HASHIKIKI! Hivyo ndivyo utakavyosema kwa kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula ambaye ameingia kwenye tano bora ya makipa wenye ‘clean sheet’ katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mechi sita za hatua ya makundi msimu huu, Simba imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili na inashika nafasi ya pili katika chati ya timu zilizoruhusu mabao machache hatua hiyo.
Simba imeruhusu mabao hayo kwenye mchezo dhidi ya AS Vita uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, uliomalizika kwa timu hiyo kushinda 4-1, kabla ya kwenda kufungwa 1-0 na Al Ahly, Cairo, Misri
Katika mechi hizo, golini alikuwepo Manula.
Orodha ya makipa wenye clean sheet nyingi zaidi msimu huu hatua hiyo ni Moussa Camara (Horoya) na Ahmed Reda Tagnaouti (Wydad Casabalnca) ambao kila mmoja ana nne, wenye tatu ni Aishi Manula (Simba), Ali Abdullah Abou (Al Hilal) na Mohamed El-Shenawy (Al Ahly).
Akizungumzia hilo, Manula alisema: “Kwangu najisikia furaha kuwepo katika orodha ya makipa wenye rekodi nzuri ya kutoruhusu mabao.
“Pongezi nyingi ziende kwa wachezaji wenzangu na benchi la ufundi lote linaloongozwa na Kocha Gomes (Didier) ambaye amekuwa akiniamini na kunipa maneno ya kuniongezea nguvu ili niwe bora zaidi.
“Bado nina kibarua kigumu mbele ya safari baada ya kufanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hii na kikubwa ninataka kuendeleza rekodi nzuri ya kutoruhusu mabao,” alisema Manula.
0 COMMENTS:
Post a Comment