WADHAMINI wa Simba, Kampuni ya Michezo na Burudani ya SportPesa, leo wameikabidhi timu hiyo hundi ya Sh 100 Mil kama bonasi baada ya kutwaa taji la Ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Simba imefanikiwa kutwaa ubingwa huo kwa mara ya nne mfululizo kwa kufikisha pointi 83 huku Yanga wakiwa wa pili wakifisha 74 katika msimamo wa ligi.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mkurugenzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa SportPesa, Abbas Tarimba amesema kuwa pongezi nyingi ziende kwa Simba baada ya kufanikiwa kuutetea ubingwa wao kwa mara ya nne mfululizo.
Tarimba amesema kuwa bonasi hiyo ni sehemu ya motisha kwa wachezaji wa Simba katika kuongeza morali ya kupambana uwanjani.
“Kama wadhamini tunajisikia fahari kuona moja ya timu tunayoidhamini ikifanya vizuri kwa maana ya kututangaza kitaifa na kimataifa kutokana na ushiriki wao wa mashindano ya kimataifa.
“Hivyo kama ilivyokuwa sehemu yetu ya makubaliano yaliyokuwepo katika mkataba, tumetimiza majukumu yetu kwa kuwapa Simba bonasi ya Sh 100Mil baada ya kuchukua ubingwa wa ligi msimu huu.
“Na hivi sasa tupo katika mazungumzo mazuri na Simba katika kuongeza mkataba mpya baada ya huu wa awali kumalizika, mwaka huu,” amesema Tarimba.
Akipokea hundi hiyo, Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amesema kuwa anaipongeza SportPesa kwa kutimiza makubaliano yaliyokuwepo katika mkataba waliongia nao kwa kipindi cha miaka minne.
“SportPesa wanastahili pongezi kwa kufanikiwa kutimiza makubaliano yaliyokuwepo katika mkataba ikiwemo sehemu ya bonasi.
“SportPesa walianza kutupa bonasi ya Sh 50Mil baada ya kufanikiwa kufika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na hii ni mara ya pili kwao kutupa Sh 100Mil za ubingwa wa ligi.
Kwa niaba wa wachezaji, beki wa Simba Gadiel Michael amesema kuwa “Tuchukue nafasi hii kwa kuwashukuru SportPesa kwa udhamini ambao wamekuwa wakitupa unatupa morali, hivyo tuahidi kuendelea kupambana kwa ajili ya kuwatangaza SportPesa kimataifa," .
0 COMMENTS:
Post a Comment