HIVI sasa
kila kona stori kubwa ni uwepo wa ugonjwa wa Covid-19 unaotokana na Virusi vya
Corona.
Jamii nzima imekumbwa
na taharuki juu ya uwepo wa virusi hivyo ambavyo vinaenea kwa kasi mno. Wana
michezo nao ni miongoni mwa waathirika wa Virusi vya Corona.
Tumeshuhudia
nchi za wenzetu kwa maana ya barani Ulaya wakianza kuahirisha ligi zao kutokana
na ishu hiyo, awali zilianza kwa kuchezwa bila ya uwepo wa mashabiki.
Ikaonekana
kwamba si suluhisho la kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo, ligi zikasimamishwa
moja kwa moja kwa takribani siku 30.
Tanzania pia
ligi zake zimesimamishwa, hiyo ilikuja baada ya mapema wiki hii Serikali
kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutangaza kufunga shughuli mbalimbali
hapa nchini zikiwemo za soka kwa siku 30.
Kuanzia
Jumanne ya wiki hii lilipotoka agizo hilo, ligi zote zikasimamishwa ambapo
tunatarajia ligi hizo kuendelea mwezi ujao.
Wakati ligi
zikisimamishwa, kuna baadhi ya timu zilikuwa tayari zimesafiri kwenda kucheza
mechi sehemu fulani, hivyo zile gharama zimeenda na maji.
Ingawa ni
kweli timu hizo zimepata hasara, lakini ni jambo zuri pia kwao kutocheza mechi
hizo kwani pengine ingeweza kuleta madhara kwao.
Serikali
imekuwa ya kwanza kutoa elimu juu ya kujikinga na virusi hivyo ambavyo hapa
nchini hadi sasa kuna wagonjwa kadhaa wameripotiwa kukumbana navyo.
Pia
tumeshuhudia klabu nazo zikiwa mbele kusapoti kile inachofanya Serikali. Hivi
sasa kila siku tunaona kwenye akaunti za mitandao ya kijamii ya klabu
mbalimbali hapa nchini zikiposti juu ya namna ya kujikinga na Corona.
Hili ni
jambo zuri na la kizalendo ambalo linaonyesha nje ya kuwa klabu za soka lakini
kwenye suala la kijamii zimejitokeza mbele na kutoa elimu kwa watu wake ambao
wanazifuatilia.
Suala hilo
liwe funzo kwa timu nyingine na zichukue elimu ya kwamba zina jukumu la kufanya
hivyo kwa sababu elimu ambayo wataitoa inafika kwa watu wao ambao wamekuwa
wakiwashabikia.
Kuwapa elimu
litakuwa jambo la maana sana kwa sababu mtawakinga na ugonjwa huo ili kwa hapo
baadaye watakapokuwa wazima waje kuwashangilia kwa mara nyingine.
Hakuna
ambaye kwa sasa haufahamu ugonjwa huu ulivyo hatari sana. Umeua maelfu ya watu
duniani mpaka sasa. Kwa Tanzania bado hakuna taarifa za kifo, lakini ni vema
tukaendelea kupambana nao na kuushinda.
Nichukue
nafasi hii kulipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa juhudi zao za
makusudi za kutii agizo la Serikali kwa kusimamisha ligi zake. Hivyo shikilieni
hapohapo kwani usalama wa afya kwa kila mmoja ni jambo muhimu sana.
Pia TFF
imeenda mbali zaidi kwa kusema baada ya kupita hizo siku 30, kuna uwezekano
mkubwa wa ligi kuchezwa bila ya mashabiki. Hili pia limekaa poa.
Kubwa zaidi
katika kuchukua tahadhari, baada ya kupita siku hizo 30, wachezaji wote
watapimwa kabla ya kucheza mechi. Ni uamuzi sahihi kabisa.
Niwaombe
Watanzania wasiuchukulie kawaida huu ugonjwa, wafahamu upo na ni hatari sana.
0 COMMENTS:
Post a Comment