March 23, 2021


UMESIKIA huko mtaani kwamba wako wanaodanganyana kwamba kwa kuwa Rais John Pombe Magufuli hayupo tena madarakani, basi fedha zitapatikana kwa wingi.

 

Wajinga wengine wanawalaghai wengine lakini wanaolaghaiwa, hakuna hata mmoja anajibu sahihi kama utamuuliza kwamba fedha hizo zitapatikana vipi bila ya kufanya kazi.

 

Wanaofikiria fedha itapatikana tu kwa kulala ndani wanajidanganya, hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan hawezi kutoa nafasi hiyo na mwisho tutamlaumu tu.

 

Lazima kuchapa kazi ili kutafuta maisha yako, lazima kujituma na kupambana kupata kile kilicho sahihi na si kusubiri ulalamike tu au kuamini kufariki dunia kwa Magufuli na wepesi wa maisha yako.

 

Watu wa aina hii nimeamua kuwazungumzia kidogo kwa kuwa huku mitaani kwetu imekuwa gumzo kwa watu kuamini eti unafuu wa maisha umewadia. Fanyeni kazi, tuache longolongo.

 

Zaidi huku ni nilitaka kama kupita na kukumbushana tu lakini lengo hasa nilikuwa nimeamua kulenga kuhusiana na nidhamu ya uongozi michezoni ambayo imechangia mambo mengi makubwa.

 

Nidhamu hii ilipatikana wakati wa uongozi wa Hayati Magufuli, unaona karibu kila sehemu kwa maana ya sehemu mbalimbali kama klabu, mashirikisho au vyama vya michezo, suala la nidhamu katika uongozi ilikuwa juu.

 

Popote pale ambako kunakuwa na nidhamu, lazima kunakuwa na mafanikio na hasa katika suala la uongozi. Maana viongozi wanakuwa wanafanya vitu vyao kwa weledi, wanafikia malengo kwa utekelezaji bora unaolindwa na nidhamu ya kiuongozi.

 

Mwisho wa nidhamu ya kiuongozi ni kufikia malengo na baadaye kwenda katika mafanikio. Najua unanielewa kwa kuwa Rais Magufuli hakuwa anaongoza michezo. Lakini aina yake ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano, ulifanya kila sehemu waige na kuachana na zile tabia za uzembe, kuamini mashirikisho au vyama vya soka ni mali yao.

Badala yake, ile aina ya Magufuli ya utendaji uliotukuka kwa ajili ya wananchi ukasonga na kufanya vema, wengi wakiiga na mwisho umeona kuwa na mafanikio na mabadiliko makubwa ya kiuongozi.

 

Mfano, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limepata mafanikio makubwa katika timu za taifa kuanzia vijana U17, U20, timu zote za wanawake na hata ile kubwa.

 

Kushiriki Afcon kwa mara ya pili halikuwa jambo jepesi lakini Taifa Stars ikarejea tena Chan, mara ya mwisho ikiwa ni 2009 nchini Ivory Coast. Timu za wanawake za U 20, U17 zikabeba makombe yote Cosafa lakini pia Cecafa. Timu za vijana zikashiriki michuano mikubwa ya Afcon.

 

Tuwapongeze TFF, wamefanya kazi kubwa lakini pamoja na ubora wao lazima wakubali alama za nyakati zimewaongoza na kufanya haya makubwa ingawa kuna baadhi hawayaoni.

 

Tunajua Simba na Yanga wamekuwa wakifanya kazi kwa juhudi kubwa kwao, wanashindana wao lakini unaiona nidhamu ya uongozi wakijua Serikali ipo macho.

 

Mawaziri wa Michezo wamekuwa na nguvu sana katika kipindi cha Rais Magufuli, wamechangia wale waliokuwa wakifuja mali michezoni, wakifanya mambo kwa kubahatisha kuingia woga kwa kuwa wanatambua Serikali ipo.

 

Haya katuacha Rais Magufuli, hatupaswi kuyabwaga kibarazani halafu baadaye tuanze kumlaumu Rais Samia kwamba alichangia.

 

Tunatakiwa kuendelea kupita njia ileile ili kufanya mambo yaendelee kwenda na tukumbuke Magufuli ni mzazi au mwalimu. Alichokifundisha, kinatakiwa kuendelezwa na si inapokuwa hayupo, basi kife. Somo lake lilikuwa linaumiza kwa kuwa watu walizoea kuishi kwa mazoea lakini ukweli bila kificho umeonekana kwamba anachokitaka ni kweli na juhudi zake ni kuliongoza taifa kwa ufasaha na mafanikio na taifa lenyewe ni sisi.

 

Kama kweli tunaamini hakuwa mwanamichezo sana lakini kuna masomo alitupa na leo yamesaidia mabadiliko michezoni, basi sisi ni wanafunzi tulioiva na tunapaswa kufanya kilicho sahihi kuendeleza michezo.

1 COMMENTS:

  1. kwa mfano mkulima wa pamba, anafanya kazi halafu soko la uhakika halipo ,,,kutwa nzima serikali bize na kukusanya ushuru kwa wajasiria mali,,hata kile kidogo tuchopata kinarudi serikalini lini tutainuka ?,,, mlala hoi na ndege wapi na wapi ? mtuletee basi hata madawa kwny vituo vya afya.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic