Anaandika Saleh Jembe
MARA zote tumekuwa
tukisema wazawazi kuhusiana na ubovu wa baadhi ya waamuzi wa Ligi Kuu Tanzania
Bara.
Hakika
wanaboronga na tunaona namna ambavyo tumekuwa tukifikisha malalamiko yetu
kwenye Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF).
Wako aina
tofauti ya wadau wa soka, wengine wanafikisha malalamiko hayo kwa lengo la
kulaumu tu ilimradi na hii inatokana na zile jazba wanazokuwa wanazipata
kutokana na kero ya waamuzi kutofanya vema.
Pia wako
wadau ambao wanafikisha kile wanachokiona kwa nia ya kujenga, wanataka kuona
mabadiliko yanakuwepo na haki inatendeka.
Sote
tunajua, kunapokuwa na haki, hakuna malalamiko. Yakiwepo, yanakuwa ni yale
yasiyokuwa na msingi na mara nyingi yanapotea kama upepo.
Bila ubishi,
malalamiko yamekuwa mengi kutokana na makosa na unaona wakati mwingine yanazua
hisia za rushwa na kadhalika. Hii inatengeneza ugumu sana katika maendeleo ya
mchezo wa soka.
Waamuzi
wanaovurunda hawatengenezwi au kusimamiwa kwa asilimia mia na TPLB au TFF,
badala yake wao wanawategemea wataalamu kutoka katika kamati ya waamuzi wenye
jukumu la kusimamia waamuzi sahihi wanaostahili kupata nafasi ya kuchezesha.
Hawa waamuzi
ili wapate nafasi na kukubaliwa na TPLB au TFF, lazima wataalamu kutoka katika
kamati ya waamuzi wawakubali. Sasa vipi viwango vyao vimekuwa hivi na nini hasa
kamati inakosa ili kuweka suala la ubora wa viwango kuwa sahihi?
Hawalipi
maanani? Lazima watasema wanalijali hilo. Lakini sasa vipi hawa waamuzi wa ligi
leo ndio mechi ya nane kwenda ya tisa malalamiko rundo.
Tumeona
tayari mwamuzi amefungiwa mwaka mzima na unaona adhabu yake ilitakiwa afungiwe
ikiwezekana aondolewe kabisa kuchezesha ligi kuu maana hakuwa na muda mrefu
tokea aboronge mechi kati ya Kagera dhidi ya Yanga na dhahiri hakutakiwa hata
kurudishwa.
Unaona pia
mechi kadhaa hapa, kumekuwa na makosa ya kimsingi na waamuzi wameendelea
kusumbuliwa na matukio ya kuotea ambayo katika hali ya kawaida yanaonekana
kabisa kuwa yanaepukika.
Mechi ya juzi
kati ya Simba dhidi ya Mwadui FC, kwa kuwa tu Simba si walalamishi sana lakini
pia inachangiwa na wao kushinda mabao 5-0 ndio maana hakuna aliyeyaona makosa
ya waamuzi.
Mabao
waliyofunga Simba yakaonekana walikuwa wameotea lakini ukirudia zile video za
tukio kwa msaada wa Azam TV, unaona kabisa hakukuwa na tatizo.
Hivyo hapa
unaweza kujifunza wakati mwingine kwamba pamoja ya kuwa kuna hofu ya suala la
kutokuwepo kwa uaminifu lakini unagundua pia ni suala la uwezo mdogo wa
utendaji wa kazi.
Ndiyo maana
nikasema kamati ya waamuzi inahusika kwa kiwango kikubwa licha ya kwamba
inakuwa imejificha nyuma ya pazia na sisi tukaendelea kuzichambua TFF na TPLB
kwa kuwa ndio wakubwa.
Ukiwa
mkubwa, kweli unapaswa kuwajibika hata kama utakuwa unawawakilisha wadogo zako.
Lakini ni vizuri mdogo naye akafanya kazi yako kwa ufasaha ili kuepuka
kumpelekea lawama nyingi huyo mkubwa.
Hapa
ninasisitiza kwamba kamati ya waamuzi inawajibika na uduni wa kiwango kutoka
kwa waamuzi hivyo inapaswa kujipanga na ikiwezekana kuwa na rekodi za uhakika
kwa wale wanaorudia matatizo.
Yaani iwe
hivi, kama kuna waamuzi wanaonekana kuwa na matatizo ya kujirudia na
yanayofanana, basi vizuri wakaondolewa na kuwe na wengine wanaoingizwa. Lakini
suala la uzalishaji wa waamuzi, pia lipewe kipaumbele ili kuwa na watu wengi wa
kutosha ili kuepuka kurudia watu wale wale wanaofanya makosa yaleyale.
Hiyo kamati ivunjwe inaonekana kazi wanapeana kishikaji
ReplyDelete