CARLOS Carlinhos raia wa Angola, nyota mpya ndani ya Yanga, ameonekana kuivana na beki wa timu hiyo, Lamine Moro.Wawili hao kwenye michezo minne waliyocheza Yanga mpaka sasa, wameonekana kuwa na muunganiko mzuri ndani ya uwanja jambo linaloonesha kuwa wana jambo lao.
Muangola huyo alianza kuonesha cheche zake kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, wakati Yanga ikishinda bao 1-0, akitumia dakika 30 tu.
Carlinhos alitokea benchi akipishana na kiungo mzawa, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambapo aliweza kuonesha uwezo wake wa kupiga mipira ya faulo na kona. Katika mchezo huo, alipiga jumla ya kona tano na moja kati ya hizo ilizaa bao lililofungwa na Lamine.
Pacha hiyo pia katika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera wakati Yanga ikiifunga Kagera Sugar bao 1-0, mambo yalikuwa magumu kwao licha ya Carlinhos aliyetumia dakika 35 kupiga kona mbili na faulo mbili ambazo hazikuzaa matunda.
Waliporudi Bongo, wakajaza mafuta tena kuwafuata Mtibwa Sugar pale Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, pacha yao ilijibu ambapo dakika ya 61 Muangola huyo alipiga kona iliyoleta bao na mfungaji ni yuleyule, Lamine wakati Yanga wakishinda bao 1-0.
Hapa Muangala huyo alitumia dakika 72.Kwenye mechi tatu alizocheza Carlinhos, ametumia jumla dakika 137 akiwa na wastani wa kuwa na hatari kila baada ya dakika 45, huku Lamine aliyeyeyusha dakika 270 sawa na mechi tatu, akiwa na wastani wa hatari kila baada ya dakika 135.
Pacha ya Carlinhos na Lamine Moro imehusika kwenye jumla ya mabao mawili kati ya manne ambayo yamefungwa na Yanga kwenye mechi nne za ligi ambapo Carlinhos ametoa pasi mbili za mabao na ni kinara kwa watoa pasi ndani ya Yanga huku Lamine akiwa amefunga mabao mawili, ndiye kinara kwa watupiaji kikosini hapo licha ya kwamba ni beki wa kati.
0 COMMENTS:
Post a Comment