October 15, 2020


 WAKATI mizunguko mitano ya Ligi Kuu Bara (VPL) ikiwa imeshamalizika kwa sasa mzunguko wa sita unarejea ni wakati wa timu kuendelea kupambana kwa ajili ya kuhakikisha zinafanya vizuri zaidi.

 

Baadhi ya makosa ambayo yalionekana katika michezo iliyopita tuna imani yamefanyiwa kazi kwenye mapumziko hayo hivyo tunategemea kuona soka lenye ushindani zaidi tofauti na hapo awali.

Ligi inazidi kuwa yenye ushindani na ugumu kwa kila timu kupata matokeo ndani ya dakika 90 unaonekana. Jambo hili ni la muhimu na linapaswa kuendelea muda wote.

 

Makosa ambayo yamepita ni muhimu kuyafanyia kazi ili kusaidia timu kusonga mbele na malengo ya klabu kutimia kama yalivyopangwa, baada ya mapumziko mafupi ambayo yalitokana na ratiba iliyopo kwenye kalenda ya FIFA ambapo timu za taifa zilikuwa na mechi za kirafiki za kimataifa.

Tumeona kwamba Tanzania ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Burundi. Kweli kabisa haikuwa rahisi lakini hakuna namna ya kufanya kwa kuwa matokeo huwezi kuyabadili.

Kwa kilichotokea Uwanja wa Mkapa ni fundisho kwa timu na mashabiki kwamba mpira wa sasa umebadilika na anayepata ushindi ni yule ambaye amejipanga.

Kufanya makosa sio tatizo kinachotakiwa ni kuona namna gani timu inaweza kwenda kwenye mashindano ya kimataifa. Muhimu kuona wapi ambapo timu imekosea ili iweze kufanya vizuri wakati ujao.

Mashabiki kwa kujitokeza kwenu ni furaha kwa timu na ni muhimu kuendelea kwa kila mmoja kuendelea kufanya hivyo.

Ninaona kwamba wapo wale ambao wameanza kukata tamaa kwa ajili ya mechi iliyopita hapana bado tuna nafasi ya kufanya vizuri.

Kwa wale ambao waliitwa kwenye timu za taifa wanapaswa kuongeza juhudi ili wakati ujao pia waitwe tena kutokana na ubora ambao watakuwa nao kwa kuwa ligi inaendelea.

 

Endapo wakijituma zaidi itawasaidia katika kujitangaza katika soko la kimataifa kwani ni ndoto ya kila mchezaji kucheza nje ya nchi.

 

Kwa wale ambao hawakuitwa wana kazi ya kuendelea kuongeza juhudi ili wapate nafasi ya kuitwa katika timu zao za taifa, wasikate tamaa bali wanapaswa kukaza buti kwa ajili ya kutimiza malengo yao.

 

Upande wa Gadiel Michael, Juma Kaseja, na Mudathir Yahya wanapaswa kupambana kwani bado nafasi yao ipo ndani ya timu ya Taifa na hawapaswi kukata tamaa.

 

Pia wakati huu ligi ikiendelea zipo timu ambazo bado hazijawa na benchi kamili la ufundi lililokamilika hapa nazungumzia uwepo wa kocha mkuu ndani ya timu kutokana na changamoto za hapa na pale.

 

Timu hizo zinapaswa kukamilisha jopo lao la benchi la ufundi na kuwaleta kwa wakati unaotakiwa ili waweze kuendana na kasi ya Ligi.

 

Katika hilo ni wakati sahihi wa kuweza kuwapa kazi makocha ili waendeleze gurudumu la maendeleo ndani ya klabu katika kuhakikisha malengo ya klabu kiujumla yanatimia.

 

Ipo wazi kwamba msingi wa timu unahitaji kujengwa kwa sasa kabla ya wakati ujao ambapo mambo hubadilika ghafla na kupelekea mtafaruku.

 

Muhimu kwa timu ambazo zimewafukuza kazi makocha kutokana na sababu mbalimbali zikapata mbadala wake kwa wakati huu.

 

Kuna mengi ya kufanya akiwepo mwalimu kwenye benchi la ufundi itamfanya awe na kikosi imara na chenye nguvu ambacho kitampa matokeo mazuri.

 

Tusisahau kwamba tulikuwa kwenye mzunguko wa tano na sasa tunaingia mzunguko wa sita maana yake ni kwamba mambo yanakwenda kasi na timu zinaonyesha ushindani mkubwa.

 

Kasi hiyo itufanye nasi pia tubadilike ili tuwe sawa katika kile ambacho tunakifanya ndani ya uwanja hasa kwa kupata matokeo chanya ambayo pia yatawaridhisha wadau na mashabiki.

 

Timu zinazoshika nafasi ya 15 mpaka 18 ikiwemo Mbeya City zinapaswa kukaza msuli ili kuhakikisha hazirudii makosa yaliyofanyika katika michezo iliyopita.

Ukweli ni kwamba licha ya kuwa Mbeya City ipo nafasi ya 18 pia imekutana na timu ambazo zilikuwa kwenye ubora wake hivyo kwa wakati huu ni muhimu kuongeza makali kwenye safu yao ya ushambuliaji.Huku ikiongeza umakini kwenye safu ya ulinzi.

 

Zikitambua makosa yao zinapaswa zijirekebishe ili kufanya vizuri katika mechi zijazo kuanzia wakati huu na sio kusubiri mwisho wa msimu kwani mambo yanaweza kuwa magumu zaidi.

 

Kuna mechi nyingi hilo lipo wazi lakini haimaanishi kwamba mna nafasi ya kubweteka bali mnapaswa kuamka na kufanya vizuri kwani hakuna timu ambayo inahitaji kushuka daraja hivyo mtakwama mbele.

 

Malalamiko kwa waamuzi yalikuwa yamepungua kwa asilimia kubwa katika hilo basi pongezi zinastahili kwa waamuzi na Chama cha waamuzi baada ya kufanya kazi nzuri na kubwa.

 

Lakini msisahau kwamba michezo bado inaendelea hivyo msiboronge wakati ujao bali mnapaswa kujiimarisha zaidi katika kuhakikisha mnaondoa hata yale makando kando madogo.

 

Kwa upande wa wachezaji kuweni na nidhamu ndani ya uwanja kwani uwepo wa nidhamu utawafanya kuisaidia timu kufanya vizuri pamoja na uaminifu kwa kocha katika kuanza kwenye kikosi cha kwanza.

Nidhamu kwa mchezaji ni jambo la muhimu sana katika kuhakikisha anaweza kulinda kipaji alichonacho kwani bila nidhamu hawezi kufikia malengo aliyonayo.

Ishu ya kupoteza pia isitutoe kwenye reli kwa mashabiki wa timu ya Taifa ya Tanzania. Pia wakati mwingine kwa mechi za nyumbani ni muhimu kuongeza makali kwenye safu ya ushambuliaji kwani hapo ndipo tatizo lilipo.

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic