November 2, 2020


 LILIKUWA suala la muda tu kabla ya kuisikia hukumu ya mchezaji aitwaye Bernard Morrison. Tulikuwa na hakika kuwa atakumbana na adhabu baada ya kamera kumnasa akimpiga ngumi beki wa Ruvu Shooting, Juma Said Nyoso.

Kikao cha Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kilikaa tarehe 27 Octoba na kutoa adhabu kwa wachezaji na timu zilizovunja sheria. Hakuna aliyejali sana kuhusu adhabu ya wachezaji wengine isipokuwa ya Morrison.

 Huyu ni staa aliyevigombanisha vilabu vikubwa nchini isitoshe anatamba sana kwenye mitandao ya kijamii. Hivyo lazima kila anachokifanya kitolewe macho. Mpira wetu bwana!

 

Nadhani ni ngumi ya Bernard Morrison iliyowahisha kikao cha bodi ligi. Kikao kilikaa masaa ishirini na nne baada ya mechi ya Simba na Ruvu Shooting. Hatujaizoea bodi ya ligi kufanya mambo kwa haraka hivi.

 

 Hatujazoea. Bodi wakatumia nafasi hiyohiyo kupitia na matukio ya nyuma. Hakuna kosa kwenye kuwahi kutolea hukumu matukio ya uvunjifu wa sheria ila kuna kosa kwenye kuchelewa. Mfano, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons amefungiwa kutokucheza michezo mitatu kwa kosa alilolifanya mechi ya tarehe 22 Octoba dhidi ya Simba.

 

Adhabu imetoka tarehe Oktoba 27.  Hiyo inamaanisha Kimenya alikuwa huru kucheza mechi ya Oktoba 26 dhidi ya Dodoma Jiji. Hii inawanyima Dodoma Jiji faida ya Tanzania Prisons kumkosa Kimenya. Bodi ya ligi na kamati husika inabidi ipitie matukio  mapema na adhabu kutolewa mapema ili kutoa faida kwa timu zingine.

 

Ndiyo maana ikaitwa kamati ya masaa 72 na ‘siyo siku 72’.

Tukimgeukia ‘staa wa nchi’ bwana  Morrison, tunajifunza nini? Kwanza Morrison amegundua ligi yetu inaendeshwa ‘kishikaji’ na wachezaji wa baadhi ya timu ni wakubwa kuliko ligi. Haya matukio ya wachezaji kupigana yametokea mara kwa mara bila hatua kuchukuliwa.

 Morrison huyuhuyu akiwa Yanga, aliwahi kuachwa bila adhabu baada ya kumpiga kiwiko mchezaji wa Tanzania Prisons. Kwanini leo asirudie wakati anajua yeye ni mchezaji mkubwa na anacheza timu kubwa? Pili, huenda wachezaji wetu hawaandaliwi vema kwa mapambano ya kisaikolojia.

 

 Morrison alifikia hatua ya kurusha ngumi baada ya kukanyagwa kwa makusudi na Juma Nyosso. Huenda Nyosso alifanya vile kwa sababu anajua Morrison ni mwepesi kutolewa mchezoni, akaamua kumtafutia kadi kijanja. Kwa bahati mbaya mwamuzi hakuona tukio lote vema ila Morrison alishanasa kwenye mtego wa Nyosso. Huu ni ushahidi kuwa Morrison hakuandaliwa vema kukabiliana na matendo yasiyo ya kimchezo.

Rafiki yangu Shomari Lawi na yeye alikula rungu la kutokuchezesha mechi kwa mwaka mmoja kwa kushindwa kumudu mchezo wa Prisons dhidi ya Simba.

Swali dogo tu naweza kuuliza hapa, alishindwa kumudu mchezo kivipi? Kutokuona penalti mbili za Simba na ngumi ya Salum Kimenya? Inashangaza ukizingatia wasaidizi wake walikuwepo na hawajachukuliwa hatua yoyote.

 

Ningeweza kuielewa hii adhabu kama ingekuwa ni kashfa ya rushwa ila siyo kutokuona penalti ambazo hadi waamuzi wa Ulaya muda mwingine zinawashinda licha ya teknolojia wanayotumia.

Mwisho kabisa nimalizie kwa utani. Hii adhabu ya Shomari Lawi inatukumbusha kuwaheshimu watu na  kuwa na ujuzi wa kazi nyingine nje ya taaluma zetu. Fikiri mwaka mzima anaenda kufanya kazi gani? Usikute aliwahi kuwaambia watu kijijini kuwa mimi siwezi kuwa mkulima. Anaenda kufanya nini sasa? sina hakika na majibu yangu.

6 COMMENTS:

  1. Huna kumbukumbu ww Morrison alifungiwa wakati yuko Yanga sambamba na Jonas Mkude

    ReplyDelete
  2. Tifutifu imesheheni wanazi wa vilabu viwili tuu@ therefore maamuzi yanakuwa challenge!
    Tutabadilika lakini tutachelewa sanaaaa

    ReplyDelete
  3. Kuna 'hatari' ya taasisi zetu kukosa 'credibility' katika jamii.....

    ReplyDelete
  4. Refa kurudia kosa moja Mara mbili hayo Ni makusudi

    ReplyDelete
  5. Ameihujumu Simba refa kama alivyotuma, amepata mtaji wa kwenda kuanzia baada ya mwaka mmoja. Morrison kafungiwa mechi 3

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic