HIVI
karibuni, ulimwengu wa soka duniani kote ulipata mshangao baada ya nyota wa
zamani wa Barcelona na Timu ya Taifa ya Brazil, Ronaldinho De Assis Moreira
maarufu kama Ronaldinho Gaucho kukutwa na hatia ya kutumia hati feki ya
kusafiria kuingia nchini Paraguay.
Ronaldinho
na kaka yake aitwaye Roberto ambaye pia ni meneja wake katika masuala ya
biashara, walikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi kabla ya kufikishwa mahakamani
ili kusikiliza mashitaka hayo.
Juhudi
mbalimbali zinafanyika ili kuhakikisha Ronaldinho aliyekiri kosa anamalizana na
soo hilo, lakini bado staa huyo yuko kwenye hatari ya kukumbana na kifungo
iwapo mahakama itajiridhisha kuhusu shauri hilo.
Kwa upande
wangu nadhani kisa hiki cha mkongwe huyu wa soka kina mengi ya kuwafundisha
nyota wetu hapa nchini kwani wachezaji wengi ambao wanapata bahati ya kufanya
vizuri na kuwa katika viwango vya juu hupata upofu wa ustaa na kusahau kuwa
kuna maisha baada ya majina makubwa na ustaa walionao.
Sekeseke
hili la Ronaldinho liwakumbushe wachezaji wetu kuwa licha ya ustaa walionao
uwanjani, mitandaoni na kwenye media bado wanabaki kuwa binadamu kama wengine na
lolote linaweza kuwakuta.
Ni nani
alidhani kuwa mshindi huyo wa Ballon d’Or mbili na umaarufu, heshima yake
angeweza kuwa mahabusu kwa muda kwa ishu ya paspoti?
Unakuta huku
kwetu mchezaji eti kwa kuwa tu anacheza Ligi Kuu, anajulikana kwenye viwanja
vya bata na kupata ‘dm’ za kutosha za wadada wa mjini mitandaoni basi anasahau
kabisa hata kujiwekeza kwa maisha ya baadaye, mwishowe anapokuja kuachana na
soka anajikuta kabaki mwenyewe huku wale wote waliokuwa wakitumbua pamoja
wamepotea.
Ni muhimu
wachezaji wetu wakakumbuka msemo usemao “fainali uzeeni” hivyo wanapaswa
kuchagua washauri na wasimamizi sahihi katika mambo yao binafsi kipindi hiki
wakiwa wanatengeneza pesa ya kutosha.
Mchezaji
unaposema ‘role model’ wako ni Cristiano Ronaldo au David Beckham usiige tu
mikimbio yao uwanjani, unadhifu wao, au jinsi wanavyotanua na vimwana huko
Dubai na fukwe za Ibiza, bali hakikisha unaiga na akili ya uwekezaji ambayo
tunaiona kwa nyota hao ambao ni dhahiri kwa uwekezaji wanaoufanya sasa shida za
uzeeni watabaki kuzisikia kwa wengine tu.
Mara kadhaa
tumeshuhudia wachezaji ambao walitamba enzi hizo katika soka hapa nchini
wakiadhirika na kuwa ombaomba katika uzee wao huku wengi wao wakitoa sababu ya
malipo madogo waliyokuwa wakipata.
Lakini bado
hatuwezi kuficha ukweli pia kuwa kuna baadhi yao ambao macho yao yalifumbwa na
ustaa wakajua kuwa watazeeka nao kumbe ustaa ni jambo la kupita tu.








0 COMMENTS:
Post a Comment