaamini wao na wanaoshirikiana nao.

Wao ni kama klabu, wanaoshirikiana nao ni wadau wakiwemo waamuzi ambao kama watafanya kazi yao kwa weledi na kujenga uaminifu kwa wadau wengine ambao ni watazamaji, kunakuwa na nafasi ya kuingia kwa fedha nyingi. Kwa maana waingie uwanjani na kuzifanya klabu kuingiza fedha ili ziendelee kujiendesha vizuri.

Watazamaji hao wana faida nyingine ya ziada, faida hii si wao kwenda kutazama mpira lakini huwa wanatazama na kuona kuwa kama wafanyabiashara wanaweza kutangaza bidhaa zao.

Shabiki wa Yanga au wa Simba, Azam FC au timu nyingine, ndio wenye nafasi ya kujua utamu na ubora wa Ligi Kuu Bara. Huyu ndiye mwenye nafasi ya kuishauri kampuni anayoifanyia kazi, au kuamua kwa kampuni anayoimiliki kuingiza fedha zake katika mpira.

Ataweza kufanya hivyo kama ataona ligi hiyo ina ubora na sehemu ya ubora huo ni kuendesha au kuchezeshwa kwa weledi unaozingatia sheria 17 za soka kwa haki kabisa.

 Kama kila siku kutakuwa na malalamiko ya uonevu, kuwa timu fulani imependelewa au waamuzi wanazinyima timu haki, yupi atafurahia kuipeleka kampuni yake au anayoifanyia kazi katika sehemu ambayo anaona umakini ni mdogo?


Hakuna umakini kwa maana ya dhuluma au umakini wa kiwango cha chini kwa kuwa waamuzi hawafanyi kazi yao vizuri na kwa weledi na wamekuwa wakiadhibiwa lakini kinachofuatia, makosa yanaendelea kama kawaida.
Unaona baada ya adhabu za waamuzi kutangazwa na walioadhibiwa wakatajwa, waamuzi wakaonekana wazi kuwanyima haki Yanga na Simba.

Juzi tena tumeona, Simba walinyimwa penalti dhidi ya Kagera Sugar, Juma Nyosso akimkwatua John Bocco kwa makusudi kabisa ndani ya eneo la 18. Siku hiyohiyo, Matheo Anthony aliifungia Polisi Tanzania bao halali kabisa dhidi ya Yanga lakini mwamuzi akakataa.



Waamuzi wanaokataa ni wasaidizi, yule aliyeinyima Simba penalti, ulikuwa upande wake na si mbali ya macho yake. Yule aliyeinyima Polisi, alikataa bao lakini hakuonyesha hata tatizo lilikuwa ni lipi!

Hili tatizo huenda linaweza kuwa la muda lakini wazi linapoteza sifa ya Ligi Kuu Bara, linapunguza umaarufu na heshima yake na linaweza kuchangia watu wengi kupungua kwenda viwanjani lakini linaweza kusababisha waliokuwa tayari kuingiza fedha katika klabu zinazoshiriki ligi hiyo au ligi yenyewe, wakaamua kutoingia kwa kuwa wafanyabiashara wanahitaji sehemu sahihi kutangaza biashara zao.


Waamuzi lazima nao waone aibu, wabadilike kweli na waonyeshe huwa wanapata mafunzo sahihi kufanya kazi yao badala ya kufanya mambo ambayo hata kwa mtu wa kawaida anaweza kuona kuna tatizo.

 Mfano mtu kuangushwa ndani ya eneo la 18, haihitaji utaalamu wa kutisha. Angalia mtu kufunga akiwa hajamgusa mtu halafu ukasema si bao, hakika inakera, inaumiza na inashusha thamani ya ligi na kuwakimbiza wanaoweza kuwa karibu kwa maana ya wadau.













1 COMMENTS:

  1. hapa uwezi ona mashabiki wa vyura wakikomen wao wana var yao ambaayo inaanonyesha tu Simba amebebwa

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic