July 13, 2020


TAYARI Gwambina na Dodoma FC zina tiketi mkononi na msimu ujao wa 2020/21 zitakuwa kwenye maisha ya Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kupambana kutoka Ligi Daraja la Kwanza.

Nianze moja kwa moja kuzungumzia timu zilizopata nafasi ya kutinga ligi kuu msimu ujao wa 2020/21 baada ya kupambana ndani ya Ligi Daraja la Kwanza na kufikia malengo waliyojiwekea. 

Awali timu ya Gwambina FC ndiyo iliyoanza kutangulia kujipatia nafasi ya kutinga Ligi Kuu, huku timu ya Dodoma FC ikifuatia baada ya Ligi Daraja la Kwanza kufikia tamati juzi, Jumamosi huku timu mbili zikisubiria kucheza playoff na timu mbili za ligi kuu zitakazoshika nafasi ya 15 na 16.

Ihefu wao kwenye kundi A walikuwa washindani wa ukaribu na Dodoma FC ila mwisho wa siku Dodoma wamewazidi kwa idadi ya mabao huu ni ushindani ambao tunaupenda kuona ukiendelea.

Hivyo kwa matokeo hayo Ihefu kiroho safi ina tiketi ya kucheza mchezo wa play off wataungana na mshindi wa tatu ambaye ni Majimaji.

Boma na Friends Rangers wao watacheza play off ya kubaki Ligi Daraja la Kwanza huku Iringa United,Pan African, Coasmopolitan na Mlale FC wao wakianga safari jumlajumla kwenye kundi A hivyo watakuwa watakuwa ndani ya Ligi Daraja la Pili msimu ujao.

Kwa upande wa kundi B hatma ya zile ambazo zinashuka ligi pamoja na kucheza play off zitawekwa wazi baada ya maamuzi ya Bodi ya Ligi kwani
mchezo wa mwisho kati ya Mawenzi dhidi ya Pamba haukumalizika baada ya kutokea vurugu hivyo Gwambina ana uhakika wa kushiriki ligi lakini hawa wengine ni mpaka pale maamuzi yatakapotolewa ndipo hatma yao itajulikana.

Hivyo ushindani ambao ulionekana kwenye Ligi Daraja la Kwanza tunaamini utaendelea pia kwa zile ambazo zimeshapanda.

Hatua hii imekuja kufuatia Shirikisho la Soka Tanzania ( TFF) kuweka wazi mikakati yao ya kutaka ligi ya msimu ujao kuwa na timu 16 badala ya 20 za sasa kutokana na kuwapa nafasi wadhamini kuweza kuzihudumia vyema timu shiriki ambapo timu nne kutoka ligi kuu zitashuka na mbili za chini zitacheza play off na zile mbili za daraja la kwanza zilizoshika nafasi ya pili.

Napenda kuzikumbusha na kuzipa hongera timu zilizofanikiwa kupanda ligi kuhakikisha zinakuja na mikakati madhubuti ya kuleta ushindani wa kutosha kwenye ligi na si kuja kushiriki kwa kuwa wasindikizaji.

Tunahitaji ushindani ambao ulikuwa ukitolewa Ligi Daraja la Kwanza uelekezwe ligi kuu ili kuwepo na ushindani wa kutosha na kusiwe na gape kubwa baadhi ya timu zikicheza mechi lazima zipoteze, tunahitaji kutoka huko ili kuweza kuusongesha mbele mpira wetu kwa kuwa na timu imara na za kiushindani zaidi.

Ifike wakati kila timu itambue wajibu wake ligi kuu ili kuweza kuwa na wachezaji bora watakaoleta ushindani kwa kuhakikisha maandalizi yanafanywa sasa ili itakapoanza ligi iwe kazi moja tu ya kushindana.

Tumeweza kushuhudia baadhi ya timu zilizopanda daraja msimu wa 2019/20 Namungo FC na Polisi Tanzania zimeweza kufanya vyema kwenye ligi ambapo zimekuwa zikileta ushindani wa hali ya juu.

Nimalizie kwa kuwaonya viongozi kuhakikisha wanakuwa kitu kimoja kuhakikisha malengo ya timu yanafikiwa na kusiwe na migogoro ya hapa na pale ambayo ndiyo inachangia timu kuboronga likiwemo suala la maslahi.

Kuwepo na mikakati ya pamoja ambayo itaweza kuzifanya timu ziweze kusonga mbele.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic