BAADA ya vuta nikuvute ya muda mrefu kati ya uongozi wa Yanga na walinzi waandamizi wa timu hiyo, Kelvin Yondani na Juma Abdul, taarifa rasmi imeeleza kuwa wachezaji hao siyo sehemu ya kikosi cha Yanga.
Taarifa za kuachwa kwa wachezaji hao zilikuja siku chache baada ya uongozi huohuo wa Yanga kuweka hadharani majina 14 ya wachezaji waliotemwa na kueleza kuwa Juma na Yondani bado walikuwa wanaendelea na mazungumzo na uongozi.
Hatimaye muafaka ukapatikana na wachezaji wakakubali kuachwa kutokana na kushindwana kwenye masuala ya kimkataba. Inaelezwa kuwa wachezaji hao walihitaji kupewa ada ya usajili shilingi mil 35 kila mmoja na kuongezewa mshahara.
Lakini Yanga wenyewe walikuwa tayari kuwaongezea mshahara bila kuwapa fedha za usajili. Kufuatia ishu hiyo Championi Jumatatu limezungumza na wachezaji wa zamani wa Yanga ili kupata maoni yao juu ya kuachwa kwa Yondani na Abdul.
ALLY MAYAI
Ally Mayai ni kati ya wachezaji ambao walicheza Yanga kwa mafanikio makubwa sana, ambapo kwa sasa ni mchambuzi maarufu na mahiri wa soka nchini.
Naye alipotafutwa azungumzue sakata hilo, alisema: “Ni vitu ambavyo kimsingi hutokea kwenye maisha ya soka, mchezaji kuachwa au kutemwa ipo kwenye kila timu.
“Lakini kwa upande wa Juma Abdul na Kelvin Yondani imekuwa kama imewagusa watu wengi kutokana na mazingira ambayo yanatajwa kuwaondoa wachezaji hao ndani ya Yanga.
“Viongozi kushindwa kuwapa kile ambacho wachezaji walikihitaji inaonekana kama siyo jambo lenye afya ndani ya Yanga, ukizingatia wachezaji wale ni wa muda mrefu na wamecheza Yanga kwa mafanikio makubwa. Hivyo wengi wanaona kama kuwakosea heshima wachezaji wale.”
USHAURI WAKO NI UPI KWA MABEKI HAO?
“Unajua ni ngumu kumpa mtu ushauri kama ukiwa haujui kwenye akili yake anawaza jambo gani. Lakini naweza nikasema wawe watulivu kama wanataka kuendelea kucheza soka timu zipo nyingi ambazo wanaweza kucheza na wakafanikiwa.”
EDIBILY LUNYAMILA
Lunyamila ni kati ya mawinga machachari wa wakati huo ambao walikuwa wanasumbua sana katika soka la Tanzania akiwa ndani ya jezi ya Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars.
Lunyamila naye hakusita kutoa ya moyoni juu ya usajili unaofanyika ndani ya Yanga na sakata la kuachwa wachezaji waandamizi wa kikosi hicho, Yondani na Abdul.
“Unajua haya ni matokeo ya mfumo mbovu ambao upo katika timu zetu za Tanzania. Kwa sababu hakuna sababu ya mchezaji ambaye umecheza kwenye timu kwa muda mrefu, ukahitaji fedha za usajili pindi linapokuja suala la kuongeza mkataba.
“Jambo ambalo kwenye nchi za wenzetu hawafanyi hivyo, kwa kawaida mchezaji anapotakiwa kuongeza mkataba, anatakiwa kuongezewa mshahara na siyo kupewa na ada ya usajili.
“Kwa hiyo ukitazama kwa mapana yake sakata la Juma na Yondani, unaweza ukasema Yanga wapo sawa, lakini wakati huohuo unaweza ukasema Yondani na Abdul wapo sawa.
“Sasa tukija kwenye nini maoni yangu juu ya sakata hili, Yanga walitakiwa kuwaelewa hawa wachezaji na kuwapa wanachohitaji kwa sababu ndiyo mfumo uliopo katika soka letu.”
UNAWAONA WAKICHEZA TIMU GANI MSIMU UJAO?
“Kwa kawaida ni ngumu sana kwa wachezaji ambao wametoka Simba na Yanga kukubali kwa haraka kwenda kucheza timu za mikoani. Lakini kwa hadhi ya Juma na Yondani nafikiri timu kama Polisi Tanzania na Azam zinaweza zikawafaa.”
USHAURI WAKO NI UPI KWA WADOGO ZAKO HAWA?
“Wakubali tu kuwa kuna wakati mambo yanabadilika na maisha lazima yaendelee, ingawa bado wanayo nafasi ya kurudi Yanga kama watakubaliana na kile ambacho viongozi wametaka.”
BAKARI MALIMA (JEMBE ULAYA)
Malima ni beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, ambaye aliwahi pia kucheza kwenye kikosi cha Simba miaka ya nyuma. Lakini kwa sasa anatambulika kama ‘Legend’ wa Yanga kutokana na kudumu kwa muda mrefu kwenye kikosi hicho.
Naye alikuwa na mchango juu ya sakata hilo: “Unajua kinapokuja kipindi cha usajili kuna mambo mengi hutokea, mfano kama hili la Yondani na Juma Abdul ni miongoni mwa matokeo ya kipindi cha usajili.
“Mara nyingi huangaliwa sana ripoti ya mwalimu, kama mwalimu aliacha ripoti kuwa wachezaji hao hawakuwa na umuhimu sana katika msimu ujao, inawezekana ndiyo maana viongozi hawakuweka mkazo wa kuwabakiza.
“Ukweli ni kwamba hawakutakiwa kuondoka, watu kama kina Ngassa, walitakiwa kuachwa kwenye kikosi ili kusaidia kwenye baadhi ya masuala kwa kuwa wao ni wachezaji waandamizi.”
MOHAMED HUSSEN (CHINGA)
Huyu ndiye anashikilia rekodi ya kufunga mabao 26 katika msimu mmoja akiwa na uzi wa Yanga. Lakini mbali na kucheza Yanga aliwahi kuvaa pia uzi wa Simba.
Kwa sasa ni kocha msaidizi wa Yanga Princesses akishirikiana na Edna Lema, alipotafutwa naye alikuwa na haya ya kusema: “Naweza kusema, ni vitu vya kawaida kwenye dirisha la usajili, kwa kuwa kwenye kila msimu kuna mabadiliko mengi hutokea kwenye vikosi mbalimbali.
“Lakini kwenye suala la hawa kina Yondani, lina mapana yake, kwanza hatujui kama ni kweli wameshindwana kwenye masuala ya fedha au mambo mengine yametokea ambayo viongozi wameshindwa kuweka wazi.
“Pia, tukija kwenye uhalisia wake sasa, hawakutakiwa kuondoka, tunaona wenzetu katika nchi zilizoendelea huko namna ambavyo wanaishi na kuwalea wachezaji wao, hasa wale ambao wamedumu na timu kwa muda mrefu na hata ikitokea wanaondoka kunakuwa na utaratibu maalumu.
“Wangepewa nafasi nyingine, kwani ukitazama uwezo wao bado haujaisha, lakini kingine kutokana na uzoefu wao wangeweza kushirikiana vema na benchi la ufundi katika kuweka mambo sawa katika timu.”
0 COMMENTS:
Post a Comment