July 16, 2020


LIGI Kuu Tanzania Bara inazidi kujizolea umaarufu kitaifa na kimataifa na hii inatokana na ushindani uliopo kwenye timu zote ambazo zinashiriki ligi.
Ukianzia kwa wachezaji wenyewe wanacheza kwa kujitoa kwa ajili ya kupambana kutafuta matokeo ndani ya uwanja baada ya dakika 90.
Achana na wachezaji benchi la ufundi pamoja na viongoz pia wamekuwa bega kwa bega kutoa sapoti kubwa huku wakishirikiana kwenye kutimiza majukumu yao ndani ya uwanja na nje ya uwanja pia.
Hii inapendeza na inaleta picha nzuri kule ambako tunatarajia kwenda kutokana na kila mmoja kuwa na kitu ambacho anakifikiria ndani ya ubongo wake na kukifanya kwa wakati.
Huku mambo yakizidi kuwa mazuri wapo wale ambao kwa sasa ndani ya ligi maisha yao yanafika tamati kwa kuwa mwisho wa ligi wanaibukia Ligi Daraja la Kwanza.
Hamna namna ya kufanya kwa sasa kwa kuwa maisha lazima yaendelee na kwa kuwa kwenye ushindani ni lazima aonekane ambaye anashindwa basi hakuna lazima itatokea wapatikane wa kushuka.
Singida United tunaona kwamba kwa sasa mambo yamekuwa magumu kwao nao wanakwenda kuanza maisha ya Ligi Daraja la Kwanza hawana budi kujipanga kwa msimu ujao waweze kutimiza lengo la kurejea tena kwenye ligi  kuu.
Kushindwa kwa sasa haina maana kwamba wao sio bora hapana ni hesabu tu zimewagomea  wanaweza kujipanga upya wakarudi wakaendelea na kasi yao ile ya wakati ule walipopanda.
Ni ngumu kuamini ila yametokea na bado kuna timu nyingine tatu zitashuka pia mbili zitacheza play off ili kumtafuta mshindi ambaye atakuja kucheza ligi kuu.
Kikubwa kinachohitajika ni maandalizi makini na kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa wakati sahihi itaongeza ushindani na kuleta matokeo mazuri.
Pia kwa namna ambavyo timu zinashuka huku nyingine zikipanda iwe darasa kwa wengine katika kujitathimini pale watakapopanda namna ya kufanya ili kulinda nafasi zao za kubaki.
Zile ambazo zinapanda kutoka Ligi Daraja la Kwanza zina kazi kubwa ya kuanza kufanya maandalizi ili ziweze kuleta ushindani wa kweli ndani ya ligi.
Kila kitu kinawezekana ikiwa kutakuwa na mpango makini na ukweli ni kwamba kupanda ni rahisi na kushuka ni rahisi pia lakini ukishashuka kurudi huku juu huwa inakuwa ngumu.
Tazama timu kongwe kama Pamba FC, iangalie Stand United hata Njombe Mji na Majimaji bado zinapambana kurejea juu ila zinakutana na ushindani tofauti kabisa.
Matumaini yangu ni kwamba kupitia matukio haya yanayoendelea wamiliki wa timu, wachezaji pamoja na wamiliki wa timu wanaona namna mambo yanavyokwenda hivyo wataongeza umakini wakati watakapokuwa kwenye ushindani.
Tunataka kuona timu ikipanda kwenye ligi iwe na uwezo na vigezo vya kuhimili mikikimikiki ya huku kwani hakuna kuzubaa ni mwendo wa kukimbizana.
Ukiachana na ligi kuu ya wanaume pia kuna ligi ya wanawake hapa pia kuna umuhimu wa kuitazama kwa ukaribu ili kutengeneza timu makini pia kwa wanawake.
Kutokana na ushindani uliopo hasa kwenye timu za wanawake kuna umuhimu wa wadau kujitokeza pia kutoa sapoti kwa wanawake ili nao pia waweze kuleta ushindani.
Mambo yamekuwa mengi na magumu huku hasa katika masuala ya uendeshaji wa timu jambo ambalo linaumiza na kuwaliza wengi ambao wanasimamia timu zetu za Bongo.
Hivi karibuni timu ya Alliance Girls ilipata ajali wakati wakirejea nyumbani ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba wachezaji wanaendelea vizuri.
Katika hili pia iwe fundisho katika kuangalia usalama na uwepo wa wachezaji wetu kwani wanajitoa kwa ajili ya kazi kwa kufanya mchana hata usiku ila hakuna ambaye anawajali.
Kuna umuhimu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutazama namna ya kuwapiga tafu wachezaji pamoja na timu kiujumla kwani wengi hali zao bado hazijawa sawa.
Pia ugumu na ubovu wa maandalizi unafanya timu moja iwe inakusanya mabao mpaka 12 kwa kuruhusu kufungwa ndani ya dakika 90.
Katika hili ni muhimu kutazama namna maandalizi yalivyo pamoja na fedha ambazo zinatumika kwenye maandalizi kamili kwa timu.
Timu chache zina uhakika kuhusu posho na stahiki za wachezaji na hii ni mbaya kwani mambo yakiwa hivi ushindani utazidi kupungua.
Wakati mwingine tunashindwa kuwa na timu bora inayoshiriki kwenye ligi ya wanawake ambayo itasaidia kupata na kuibua vipaji.
Kufungwa mabao 10 kwa timu moja inamanisha kwamba haipo tayari kuendelea na safari ila inapambana  kutimiza wajibu wake kwa kuwa ipo shemu ya safari.
Kwa namna mambo yanavyokwenda hii haileleti afya katika maisha ya soka na ili uweze kuushinda mpira na kupata matokeo ndani ya Uwanja ni lazima kupambana.
Wakati uliopo kwa sasa kwa mechi ambazo zimebak nii timu kujipanga upya kumaliza vema lala salama huku Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF) pamoja na wadau kutazama namna mpya ya kuendelea kutoa sapoti kwa wanawake.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic