March 19, 2021




Saleh Ally

MOJA ya mambo yanayouangusha mchezo wa mpira nchini ni unafiki wa wadau wake wanaouzunguka.

 

Watu hawafanyi mambo kwa maslahi ya mpira wenyewe, wanafanya kila jambo kwa ajili yao, hali inayowafanya kuwa wanafiki kwa mambo mengi sana.

 

Wanasingiziana mambo, wanajengeana uadui, wanatumia visingizio vya ushabiki kuwaumiza au kuwasemea wengine mambo mabaya na haya mengi yanaendelea chinichini ndani ya mpira wa Tanzania.

 

Kitu kibaya zaidi ni wachache sana wanaoweza kusema ukweli na kuyazungumzia matatizo ya wanadamu hawa ambao ni wadau wa soka kwamba yanaukabili mchezo huu na inapaswa kubadilika.

 

Rais wa Awamu ya Tano, John Joseph Pombe Magufuli, ndiye pekee ambaye alikuwa chachu na akaweza kusema maneno mengi ya wazi na ukweli kama kiongozi.

 

Pamoja na kwamba ilikuwa ni mara ya kwanza anahudhuria katika mechi ya mchezo wa soka kama kiongozi mkuu wa nchi, Magufuli aliendelea kuonyesha kwamba yeye si mtu wa kubabaisha mambo na kama ni kusema ukweli, basi ni ukweli moja kwa moja bila ya kuhofia wala kuingiza siasa.

 

Ninaamini leo, Simba wanaishi na wanafanikiwa kupitia maneno ya Magufuli ambayo aliwaambia kuhusiana na ubora na namna ambavyo timu zimekuwa zikitolewa katika michuano mikubwa hasa ya Afrika.

 

Magufuli aliwaeleza Simba wakifungwa na Kagera Sugar bao 1-0 wakati tayari wakiwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara. Aliwaeleza wazi akisisitiza “Kwa kiwango hiki hamtafika popote.”

 

Aliwaambia anataka kombe la Afrika, akawaambia Simba kwamba amewaheshimu kwenda Uwanja wa Taifa wakati huo kuwakabidhi kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Lakini anatamani ubingwa wa Afrika na kuwataka Simba wawe wa kwanza kuuleta Tanzania. Haya maneno ni dawa ndani ya mioyo ya wachezaji, viongozi na hata mashabiki wa Simba.

 

Wanajua nini kinatakiwa sasa, wanajua inawezekana hata kama ilionekana haitawezekana au ni ngumu. Wanaelewa kwamba wao si wa kushindwa na hii inakuwa na mchango mkubwa hata katika mwendo wa Simba kwa sasa.

 

Tunaona mwendo wa Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika leo. Baada ya mechi nne za hatua ya makundi, hawajafungwa hata bao moja. Wakati misimu miwili iliyopita, walifungwa mabao 13 katika mechi tatu za ugenini.

 

Simba wamejifunza mengi kwa njia zao lakini somo la Magufuli limeendelea kuwa sehemu ya mabadiliko yao na huenda litawasaidia na wengine watapata nafasi ya kujifunza kwa kuwa sauti yake itaendelea kuishi.

 

Rais Magufuli hakuwa na uoga wa zile tabia za kinafiki za kutaka kuwafurahisha Simba na ukumbuke siku hiyo Simba walikuwa wengi uwanjani lakini akawaeleza ukweli bin haki kuhusiana na uhalisia.

 

Alieleza kwa nini hana timu Simba au Yanga, alisema ni kutokana na timu za Tanzania kutofanya vizuri au kufungwafungwa tu. Hivyo ikamkatisha tamaa kwa kuwa yeye si mtu anayependa kushindwa. Maana yake aliyakimbia maumivu ya kushindwa kwa kukaa mbali na ushabiki wa soka.

 

Nakumbuka alisimulia namna alivyokuwa akicheza soka shuleni, alikuwa fowadi, baadaye akaamua kuwa kipa lakini akaacha baada ya kulazimika kuvaa miwani akiona kutakuwa na ugumu kwake katika suala la uvaaji miwani wakati akidaka. Maana yake kweli alikuwa mwanamichezo ambaye baadaye maumivu ya kufeli, yalimkimbiza.

 

Magufuli ameondoka mapema, angekuwa dawa ya kudumu katika michezo nchini kwa ukweli wake, kutokuwa muoga wala unafiki wa wanamichezo kulikuwa msaada mkubwa kwa michezo nchini.

 

Angalia vyama vingi au mashirikisho ya soka, kuna mambo yamebadilika katika masuala ya uongozi au utendaji yamebadilika kabisa. Maana watu wamekuwa waoga na mwenendo wa maisha ya Magufuli yalivyokuwa kuhusiana na uongozi.

 

Hakuna anayeweza kupinga kwamba tumejifunza mengi sana na uwepo wake. Wakati mwingine Magufuli kuwepo kwake tu kulikuwa kunabadilisha mambo.

 

Wale ambao hawakuwa na uoga wa mali za umma au hofu ya kufuja mali za Watanzania, hii imekuwa ni kama kitu cha kawaida lakini wakati wake mambo yalibadiliika na watu wakawa waoga na faida ya mali za umma kwa umma wenyewe zikaanza kuonekana.

 

Tumejifunza mengi kutokana na muda wa Magufuli takribani miaka sita na michezo imefaidika lazima tukubali na tuseme ahsante sana Mungu na baada ya hapo tuendelee kumuombea kama sehemu ya shukurani kwake Mungu.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic