July 29, 2021

LIGI Kuu Soka Tanzania Bara msimu wa 2020/21  Jumapili iliyopita iliumaliza mwendo baada ya michezo yote tisa ya mzunguko wa 34 kupigwa katika viwanja mbalimbali hapa nchini.

Michezo hiyo ndiyo ilitoa taswira halisi ya kundi la timu ambazo zilikuwa zinapigana vikumbo kujiondoa katika hatari ya kushuka daraja. 

Bila shaka Ligi ya msimu huu imekuwa na mafanikio makubwa kulinganisha na misimu iliyopita, ambapo tumeshuhudia ushindani mkubwa kwa klabu zote shiriki.

Kwa hili nadhani Uongozi wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), na Bodi ya Usimamizi wa Ligi Kuu Tanzania (TPLB), unastahili pongezi kubwa kwa mafanikio haya na yale ambayo yanaendelea kuonekana katika mchezo wa soka kupitia uongozi wao.

Ni jambo lisilopingika kuwa, kuongeza kwa ushindani huu kwa kiasi kikubwa ndiyo sababu ambayo imekuwa ikifanya wawekezaji waanze kufikiria kufanya uwekezaji mkubwa kama ambavyo tumeona kupitia mkataba wa haki ya kurusha matangazo ya michezo ya Ligi Kuu Bara ambao TFF na Kampuni ya Azam Media wameingia.

Uwekezaji huu unatarajiwa kuwa chachu ya kupambana kwa timu shiriki kwa msimu ujao wa 2021/22, ambao unatarajiwa kuhusisha timu 16.

Licha ya mafanikio haya makubwa, TFF na TPLB wana kazi kubwa ya kufanya marekebisho katika baadhi ya maeneo ambayo bado yanaonekana kulega hasa katika suala zima la upangaji wa ratiba.

Ishu ya matatizo ya upangaji wa ratiba imekuwa kisiki kigumu kuking’oa kwa misimu mingi kwenye ligi yetu, ambapo mara kwa mara kumekuwa na malalamiko yasiyoisha juu ya baadhi ya klabu kuonekana kupendelewa huku vingine vikiumia kutokana na sintofahamu ya upangaji wa ratiba.

Uthibitisho wa hili ni mapumziko mawili ambayo ligi imelazimika kuyaendea ndani ya kipindi cha mwezi mmoja uliopita, ambapo kabla ya mapumziko ya kupisha michezo ya kimataifa mwezi Mei, mwaka huu kulikua na mapumziko ya kupisha ratiba ya michezo ya viporo pamoja na ile ya hatua ya robo fainali ya kombe la Shirikisho.

Hali hii imekuwa ikiwaacha na sintofahamu kubwa wadau wengi wa soka hapa nchini, ambao wamekuwa wakijiuliza maswali mengi kuhusiana na utaratibu ambao umekuwa ukitumiwa na Bodi ya Usimamizi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), katika mchakato mzima wa upangaji wa ratiba.

Mapungufu yanayoonekana kwenye ratiba yetu na sababu zinazotajwa kutetea mapungufu hayo kuna wakati zinafikirisha. Kuna wakati mnaweza kuambiwa viporo hivi vinatokana na baadhi ya timu kuwa na michuano ya kimataifa, hivyo ratiba zao kuahirishwa mara kwa mara.

Hapa ndipo ambapo TPLB wanapaswa kutuliza akili kuelekea msimu ujao wa 2021/22 ambapo Tanzania Bara itakuwa na wawakilishi wanne kwenye michuano ya kimataifa ambao ni; Simba, Yanga, Azam na Biashara United.

Sasa kama tutaendekeza sababu za ajabu za uwepo wa michuano ya kimataifa kuwa chanzo cha kuharibu ratiba, kwa idadi ya wawakilishi wanne kimataifa bila shaka ligi yetu ya msimu ujao inaweza isiishe.

Hivyo mabadiliko ya haraka yanapaswa kufanyika kuelekea msimu ujao, ili kuepukana na bomu linaloweza kutokea kutokana na mrundikano wa mechi.

 

 

 

 

 

 

 

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic