Saleh Ally
Yanga
wamecheza mechi 23 na kukusanya jumla ya ponti 50. Pointi hizo zinawafanya wao
kuwa kileleni lakini hofu ni walio katika nafasi ya pili, watani wao Simba
ambao wana pointi 46 baada ya kucheza mechi 20.
Ukiangalia
tofauti ya pointi nne tu na michezo ni mitatu, kama Simba atashinda yote,
atakuwa ameiacha Yanga mbali. Kwa Yanga hili ni jambo linalowachanganya.
Kwamba baada
ya muda mfupi wataondoka kileleni na kama ni hivyo wataing’oa vipi tena Simba
kileleni na hasa kuhusiana na suala la kiwango cha wenyewe Simba itakuwaje na
hakuna ubishi kwa aina ya uchezaji wao, wako vizuri zaidi.
Hii presha
inatembea ndani ya viungo vya Yanga na kuifanya wakati mwingine kujilazimisha
kufanya vitu nje ya mwendo wake ambayo ni hatari zaidi.
Kwa Kocha wa
muda, Juma Mwambusi yeye lazima atakuwa na presha kwa kuwa amekichukua kikosi
kikiwa kimecheza mechi sita na kupata sare nne, kikashinda moja na kupoteza
moja. Hiki ndicho kilimfanya Kocha Cedric Kaze raia wa Burundi atupiwe virago
vyake.
Kwake
Mwambusi lazima atakuwa anataka kuanza ligi na ushindi lakini ukweli,
inawezekana kukawa na ugumu katika hili kwa kuwa bahati mbaya ligi imelazimika
kusimama kwa muda mrefu kutokana na mapumziko yaliyotokana na msiba wa Rais
John Pombe Joseph Magufuli.
Timu
inapokaa muda mrefu bila ya kucheza, hata kama inaendelea na mazoezi, bado
itakosa match mentality na match fitness. Maana yake wakati kikosi cha Mwambusi
kinarejea katika ligi, basi kitakuwa ndio kinajijenga.
Yanga kuanza
kujijenga kutokana na mechi zinazoendelea kunaweza kutengeneza presha zaidi.
Mfano angalia mechi ya kwanza dhidi ya KMC, haiwezi kuwa mechi nyepesi na
unakumbuka mara ya mwisho wawili hao walipokutana, KMC walilalama kuonewa.
Angalia
baada ya hapo Yanga wanakwenda kukutana na Biashara United, timu ambayo unaweza
kusema ukiacha timu za Dar es Salaam, inaonekana kuwa ndio timu imara zaidi
inayotokea nje ya mkoa huo kwa timu za Ligi Kuu Bara.
Kama
itatokea Yanga wataanza vizuri mechi dhidi ya KMC kwa kuwa ushindi, basi hii
itakuwa msaada mkubwa sana kwenda katika mwendelezo wa mechi nyingi kwa kuwa
itaamsha morali na ile hali ya hamu ya kushinda itaendelea.
Bahati
waliyoipata Yanga, katika mechi zao nne zinazifuatia, zote hawatalazimika
kusafiri, zote watakuwa nyumbani na hii ni nafasi kubwa kwa kusimama.
Ikitokea pia
Yanga wakafanikiwa kushinda mechi zao zote nne zinazofuatia. Basi watakuwa na
nafasi ya kufanya vema zaidi katika mechi nyingine zinazofuatia ingawa si
uhakika wa asilimia mia itakuwa hivyo.
Mwambusi
inabidi ajiandae, kwamba kwa kuwa mechi ndio zinaanza na wao walisimama kwa
muda mrefu na bahati mbaya hakuna hata nafasi ya kucheza mechi za kirafiki
kwenye viwanja vya ushindani, basi litamsumbua.
Ikitokea
limemsumbua jambo hili, lazima ajipange na kupambana. Mashabiki na mambo ya
ufundi, ni wachache wao sana. Wengi wanachotaka kama ilivyo kwa mashabiki
wengi, wanataka kushinda na hakuna mjadala.
Mashabiki
wanachojua ni timu yao kushinda na unaona ndio maana nilisema Mwambusi ameingia
wakati mbaya. Kwamba mashabiki watakacholenga ni kwamba, kwa kuwa Mwambusi
amerejea kama kocha mpya, watataka kuona timu yao inashinda tu.
Presha kwa
Yanga haiwezi kushuka leo au mapema, lazima kuwe na subira kutoka katika kila
pande kwamba kuibadilisha hii hali, katikati yake lazima kuwe na maumivu.
Na presha kubwa kwa Yanga ni pale unapoona kiongozi Mkubwa tena wa kutegemewa anasimamishwa kazi na kupigwa faini kubwa kwa kutumia uongo na kukosa nidham ni aibu kubwa sana na huku timu ikiutaka ubingwa, vipi itakuwa morali ya wachezaji unaitegemea na huku kwa watani kumetulia wakikata mbuga. Kweli inatuvunja moyo
ReplyDelete