LIGI Kuu Bara pamoja na michuano mbalimbali iliyo chini ya
Shirikisho la soka Tanzania (TFF), imesimama kwa muda kupisha michezo ya
kimataifa iliyo kwenye kalenda ya Shirikisho la soka la kimataifa (FIFA).
Ipo michezo michache ya ligi hiyo ambayo kwa sababu maalum
imeendelea kuchezwa. Kwa mahali ambapo ligi imefikia unaweza kusema utamu
umezidi kuongezeka, hii ni kwa sababu huu ndiyo mzunguko wa kuweka sawa hesabu
na kuvuna matunda ambayo timu ziliyapanda tangu kuanza kwa msimu.
Ukiangalia msimamo wa ligi, utagundua kuwa vita ni kubwa sana
katika maeneo mawili ambayo ni kwa wale wanaochuana kusaka taji la ubingwa,
ambapo Simba na Yanga zinapewa nafasi kubwa licha ya kwamba Azam nao kwa sasa
hawapo mbali.
Lakini vita nyingine kubwa ni ile iliyopo chini mwa msimamo ambapo
zipo timu zinapambana kuhakikisha hazishuki daraja, bali zinasalia kuwa sehemu
ya ligi kwa msimu ujao wa 2020/21.
Kama ilivyokuwa mwaka jana, mwaka huu timu nne zitashuka moja
kwa moja huku mbili zikicheza hatua ya mtoano.
Hapa ndipo kasheshe linapoanzia, kwani kila mmoja anapambana
kutokuwa sehemu ya watakaopotea, bali anarudisha matumaini na kutetea eneo
analotoka. Katika hali kama hii, ishu ya umakini kwa wasimamizi wa ligi
inapaswa kupewa kipaumbele sana.
Hii ni kwa sababu zipo klabu ambazo zinaweza kuonewa kwa kuwa
tu zinakosa misuli katika hali zao za uwekezaji na uchumi.
Kwa bahati mbaya mara nyingi yanapotokea mambo kama hayo taaluma
ya Waamuzi hugusiwa zaidi, ambapo wamekuwa wakituhumiwa kushindwa kusimamia kwa
uhakika sheria 17 sa soka.
Hali hii kwa hapa nchini imedhibitiwa kwa kiwango fulani
kulinganisha na siku za nyuma, lakini bado kuna maeneo yanaonekana kulega, kuna
wakati msimu uliopita Waamuzi walishutumiwa sana kutokana na makosa ya
kujirudia katika kila mchezo.
Hali hii kuna wakati ilioanishwa na changamoto ya mazingira
ya kufanyia kazi, ikiwemo kukosekana kwa malipo ya stahiki zao kwa wakati, na
wakati mwingine mapungufu yao ya kibinadamu.
Ni kweli Waamuzi hawa sio Malaika hivyo, ni wazi wanaweza
kufanya makosa, lakini hata kama wanafanya makosa basi haipaswi kuwa ya
kujirudia.
Bado kuna changamoto ya ubora kwa waamuzi wetu, na hili
limekuwa likithibitishwa mara kwa mara na malalamiko mengi ya wadau wa soka
hapa nchini, na hata kupitia adhabu zitolewazo na bodi inayosimamia uendeshwaji
wa ligi kuu (TPLB).
Tujiulize tunawezaje kulipunguza kama sio kuliondoa kabisa
tatizo hilo, kwa kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo mafunzo, kuboresha
mazingira ya kazi, kuongeza vifungu vya adhabu kwa waamuzi watakaokiuka miiko
ya kazi.
Hii inaweza kutusaidia kuondokana na changamoto za maamuzi na
kutusaidia kuwa ligi iliyo bora. Hivyo chonde Waamuzi msiturudishe tulikotoka.







Edibili J. Lunyamila ni Mtu na nusu, walioingia kwenye ushabiki juzi juzi hawawezi kujua shughuli yake.
ReplyDelete