July 19, 2020


LICHA ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu huu akiwa na Simba, beki wa pembeni wa timu hiyo, Gadiel Michael, hana furaha Msimbazi kiasi cha kutaka kurejea Yanga ambako alicheza msimu uliopita.

Beki huyo tangu alipojiunga na Simba msimu huu akitokea Yanga, ameonekana kukosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza chini ya Kocha Mbelgiji, Sven Vandenbroeck.

Gadiel akiwa na Yanga kwa misimu miwili alijihakikishia nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo kiasi cha kuwashawishi mabosi wa Simba kumsajili lakini huko amekwenda kukutana na upinzani mkali kutoka kwa nahodha msaidizi, Hussein Mohammed ‘Tshabalala’.

Taarifa zinaeleza kuwa, Gadiel alipeleka Yanga mkataba wake aliosaini Simba ili kuangalia uwezekano wa yeye kurejea ‘nyumbani’ lakini alikumbana na kikwazo kikubwa.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kikwazo alichokutana nacho ni timu itakayomhitaji akiwa ndani ya mkataba, basi ikubali kutoa kitita cha dola 100,000 (Sh mil 231.3) jambo ambalo Yanga wamegomea na kumtaka asubiri kwanza aumalize mkataba kisha atarejea tena msimu wa 2021/22.

Chanzo kikubwa cha kutaka kuondoka ni kukosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha timu hiyo, hali iliyomfanya akose furaha ndani ya timu hiyo iliyochukua ubingwa wake wa ligi mara tatu mfululizo msimu wa 2017/ 2018, 2018/2019 na 2019/2020.

“Kama mkataba wake usingekuwa na kipengere cha kuuvunja mkataba wake kwa timu itakayomhitaji kutoa dola 100,000, basi Gadiel angerejea kuichezea Yanga msimu ujao.

“Kwani mkataba wake ulipitiwa na mabosi wa Yanga kuonekana kubanwa na kipengere hicho kigumu ambacho yeye kitamzuia kurejea kuichezea kwa mara ya pili lakini wamemwambia amalize kwanza kandarasi yake kisha atarejea 2021/22.

“Beki huyo amepoteza nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, kitendo kilichomfanya avurugike na kuonekana kukosa furaha katika timu hiyo aliyoichezea kwa msimu mmoja akibakisha mmoja wa msimu ujao,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said, kuzungumzia hilo hakuweza kupokea simu yake ya mkononi, aidha alitafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumburi ambapo alikataa kulizungumzia suala hilo.

Chanzo: Championi

1 COMMENTS:

  1. Hii ndio mikataba sio mkataba mchezaji anacheza miezi mitatu anakuwa huru na kuanza kujiuza kwa timu pinzani. Tuendelee kijifunza

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic