April 4, 2021


 MAPUMZIKO ambayo yapo kwa sasa kwa timu za Tanzania yanapaswa yatumike vizuri ili kuweza kurejesha nguvu mpya ya ushindani kwa timu zote.

Sababu kubwa ya mechi kusimama inatokana na maombolezo ya msiba wa aliyekuwa Rais wa awamu ya tano wa Tanzania, John Pombe Magufuli.


Tayari Magufuli ambaye alipumzishwa kwenye makazi yake ya milele Machi 26, mwendo wake ameumaliza tunajukumu la kumuombea apumzike salama.


Kwa yale ambayo ameyatenda ni muhimu kumuenzi kwa vitendo. Kuanzia kwenye familia ya michezo pamoja na masuala ya kijamii kiujumla ni muhimu kuwekeza nguvu kubwa katika kutenda yale ambayo alikuwa akipenda kuona yanatokea.


Ameondoka wakati taifa la Tanzania likiwa linahitaji huduma yake na hata Afrika kiujumla bado ilikuwa inahitaji mchango wake kwenye utendaji kazi.

 

Hakuna namna nyingine ya kufanya zaidi ya kushukuru kwa yote kwa sababu ni kazi ya Mola na kilichotokea hakiwezi kubadilika.


Rekodi yake nzuri katika kutekekeleza majukumu yake imebaki kwenye vichwa vya wengi. Matendo yake mema yanaishi kwenye vichwa vya Watanzania pamoja na Afirika kiujumla.


Basi jukumu letu ni moja kufanya yale mazuri ambayo ni faida kwa Tanzania na ulimwengu kiujumla. Kwa upande wa timu ambazo zinashiriki mashindano ya kimataifa aliacha ujumbe kwenu.


Agizo lake la kuona kwamba siku moja ardhi ya Tanzania inapokea kombe la Afrika bado inaishi. Hii inapaswa ifanyiwe kazi na timu zote ambazo zinashiriki kwenye mashindano ya kimataifa.

Atakumbukwa kwa kupenda kusema kweli daima. Aliwaambia mabingwa wa Ligi Kuu Bara Simba waziwazi kwamba ikiwa wataendelea kucheza mpira kama ambavyo walicheza wakati wakifungwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar hawataweza kubeba ubingwa wa Afrika.


Ilikuwa ni kauli ya kishujaa tena yenye mamlaka kwa kuwa alikuwa anapenda kutibu palipo na tatizo na alijua kwamba aina ya mpira ambao Simba walicheza mbele ya Kagera Sugar haukuwa kwenye viwango.

 

Bado hotuba yake inaishi na ina maneno mengi ambayo ni maagizo yanapaswa yafanyiwe kazi na timu zote Tanzania sio Simba pekee wala Namungo.


Ikumbukwe kwamba aliweka wazi kwamba alikwenda Uwanja wa Mkapa kushuhudia mchezo wa Simba na Kagera Sugar kwa ajili ya heshima kwa mashabiki na Watanzania kiujumla.


Hapa pana kitu kawaachia viongozi wengine kwamba ni lazima wawe na heshima kwa Watanzania katika utendaji wa mambo yao.


Yapo majukumu mengine ambayo wanapaswa wayafanye kwa ajili ya upendo na heshima kwa Watanzania. Hii ni muhimu kuanzia kwa wachezaji, mashabiki pamoja na viongozi katika sekta zote.


Namna ambavyo alikuwa akifundisha kwa vitendo iwe somo kwetu kwa sasa kutenda hayo mambo aliyokuwa akiyatenda kwa vitendo kwa kuwa shujaa ameumaliza mwendo.


Msukumo wake wa kupenda kuona mambo yakitokea uwaguse pia wale ambao kwa sasa timu zao zinapambana kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja.


Zile timu ambazo zimekuwa zikipata matokeo ya kusuasua wakati huu ni wao kuanza kuwa na msukumo mpya na hesabu tofauti katika kusaka matokeo uwanjani.


Itasaidia na kurejesha ule morali ambao ulikuwa umeanza kuondoka kwa wachezaji. Wapo wale ambao wanashindwa kuonyesha uwezo kwa kuwa bado hawajalipwa stahiki zao hawa wanapaswa watimizizwe madai yao.


Wapo wachezaji ambao wamekata tamaa bado wana deni la kurejea kwenye ubora na kutimiza majukumu yao ipasavyo.


Ukweli ni kwamba ili timu ipate pointi tatu iwe ni kuanzia kwenye Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Kuu Bara pamoja na Ligi ya Wanawake Tanzania ni lazima ishinde mechi zake itakazocheza.


Na kwa kuwa tupo mzunguko wa pili wa kukamilisha hesabu kwa timu zote kazi imeanza kuonekana ngumu kwa baadhi ya timu ambazo hazina matumaini ya kubaki kwenye ligi msimu ujao.


Ushindani mkubwa unaoonekana kwenye mzunguko wa pili unapaswa kuwa chachu kwa zile ambazo hazijawa kwenye mwendo mzuri kubadili mbinu za kushindana.


Inatakiwa kuwa endelevu ili kuifanya ligi yetu kuwa imara. Kila timu zinapaswa kutimiza majukumu huku zikiendelea kumkumbuka shujaa Magufuli.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic