UONGOZI wa Gwambina FC yenye maskani yake Mwanza umesema kuwa kupanda kwao Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2020/21 kumetokana na kujipanga vizuri tangu mwanzo wa Ligi Daraja la Kwanza ilipoanza.
Ushindi wa bao 1-0 walilopata mbele ya Pamba FC jana, Juni 27 kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba umewapa tiketi ya kupanda kwenye ligi kuu jumla.
Akizungumza na Saleh Jembe, Mkuu wa Idara ya Mashindano wa Gwambina FC, Mohamed Moshi Almas maarufu kama Mtabora amesema kuwa ni furaha kwa timu ya Gwambina kufikia malengo waliyojiwekea awali.
'Tulipanga kupanda ligi tukiwa na mechi mkononi na awali kazi ilikuwa mbele ya Trasnit Camp kule Dar, tuliambulia pointi moja baada ya kufungana bao 1-1, ila jana tumeibuka na ushindi mbele ya Pamba na kutupa tiketi ya kushiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao.
"Kwa sasa tunachokifanya ni kutazama namna ambavyo tutamaliza mechi zetu ambazo zimebaki mkononi kwani bado tuna kibarua mbele ya Rhino Rangers na Mashujaa," amesema.
Kwenye Kundi B, Gwambina FC mshindani wake mkubwa alikuwa ni Geita Gold, ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 34 baada ya kucheza mechi 20.
Gwambina wao wamecheza jumla ya mechi 20 wao wamefikisha jumla ya pointi 44 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote kwenye kundi hilo B.
Bao lao la ushindi lilipatikana kipindi cha pili dakika ya 90 kupitia kwa Meshack Abraham.
0 COMMENTS:
Post a Comment