ETIENNE Ndayiragije, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania amesema kuwa amekuwa akiwafuatilia wapinzani wake ambao atakutana nao uwanjani Oktoba 11 kwenye mchezo wa kirafiki uliopo kwenye kalenda ya Fifa, timu ya Taifa ya Burundi.
Tanzania ina kazi ya kumenyana na wapinzani hao ambao wanatarajiwa kutua leo Bongo saa 5:00 asubuhi kwa ajili ya maandalizi ya mwisho. Miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye kikosi kitakachotua leo ni Jonathan Nahimana, Bigirimana Blaise ambao wanakipiga ndani ya Klabu ya Namungo.
Stars imeingia kambini Oktoba 5 na jana Oktoba 6 ulifanyika uzinduzi rasmi wa jezi zitakazotumika kwenye mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Ndayiragije amesema:-"Nimewaita wachezaji kulingana na uwezo wao pamoja na wakati ambao tupo kwa sasa kwani hii ni mechi ya kirafiki lakini ina umuhimu kwa Taifa la Tanzania.
"Nina amini kwamba kwa muda wa maandalizi ambao tutaufanya pamoja na wachezaji waliopo tuna nafasi ya kupata matokeo, kikubwa ni kuona namna gani wachezaji watakuwa pamoja na mbinu ambazo tutatumia.
"Ninawatambua wapinzani wangu sio timu ya kubeza lakini haina maana ya kuhofia lazima tufanye vizuri na tunahitaji matokeo." amesema.
0 COMMENTS:
Post a Comment