UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kuwa unahitaji pointi tatu muhimu kesho kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United ya Mara utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex majira ya saa 1:00 usiku.
Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu, George Lwandamina imekuwa kwenye mwendo mzuri kwa sasa ambapo imetoka kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 mbele ya KMC katika mchezo wa mzunguko wa kwanza.
Mchezo wa mzunguko wa pili walipokutana Uwanja wa Azam Complex ubao ulisoma Azam FC 2-1 KMC huku mtupiaji wa bao la kwanza alikuwa ni Prince Dube na lile la ushindi lilifungwa na Agrey Morris.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit, amesema kuwa wapo tayari kwa mechi zote ambazo zimebaki ili kufikia malengo ambayo wamejiwekea.
"Kwa sasa kwa kila mechi ambayo tutacheza tunahitaji pointi tatu na baada ya hapo tutajua nini tumekikusanya baada ya ligi kukamilika ila kikubwa ni ushindi," amesema.
Kwenye msimamo Azam FC ipo nafasi ya tatu imekusanya pointi 57 baada ya kucheza mechi 29 inakutana na Biashara United iliyo nafasi ya nne na pointi 45 baada ya kucheza mechi 29.
0 COMMENTS:
Post a Comment