KESHO
Jumapili, msimu wa Ligi Kuu Bara 2019/20 unatarajiwa kufikia tamati ambapo
tutashuhudia mechi kumi zikichezwa huku timu 20 zikichuana vikali.
Tayari
bingwa anajulikana ni Simba na wamekabidhiwa kombe lao muda tu. Kama umesahau,
nikukumbushe kwamba baada ya kucheza na Namungo kule mkoani Lindi ndiyo
walikabidhiwa kombe.
Vita kubwa
iliyobaki sasa ni katika kupambana na janga la kushuka daraja ambapo huko vita
yake si ya kitoto kabisa.
Ikiwa tayari
Singida United imeshuka daraja rasmi kabla ya ligi kumalizika, zimebaki timu
takribani saba ambazo zinapambana zisishuke daraja.
Kuanzia timu
ya nafasi ya 13 hadi 19, ndizo zinapambana na janga hilo kwa sasa. Kumbuka timu
zinazotakiwa kushuka daraja moja kwa moja ni nne. Singida tayari, bado zingine
tatu.
Lakini kuna
zingine mbili zitalazimika kucheza mechi za mtoano ‘playoffs’ ili kupambania
nafasi zao za kubaki ligi kuu. Zitacheza dhidi ya Ihefu SC na Geita Gold.
Ngoja
nikufahamishe kitu hapa kabla sijaenda mbali zaidi. Timu zitakazoshika nafasi
ya 17, 18, 19 na 20 ndizo zitashuka daraja moja kwa moja, kisha zile za nafasi
ya 15 na 16 ndizo zitacheza mechi za mtoano.
Ukitazama
msimamo ulivyo mpaka sasa wakati timu zote zikiwa zimecheza mechi 37, Mbeya
City, Alliance, Ndanda na Singida, ndizo zinashika nafasi nne za chini, huku
Mbao na Mtibwa zikiwa nafasi ya kucheza mechi za mtoano.
Kuwa nafasi
hizo kwa sasa haimaanishi kwamba ndiyo tayari kazi imeisha kwao, bali wanaweza
kubadili upepo kulingana na matokeo ya mwisho hapo kesho.
Ndanda ina
pointi 41, Alliance sawa na Mbeya City, Mbao na Mtibwa. Pia Mwadui ina 44 kama
ilivyo kwa Lipuli.
Mwenye
pointi 41, akishinda mechi ya mwisho anafikisha 44, yule mwenye 44 akipoteza
mechi ya mwisho, wanakuwa sawa, hapo ishu ya tofauti ya mabao itaamua.
Kwa manaa
hiyo ni kwamba, vita yao ni kubwa sana. Hapa lazima jambo lifanyike kipindi
hiki msimu unamalizika.
Mamlaka
husika kwa maana ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu
Tanzania (TPLB), zinapaswa kuwa na jicho la tatu katika mechi hizi za mwisho.
Suala la
upangaji matokeo hatutaki kuliona wala kusikia limetokea kesho wakati msimu
unamalizika.
Zibeni
mianya yote ya rushwa ili kila timu iweze kupata matokeo kulingana na
ilivyojiandaa. Haitapendeza kusikia timu fulani imebebwa na nyingine kunyimwa haki
yake.
Siku zote
dhuluma si jambo zuri, timu itakayotumia njia zisizo sahihi katika kutafuta
matokeo, itakuja kuhukumiwa huko mbele. Pengine isihukumiwe na mamlaka husika,
lakini inaweza kuhukumiwa uwanjani kwa maana ya kupata matokeo mabovu msimu
ujao.
Yote kwa
yote, nizipongeze timu zote 20 zilizoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu kwani
zimeonesha ushindani mkubwa hadi sasa tunakwenda kumaliza msimu, ni timu moja
tu ndiyo imeshuka daraja.
Kuna ligi
zingine huko utakuta ligi inaendelea ikiwa imebaki mechi tatu au nne, lakini
tayari kuna timu zaidi ya moja tayari zimeshuka. Kwetu imekuwa tofauti msimu
huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment